Tuesday, 16 September 2014

Bunge la Katiba lachafuka

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba Ally Kessy.
BUNGE la Maalum la Katiba jana lilikumbwa na msukosuko mkubwa baada ya Mjumbe wa Bunge hilo, Ally Kessy, kuwavuruga wabunge kutoka Zanzibar akiwatuhumu kutafuna fedha za walipakodi wanyonge wa Tanzania bila sababu, huku akitaka kila upande wa nchi ubebe msalaba wake wenyewe.

Akichangia sura za rasimu ya Katiba bungeni mjini Dodoma jana, Kessy aliwatuhumu wabunge kutoka Zanzibar kuendelea kunufaika na fedha za Muungano, huku akitaka sasa Katiba Mpya itamke wazi kuwa kila Taifa lijitegemee lenyewe kwa kila kitu ili kuondoa manung’uniko ya upande mmoja kunyonywa.

Kessy alisema haoni sababu ya wabunge kutoka Zanzibar kuendelea kuhudumiwa kwa kulipwa mishahara na marupurupu mengine kutokana na fedha za Serikali za Muungano na kutaka kila upande uhakikishe unachangia mapato kwenye Muungano.

Hatua hiyo ya Kessy ilisababisha Bunge hilo kuchafuka, huku wajumbe kutoka Zanzibar wakiwasha vipaza sauti na kupiga kelele kutounga mkono kauli za Mjumbe huyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini mkoani Katavi (CCM), hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kukubali ombi la miongozo kutoka kwa wajumbe wengine kusahihisha kauli hiyo ya Kessy.

Wajumbe wengi kutoka Zanzibar wakifafanua kauli hiyo, walisema ni tabia ya Mjumbe huyo (Kessy) kuwatukana Wazanzibari katika Bunge hilo, huku wakisisitiza kuwa ana ajenda ya siri inayomsukuma kufanya hivyo.

Walisisitiza kuwa muundo wa Bunge la Muungano linaundwa na pande mbili za Zanzibar na Tanzania Bara.
Hali hiyo pia ilimsukuma kusimama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda, ambapo alisema kuwa Bunge Maalum la Katiba limefanya kazi kubwa kwa kuheshimiana na kujenga hoja za msingi, hivyo kunapotokea vitendo kama hivyo alivyofanya Kessy vinapaswa kudharauliwa kwa ajili ya kujenga mustakabali mwema wa Taifa.

Naye Mjumbe wa Bunge hilo kutoka Zanzibar, Mahamoud Thabit Kombo, alisema Bunge hilo limekuwa likiendelea vizuri na kwamba kero nyingi za Muungano zimekuwa zikishughulikiwa hivyo kitendo hicho hakipaswi kuvumiliwa kwani kinachangia kuleta mgawanyiko.

Kwa upande wake, Hamad Rashid Mohamed, alisema Kessy anapaswa kutambua kuwa si kweli Zanzibar inashindwa kujitegemea kwani imekuwa na mchango mkubwa wa kusaidia mataifa mengi ikiwemo ya Kiarabu, huku Tanzania Bara nayo ilishawahi kukopeshwa fedha na Zanzibar.

Hamad alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa undugu wa damu, hivyo hakuna sababu ya kujenga taswira ya kuonesha kuwa kuna tatizo kwani hata katika vita vya kumwondoa Idi Amin, askari wengi wa KMKM Zanzibar walitumika katika vita hivyo na wengi walipoteza maisha.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bunge hilo, Stephen Wassira alisema Kessy anapaswa kuwa makini na kauli zake anazotoa kwani hata vita huwa vinaanza kwa kauli ya mtu mmoja, hivyo kusiwepo mambo ya kuwagawa watu.

Alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukutokana na utajiri bali ni Muungano wa watu si fedha.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Sitta alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo, Kessy amezivunja kwani zinakataa mjumbe yeyote kutoa kauli za kuchafua wengine huku akitaka kuwaaminisha wananchi kuwa wengine ni tegemezi kitu ambacho amesema si sahihi na kumtaka kuomba radhi kwa kauli hiyo.

Wakati akiomba radhi Kessy alisema hakuzungumza kuhusu kuvunja Muungano, bali alitaka Katiba Mpya kuweka Muungano usio na manung’uko ila kutokana na kauli hiyo kutofurahisha wengi alilazimika kuomba radhi.

No comments:

Post a Comment