Ushauri huo umetolewa bungeni mjini Dodoma jana na Askofu Amos Mhagachi akisema ni vyema masuala ya dini, yakaachwa kwa taasisi za dini ili kusiwepo muingiliano na Serikali.
“Kila dini ina utaratibu wake kwa mfano, suala la kujua idadi ya waumini wa dini husika, kila Mchungaji tukimpa kazi ya kuongoza lazima atuambie ana wakristo wangapi,” alisema.
Aliongeza kuwa, ukristo ni mfumo uliojitosheleza wenyewe hivyo ili nchi ibaki salama, isijihusishe na masuala ya kidini basi shughuli za kidini zijiendeshe zenyewe chini ya taasisi zake.
Askofu Mhagachi alisema kanisa lilijitenga na shughuli za kiserikali tangu karne ya 16 kwenye miaka ya 1,525 hadi sasa.
“Tangu hapo, kanisa liliamua kumtegemea Mungu pekee likiachana na Serikali…shughuli za kikabila na dini zikiruhusiwa kwenye Katiba, kutakuwa na kutoelewana baina ya wananchi,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa ripoti ya maendeleo ya haki za watu na taasisi za dini ya Novemba 2011 pamoja na tafiti alizofanya, nchi zinazoongoza kwa misingi ya dini duniani ndizo zinaongoza kuvunja haki za binadamu.
“Tukiruhusu dini iingie katika hili, lazima kutakuwa na uonevu kwa wale ambao hawaamini katika dini fulani…suala la dini tuliache kama lilivyo ili nchi iendelee kuwa salama,” alisema.
Mwakilishi wa Kundi la Wavuvi, Issa Suleiman, alisema suala la Mahakama ya Kadhi si la kikabila bali kinachopaswa kuangaliwa ni uwepo wa wanasheria wanaojua sheria za dini ya Kiislamu katika Mahakama ya Rufaa.
“Mahakama iliyopo sasa inazungumzia sheria kwa ujumla hivyo Muislamu anapokata rufaa kwenda mahakama ya juu, hamna wanasheria wanaojua hizo taratibu,” alisema.
Aliwataka viongozi wote wa dini, wakutane na kamati ya uongozi ili watatue kero za uwepo wa Mahakama ya Kadhi zilizojitokeza.
No comments:
Post a Comment