Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jecha Salim Jecha. |
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imekamilisha awamu ya kwanza ya kazi ya uchunguzi wa idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi Zanzibar baada ya kupokea maoni mbali mbali ya wadau Unguja na Pemba.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alipokuwa akizungumza na waandishi habari ofisi za ZEC, Maisara mjini Unguja jana ambapo alisema, kinachofanyika hivi sasa ni kuyachambua maoni yaliotolewa katika mchakato huo uliochukuwa karibu miezi mitatu.
Alisema katika utaratibu huo wa kupokea maoni ya wadau juu ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi, ZEC ilikutana ana kwa ana na kupokea maoni ya vyama vya siasa 14 vikiwemo vya CCM na CUF huku vyama vyengine vinane viliwakilisha maoni yao kwa maandishi.
Alizitaja taasisi nyengine zilizotoa maoni ni pamoja na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wawakilishi wa Asasi mbali za kijamii pamoja na wananchi.
Alisema maoni makuu yaliosikilizwa na kupokelewa na tume ni pamoja na matatizo ya mipaka ya majimbo katika wilaya, wadi za uchaguzi na mipaka ya shehia, matatizo ya majimbo yatokanayo na mgawanyo wa hali ya jiografia, ongezeko la idadi ya watu katika majimbo ya wilaya na maoni ya jumla ya wadau.
“Yapo baadhi ya majimbo yenye idadi kubwa ya watu na mengine yakiwa na idadi chache na kukosekana kwa uwiano katika mgawanyo wa majimbo uliopo hivi sasa,” alisema.
“Watu wanazaliana, mamlaka zinapeleka huduma, lakini ni vyema kukawepo uwiano wa kuwahudumia,” alisema.
“Katiba haijasema kuwa lazima jimbo lizingatie idadi ya watu, lakini inataka kuangaliwa uwiano na ZEC itazingatia hilo,” alisema.
Alisema ZEC haijakaa kwa lengo la ukataji au upunguzaji wa majimbo ya uchaguzi na kwamba kinachofanyika ni uvumi unaoenezwa na watu wachache kwa maslahi binafsi.
“Ni uvumi na hofu za wanasiasa, ZEC haijafanya uamuzi huo kwa sasa,”alisema.
Naye Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, alisema, kazi hiyo inaendeshwa kwa matakwa ya katiba ambayo inaelekeza kufanyika kila baada ya miaka minane hadi 10 ambapo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2005 ikiwa sasa ni miaka tisa tokea Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilipofanya uchunguzi wa idadi, mipaka na majina ya majimbo ya uchaguzi.
Alisema, kulikuwepo na changamoto mbali mbali juu ya zoezi hilo la ukusanyaji wa maoni ikiwemo baadhi ya maeneo watu kuonekana kuwa na jazba za kisiasa.
“Watu walikuja kama vile ilivyokuwa wakati wa ukusanyaji wa maoni ya katiba mpya ya Tanzania, lakini, mishowe walituelewa na kufanikisha kazi yetu.
Juu ya mchakato huo kuhodhiwa na wanasiasa, alisema,ZEC imejidhatiti kufanikisha mchakato huo kwa kuzingatia matakwa ya katiba na kwamba haitokuwa na nafasi ya kwenda kinyume na matakwa hayo kwa maslahi ya taifa na wananchi wake kwa ujumla.
“Mtaji wa wanasiasa ni wapiga kura, huo ndio uhalisia, lakini si katika hili,” alisema.
Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa baadhi ya majimbo yenye idadi kubwa ya watu likiwemo jimbo la Fuoni lenye watu zaidi ya 60,000, Dimani watu 58,000 na Dole lenye idadi ya watu karibu 35,000.
“Haya ni baadhi ya majimbo yenye idadi kubwa ya watu, lakini, yapo yenye idadi chache likiwemo jimbo la Rahaleo, Chambani na Mgogoni,” alisema.
No comments:
Post a Comment