Mansour alijiunga na CUF baada ya kuvuliwa uanachama wa CCM, Agosti
mwaka jana kwa tuhuma za usaliti na kwenda kinyume na sera za chama
hicho, hivyo kupoteza nafasi yake ya uwakilishi wa Jimbo la
Kiembesamaki.
Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Salum Abdallah
Bimani alisema Mansour ameteuliwa kushika wadhifa huo kuanzia Agosti 27,
mwaka huu hadi utakapofanyika Uchaguzi Mkuu mwingine wa Taifa wa CUF
mwaka 2019.
Bimani alisema majukumu ya Mansour ni kuratibu mipango na mikakati ya
kisiasa na kuhakikisha CUF inafikia malengo yake ya kushika madaraka
kwa njia za kidemokrasia.
Alitaja sifa za mwanasiasa huyo kuwa ni mwanaharakati, mchapakazi na
mpenda mabadiliko na kwamba hivyo amekabidhiwa jukumu hilo akiaminiwa
kuwa ni kiranja atakayefanikisha malengo hayo kwa weledi na ushupavu.
“Siku zote (Mansour) hufanya jambo analoliamini bila ya kusukumwa,
analolisimamia huzaa matunda bila ya kusukumwasukumwa, ni jasiri na
hodari,” alisema Bimani.
Alisema kikao cha Kamati ya Uongozi cha CUF kilichokaa hivi karibuni
na kuwakutanisha wajumbe 300 wa wilaya sita za Unguja, kilitambulishwa
nafasi mpya ya Mansour.
Alisema madhumuni ya mkutano huo ilikuwa ni kuwatambulisha viongozi
wapya wa Kamati ya Utendaji Taifa ya CUF ambayo itafanya kazi kuelekea
Uchaguzi Mkuu ujao.
Mansour alithibitisha uteuzi huo lakini hakuwa tayari kuzungumza chochote.
Mwanasiasa huyo ameshiriki katika mikakati ya kampeni za uchaguzi za
vipindi vitatu akiwa CCM wakati wa Rais mstaafu, Amani Abeid Karume na
kushiriki kikamilifu katika kampeni za Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein.
No comments:
Post a Comment