Saturday, 6 September 2014

Mwanasheria Mkuu SMZ ajiuzulu Kamati ya Uandishi,

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Othman Masoud Othm
Dodoma. Kuna dalili hali si shwari ndani ya Bunge Maalumu la Katiba baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman kujiuzulu ujumbe wa Kamati ya Uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

Habari za uhakika zilizopatikana jana bungeni mjini Dodoma, zinaeleza kuwa kigogo huyo wa SMZ amemwandikia barua Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta akimwarifu juu ya uamuzi wake huo.

Kamati hiyo ndiyo moyo wa Bunge hilo katika kuandika vifungu, ibara na sura za rasimu kulingana na mapendekezo ya kila kamati na baada ya majadiliano na mwisho inawajibika kuandika Katiba itakayopendekezwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Kujiengua kwake ni pigo kwa Bunge Maalumu, kwani kunapunguza uhalali wa Katiba itakayopendekezwa kwani Othman akiwa Mwanasheria Mkuu wa upande huo wa Muungano ndiye anayepaswa kuwa kinara wa kulinda masilahi ya Zanzibar wakati wa uandishi wa Katiba inayopendekezwa.

Jana Othman alilithibitishia gazeti hili kuhusu kujiuzulu kutoka kwenye kamati hiyo, lakini akakataa kueleza sababu zilizomsukuma kuchukua uamuzi huo akitaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu atafutwe kwani barua yake ya kujiuzulu ameikabidhi kwake.

“Ni sahihi kwamba nimejiuzulu…hizo sababu ndiyo siwezi kukutajia maana kwa mujibu wa taratibu za Bunge Maalumu zinapaswa kuzungumzwa na Mwenyekiti maana barua yangu ya kujiuzulu anayo yeye,”alisema Othman alipozungumza na gazeti hili kupitia simu yake ya mkononi jana.

Hata hivyo, Sitta alipotafutwa jana, alikataa kuzungumza lolote juu ya taarifa hizo akisema hawezi kufanya mahojiano na mwandishi asiyemfahamu kwa njia ya simu.

“Kwanza sikujui halafu unataka nifanye mahojiano kwenye simu? Mimi sipo (Dodoma), nipo Dar es Salaam ninarudi Jumatatu niliondoka huko (Dodoma) mara tu baada ya kipindi cha asubuhi,” alisema Sitta.

Kwa upande wake, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, alipotafutwa alisema hajaiona barua hiyo ya Othman, lakini kwa utaratibu, mjumbe anayetaka kuchukua uamuzi kama huo humwandikia barua mwenyekiti ndipo ishuke chini.

“Mimi bado sijapata taarifa hiyo, labda atakuwa amewasilisha kwa mwenyekiti akishaipata ndiyo inaletwa huku kwangu,”alisema Hamad.

Alisema kwa sababu nafasi hizo ni uteuzi unaofanywa na mwenyekiti na kanuni ziko kimya kuhusiana na idadi ya wajumbe katika kamati, mwenyekiti ndiye mwenye uamuzi wa kuteua mtu mwingine ama kuacha.

Habari hizo zilieleza kwa mara ya mwisho, Othman aliingia katika kikao cha Kamati ya Uandishi Jumanne na tangu siku hiyo hakuhudhuria vikao na hata jana wajumbe walikutana Ukumbi wa Pius Msekwa bila ya kigogo huyo kuhudhuria.

Vyanzo hivyo vimelidokeza gazeti hili kuwa sababu kubwa ya kujiondoa katika kamati hiyo ni kutokana na kutoridhishwa na hali ya mambo katika uandishi wa ibara za katiba kama zilivyopendekezwa na kamati 12 za Bunge Maalumu.

Habari hizo zinadai, Othman alisikika akiwatahadharisha baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, nje ya vikao juu ya athari za wajumbe wa kamati za Bunge, kuamua kuifumua rasimu iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Alitahadharisha juu ya kubadili maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyoandikwa kwa misingi ya serikali tatu na kuiandika kwa misingi ya serikali mbili kuwa itakuwa na athari huko baadaye,” alidokeza mmoja wa watoa habari.

Kujiuzulu kwa Othman kumekuja wakati Bunge hilo likiwa limegawanyika vipande vipande baada ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuamua kususia vikao vya Bunge hilo tangu Aprili 16, mwaka huu.

Sababu inayotajwa na Ukawa ya kususia vikao hivyo, ni hatua ya Bunge hilo kuamua kuacha kujikita katika kujadili na kuboresha Rasimu ya Katiba na badala yake kuifumua upya ili kuingiza masilahi ya CCM.

Hata hivyo, pamoja na wajumbe wa Ukawa kususia, Bunge hilo limeendelea na vikao vyake huku jitihada za kutafuta maridhiano zikielekea kukwama kutokana na kila upande kushikilia msimamo wake.

Kadhalika baadhi ya wajumbe ambao pia ni makada wa CCM wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba wamekuwa wakipinga kuendelea kwa Bunge hilo kwa maelezo kwamba litakosa uhalali wa kisiasa, huku kukiwa na hofu ya kutopatikana kwa idadi ya theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar.

Sitta, mara zote amenukuliwa akijitetea kuwa Bunge hilo halijatoka nje ya msitari na kwamba kinachojadiliwa ndani ya Bunge hilo ni Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na siyo vinginevyo.

Kamati ya Uandishi inajumuisha wajumbe 24 wakiwamo watu wazito na inaongozwa na Mwanasheria Mkuu mstaafu, Andrew Chenge na mjumbe mwingine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema na wanasheria mbalimbali waliobobea katika taaluma ya sheria.

CHANZO: MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment