Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama cha Wananchi CUF Omar Ali Shehe. |
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Omar Ali Shehe, alisema siyo kweli kuwa baadhi ya majimbo yakiwamo Magogoni na Chambani Kisiwani Pemba kuwa na idadi ndogo ya watu kwani suala hilo linahitaji utafiti zaidi.
“Idadi ndogo ya wananchi isiwe kigezo cha Tume ya Uchaguzi kupunguza majimbo, mbona Tanzania bara kuna Jimbo la Mafia ambalo lina wakaazi 13,000 na linafahamika kama jimbo?” alihoji Omar.
Alisema ni vyema tume hiyo kufuata katiba na sheria, hivyo ipo haja ya kuongeza majimbo na siyo kupunguza majimbo.
Alisema kuwa endapo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) itapunguza majimbo haitokuwa na uadilifu na upo uwezekano mkubwa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015 kutokuwa huru na wa haki.
“CUF inahisi tume haina nia njema katika zoezi hilo, kama tume hiyo itaamua kupunguza majimbo hasa ya Pemba,” alisema.
Afisa Habari na Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Dadi Kombo Maalim, alisema Chadema hakijashawishika na upunguzaji au uongezaji wa majimbo kwani wanahisi majimbo 50 yaliopo yanatosheleza.
Alisema bado wana mashaka na ZEC katika utaratibu wa ugawaji wa majimbo, hivyo ipo haja kwa tume hiyo kuepukana na mizozo isiyokuwa ya lazima.
“Fedha zinazotumika katika ukusanyaji wa maoni kuhusu mgawanyo wa majimbo ni fedha za wananchi, hivyo fedha hizo zisifanyiwe ubadhirifu,” alisema Dadi.
Licha ya mtazamo huo wa vyama vya siasa, ZEC ilisema bado haijaamua kupunguza au kuongeza majimbo na sasa ipo katika utaratibu wa kukusanya na kuchambua maoni yaliowasilishwa kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salum Jecha, alisema tume yake itafikia maamuzi kutokana na mapendekezo ya wadau na kuwataka wananchi wasubiri maamuzi ya tume.
No comments:
Post a Comment