Mtuhumiwa wa kesi ya ugaidi mkoani Arusha, Abdallah Maginga, ameiomba
Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo, kumruhusu kutohudhuria siku za
kesi na abaki magereza kutokana na maumivu makali anayopata sehemu za
siri alikodai kuminywa na polisi, pamoja na kuingiziwa mti sehemu ya
haja kubwa.
Mshtakiwa huyo alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Devota Msofe.
“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako inipe ruhusa ya kutohudhuria
siku ya kesi, sababu ninapopanda gari napata maumivu makali sana sehemu
za siri kunauma, kwa sababu polisi walinitesa kwa kuniingizia mti kwenye
haja kubwa na kuminya sehemu zangu za siri,” alisema.
Alidai kuwa mbali na maumivu ya sehemu za siri pia mguu wake uliokatwa hospitalini bado una maumivu makali.
Maginga pia aliiomba Mahakama iagize Magereza wamruhusu akatibiwe
hospitalini, kwani alitakiwa kwenda kupata matibabu Septemba 5 mwaka huu
lakini amezuiwa hadi sasa.
Akijibu ombi hilo, Hakimu Msofe, alisema suala la kwenda mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi kumpa ruhusa hiyo.
Pia alimshauri mshtakiwa huyo kuwa kama ana maelezo mengi amweleze
hakimu anayesikiliza kesi yake Mustapher Siyani, ambaye kwa siku hiyo
hakuwapo.
“Sikiliza Maginga suala la kuja mahakamani ni lazima na sio hiyari
wala majadiliano, ila kuhusu kwenda hospitalini liwasilishe Magereza
ndiyo mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema hakimu huyo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao wameshtakiwa kwa
makosa yaliyo chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi Namba 22 ya Mwaka 2002 na
kwamba upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya
kuisikiliza na kutoa uamuzi.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na kundi la Al-Shabaab.
Mbali na mashitaka hayo pia wanahusishwa na tukio la mlipuko wa bomu
lililotokea katika baa ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha
kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.
Washtakiwa hao ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti (yupo wodini
Hospitali ya Mount Meru), Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemed,
Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa, Swalehe Hamisi,
Abdallah Yasini, Abdallah Maginga na Sudi Nasibu Lusuma.
Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni Shaban Musa, Athuman
Hussein, Mohamed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohamed na Said Michael Temba .
CHANZO: NIPASHE,
No comments:
Post a Comment