Jaji Joseph Sinde Warioba. |
Katika waraka wa maandishi alioutuma kwa gazeti hili, Jaji Warioba
alisema maelezo ya Wasira dhidi yake katika mahojiano maalumu na gazeti
hili hayakuwa sahihi na hivyo akamtaka ajifunze kusema ukweli kwa kuwa
mambo anayosema yanaweza kumrudia baadaye.
Waraka wenyewe
Tarehe 22 Septemba 2014, Gazeti la Mwananchi lilitoa taarifa ya
mahojiano kati yake na Mheshimiwa Steven Wasira. Katika mahojiano hayo,
Mheshimiwa Wasira alisema mimi ndiye niliyemkimbiza CCM.
Tangu mchakato wa Katiba Mpya kuanza nilikuwa napata taarifa kwamba
Mheshimiwa Wasira alikuwa amenifanya mtaji wake katika kutetea msimamo
wake. Wakati mmoja kuna kiongozi mwenzake aliniuliza kama nina ugomvi
binafsi na Mheshimiwa Wasira kwa sababu kila akipata nafasi kwenye vikao
vyao ananishambulia. Wakati wa mabaraza ya Katiba nilipata taarifa za
aina hiyo. Nilichofanya ni kuwaarifu viongozi wake wa CCM.
Mengi aliyosema Mheshimiwa Wasira siyo ya kweli. Napenda nitoe ufafanuzi kwa machache yafuatayo:-
Niligombea mara mbili na Mheshimiwa Wasira. Baada ya Uchaguzi wa 1990
ambao nilishinda kwa kura nyingi sana, uchaguzi huo ilitenguliwa kwa
sababu nilifanya kampeni kwa kutumia gari la Waziri Mkuu.
Uchaguzi ulirudiwa mwaka 1992. Niliunda timu ya kampeni, Mheshimiwa
Wasira akiwa kiongozi. Aliniomba atangulie jimboni kuandaa mazingira.
Alipofika huko akaanza kampeni dhidi yangu na kutangaza kwamba
anagombea. Wakati huo kura za maoni zilikuwa zinapigwa na wajumbe wa
halmashauri kuu ya wilaya.
Wajumbe walikuwa kama 600. Nilipata kura 400 na Mheshimiwa Wasira alipata kura chache akiwa mtu wa tatu au nne. Baada ya matokeo akatangaza anajitoa kwenye mchakato na jina lake lisipelekwe NEC. Alikataliwa kwa sababu kufuatana na kanuni, muda wa mtu kujitoa ulikuwa umepita.
Wajumbe walikuwa kama 600. Nilipata kura 400 na Mheshimiwa Wasira alipata kura chache akiwa mtu wa tatu au nne. Baada ya matokeo akatangaza anajitoa kwenye mchakato na jina lake lisipelekwe NEC. Alikataliwa kwa sababu kufuatana na kanuni, muda wa mtu kujitoa ulikuwa umepita.
Mwaka 1995, kura za maoni zilikuwa zinapigwa kwenye kata. Tulianza na
Kata ya Sarama ambayo iko upande wa mashariki, siku ya tatu tulifika
Nyamuswa ambacho ndicho kijiji ninachotoka. Nyamuswa ilikuwa kituo cha
tano kati ya vituo 12.
Baada ya hapo tulielekea magharibi ya jimbo anakotoka Mheshimiwa
Wasira. Baada ya kura kupigwa katika Kata ya Guta, Mheshimiwa Wasira
alijitoa kwa sababu aliona hawezi kunishinda hata kama angepata kura
zote za kata mbili zilizobaki. Siyo kweli kwamba Nyamuswa ilikuwa ya
mwisho kupiga kura na siyo kweli wananchi wa kata nzima walipiga kura.
Kumbukumbu zote zinaweza kupatikana wilayani na makao makuu ya CCM.
Mheshimiwa Wasira anasema kwamba nilikuwa Jaji na kesi iliyopelekwa
mahakamani ni kama kesi ya tumbili kupelekwa kwa nyani, kwa maana kwamba
majaji walinipendelea. Kumbukumbu za kesi hiyo zipo. Wakati huo sikuwa
jaji. Isitoshe huko nyuma uchaguzi nilioshinda 1992 ulitenguliwa. Kwa
nini wakati huo sikupendelewa? Kumbukumbu za kesi zinaeleza kwa nini
Mheshimiwa Wasira alifungiwa kugombea kwa kipindi.
Mheshimiwa Wasira ni kiongozi wa Taifa kwa kipindi kirefu. Ni mbunge
wangu na namtambua hivyo. Tunaweza kuwa na mtazamo tofauti katika baadhi
ya mambo lakini hiyo si sababu ya kusema mambo yasiyo ya kweli kwa nia
ya kujijenga kisiasa.
Yeye ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM. Yeye ni
Waziri mwandamizi. Yeye anafikiria kugombea urais. Ni vizuri basi
akajifunza kusema kweli (ambayo ni ahadi mojawapo ya WanaCCM). Akumbuke
anayosema yanaweza kumrudia mbele ya safari.
J.S. Warioba
24-09-2014CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment