Mkutano wa jana ulikuwa na sehemu mbili kuu, wa
kwanza ulifanyika katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma ambako viongozi hao
walikutana na Rais Kikwete na mwingine katika Hoteli ya St. Gasper ambao
uliwashirikisha viongozi na maofisa wa vyama vilivyoshiriki bila Rais
Kikwete.
Mkutano huo ni matunda ya jitihada zinazofanywa na
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho kiliratibu mazungumzo hayo
yaliyochukua zaidi ya saa mbili na nusu, katika Ikulu ya Kilimani,
wakati yale ya St. Gaspar yalichukua takriban saa moja na nusu.
Viongozi walioshiriki kikao hicho cha Ikulu ni
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Philip Mangula, Katibu Mkuu wa
chama hicho, Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod
Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara),
Magdalena Sakaya.
Wengine ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James
Mbatia, Katibu Mkuu wake, Mosena Nyambabe, Mwenyekiti wa TLP, Augustine
Mrema, Mwenyekiti wa UDP ambaye pia ndiye mwenye zamu ya uenyekiti wa
TCD, John Cheyo na Mwenyekiti wa UPDP pamoja na mwakilishi wa vyama
visivyokuwa na wabunge ndani ya TCD, Fahmi Dovutwa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Rais
Kikwete baada ya kuanza kwa kikao hicho alitoa fursa kwa kila
aliyekuwapo kuzungumza na hapo zilijitokeza hoja mbalimbali, nyingi
mwelekeo wake ukiwa ni kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu ili kutoa
fursa kwa nchi kuendelea na masuala mengine makubwa.
Chanzo chetu kilisema: “Rais amekuwa msikivu
kweli, amewasikiliza wote lakini ugumu ulianza kuonekana pale
ilipotolewa kauli ya kuwauliza wale watu wa Ukawa kama wanaonaje
wakirejea halafu hoja zao zikazungumzwa ndani ya Bunge Maalumu, yaani
hawataki kabisa kusikia hilo.”
Kuhusu hoja ya kusitishwa kwa Bunge, habari
zinasema ilijadiliwa kwa kirefu na wataalamu wa sheria wakijaribu kutoa
uzoefu wao, lakini kikwazo kilichoonekana ni Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba ambayo haimpi Rais mamlaka ya kusitisha Bunge.
“Rais alisema hoja zao ni nzuri na zina mashiko,
lakini suala kubwa likawa ni kwamba tunafikaje huko wanakopendekeza?
Maana sheria iko kimya kuhusu mamlaka ya Rais kusitisha Bunge Maalumu,
ndiyo maana sasa tulitoka Ikulu tukaenda St. Gaspar ili kujadili, ngoja
tusubiri hiyo tarehe 8 maana siyo mbali,” alisema mmoja wa wajumbe wa
kikao hicho.
Kauli ya TCD
Baada ya kikao cha St. Gasper, Mwenyekiti wa TCD,
Cheyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba mazungumzo na Rais Kikwete
yalikuwa mazuri na kwamba wamekubaliana kukutana naye tena Septemba 8,
mwaka huu baada ya kuwa wamezifanyia kazi hoja ambazo zilijitokeza
kwenye vikao hivyo.
“Kama nilivyowaambia siku ile tulipokutana,
tulikuwa na ajenda mbili tu kubwa, kwanza ni mchakato wa Katiba Mpya
unavyokwenda na ajenda ya pili ni jinsi tunavyoweza kusonga mbele na
kuwa na maandalizi ya uchaguzi mzuri mwakani,” alisema Cheyo lakini
akikataa kujibu maswali mengine ya waandishi wa habari.
Cheyo alisema baada ya kukutana na Rais Kikwete, waliendelea na
kikao cha viongozi wa vyama kwa ajili ya kuona jinsi ya kuyafanyia kazi
mambo yaliyojitokeza, hivyo wameamua kuunda kamati ndogo ya watu wanne
itakayoongozwa na Mbatia kwa ajili ya kutekeleza wajibu huo.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Kinana, Profesa
Lipumba na Dk Slaa ambao wamepewa wajibu wa kuwasilisha ripoti yao
kwenye kikao cha wenyeviti wa vyama vinavyounda TCD ili ijadiliwe kabla
ya kikao cha Septemba 8, ambacho hata hivyo, hakijafahamika kitafanyika
wapi.
Habari zinasema miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa
kazi ni pamoja na kuona kama Bunge linaweza kusitishwa bila kuleta
athari zozote za kisheria na kisiasa, lakini wakizingatia uwapo wa
makundi mengine ndani ya Bunge hilo hasa wabunge wa kuteuliwa kupitia
kundi la 201.
“Lakini hapa kuna suala moja kwamba Ukawa wako nje
ya Bunge, ni vigumu kuwaamrisha wale walioko ndani ya Bunge ili
watekeleze matakwa yao, kwa hiyo kuna kazi kubwa sana ya kufanya,”
kilisema chanzo chetu.
Mgomo wa Ukawa
Dalili za Ukawa kukataa kurejea bungeni zilianza
kuonekana mapema baada ya mazungumzo yasiyo rasmi ambayo yalifanyika
katika moja ya kumbi za Hoteli ya Dodoma ambako walikwenda kupata chai
baada ya kuwasili.
Wakati wakitoka kwenye ukumbi huo kuelekea Ikulu
Kilimani, baadhi yao walisikika wakipeana tahadhari kwamba wasikubali
wazo la kurejea bungeni, ambalo ni dhahiri walikuwa wamepewa wakati
wakinywa chai.
Baadaye ndani ya basi dogo wakati wakielekea
Ikulu, Lissu alisikika akisema: “Eti wanataka turejee, yaani tumekaa nje
muda wote huo halafu leo hii tuje hapa kujadili kurudi, eti kurudi
haiwezekani kabisa.”
Pia habari kutoka katika Ukumbi wa St. Gaspar
zinasema hata katika kikao hicho, viongozi hao walishauriwa kurejea
bungeni ili hoja za kuahirishwa kwa Bunge Maalumu zitolewe huko, lakini
waligoma.
Taarifa zinasema Ukawa walijenga hoja kwamba Bunge
Maalumu halipaswi kuendelea kwa sababu kuna kila dalili kuwa muda
uliopo hautoshi kukamilisha mchakato na ikizingatiwa kwamba nchi
inakabiliwa na mambo mengi ukiwamo Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Pia kulikuwa na hoja kuhusu mambo ya Daftari la
Wapigakura na mabadiliko ya sheria ambazo zinagusa taasisi kama Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, sheria mbalimbali zinazihusu vyama vya siasa na mambo
ya matokeo ya rais kuhojiwa nadhani,” kilieleza chanzo kingine.
Kushindwa kupatikana kwa suluhu ya mchakato wa
Katiba, kunaendelea kuuweka mchakato huo njiapanda hasa ikizingatiwa
kwamba Bunge Maalumu linaendelea kesho kupokea ripoti za kamati kuhusu
uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba.
Nukuu
“Eti wanataka turejee, yaani tumekaa nje
muda wote huo halafu leo hii tuje hapa kujadili kurudi, eti kurudi
haiwezekani kabisa.” Lissu
No comments:
Post a Comment