Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad
alipotakiwa kueleza idadi kamili ya wajumbe wa Bunge hilo wanaotarajiwa
kuwa nje ya nchi na jinsi watakavyopiga kura.
Juzi, Bunge hilo lilizifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwaruhusu
wajumbe watakaokuwa nje ya Ukumbi wa Bunge wakiwamo wanaokwenda Hijja
kuipigia kura Katiba inayopendekezwa, iliyokabidhiwa kwa Kamati ya
Uongozi jana.
Chini ya marekebisho hayo, mjumbe aliye nje ya Bunge, ataruhusiwa
kupiga kura ya wazi au ya siri kwa njia ya fax au mtandao kama
itakavyoelekezwa na katibu kwa kushauriana na mwenyekiti.
Hamad alisema hadi kufikia jana mchana walikuwa wamewatambua wajumbe
wanane ambao watakwenda Hijja huko Uarabuni lakini orodha ya watakaokuwa
nchi nyingine bado haijajulikana.
Hamadi alisema ofisa wake huyo atasimamia kura za wajumbe wanaokwenda
Hijja katika upigaji kura unaotarajiwa kuanza Septemba 29 hadi Oktoba 2
mwaka huu.
Alisema ni vigumu kutaja vituo watakavyopigia kura sasa kwa sababu
bado hawajawauliza wajumbe wengine waliopo nje ya nchi ambao wangependa
kupiga kura wakiwa huko.
Kuhusu iwapo watapiga moja kwa moja kwa mtandao au watapiga kwenye
karatasi na kutoa vivuli, Hamad alisema suala hilo litaamuliwa na Kamati
ya Uongozi ya Bunge chini ya Mwenyekiti, Samuel Sitta.
Ukawa wapinga
Wenyeviti wenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Profesa
Ibrahim Lipumba na James Mbatia wamelishukia Bunge hilo kwa kuruhusu
upigaji kura nje ya nchi.
Akizungumza jana, Profesa Lipumba alisema kilichofanywa na Sitta na
wajumbe wake ni uchakachuaji unaoweza kuliingiza Taifa kwenye mgogoro
mkubwa.
“Kwanza taratibu za kura mabunge ya Jumuiya ya Madola ni kura zote
zinapigwa ndani ya Bunge.Unapozungumzia akidi imetimia ni wajumbe walioko ndani ya Bunge,” alisema Profesa Lipumba.
Kanuni mpya ya 30 (1) baada ya marekebisho yaliyofanyika juzi
inasomeka, “Akidi kwa kila kikao cha Bunge Maalumu itakuwa ni nusu ya
wajumbe wote wa Bunge Maalumu.”
Awali, kanuni hiyo iliweka sharti la lazima kwamba akidi ya kikao
itakuwa ni nusu ya wajumbe, isipokuwa kwa kikao kinachohusu kupitisha
uamuzi wa Bunge Maalumu.
“Mwenyekiti hawezi tu kutangaza kuwa akidi imetimia kwa sababu
nimepata barua kuna wajumbe wako nje kwa hiyo watapigia kura huko. Ni
uvunjifu wa sheria na taratibu ulio wazi,” alisisitiza.
“Hakuna maridhiano lakini zaidi ya hapo huu mchakato wote
umeshaharibika. Kinachofanyika hapo ni Sitta kujaribu kuhalalisha
matumizi ya Sh20 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo,” alisema.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema
kinachofanywa na Sitta ni kuhakikisha wanatoka na Katiba hata kama haina
uhalali wa kisiasa.
“Kwa hiyo inabidi lazima atoke na kitu ili aseme tumepitisha uamuzi
tumetoka na Katiba hii ili kuhalalisha matumizi,” alisema Lipumba na
kuhoji uharaka huo wa Sitta ni wa nini?
“Kama muda hautoshi kwenda kwenye kura ya maoni kulikuwa na sababu
gani ya kuendelea na mchakato huo. Mchakato wa Katiba unakwenda katika
utaratibu wa sheria,” alisema.
Profesa Lipumba alisema sheria iko wazi na iliweka utaratibu kuwa
baada ya kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, isipite siku zaidi ya
120 bila kura ya maoni kufanyika.
“Ni wazi sheria yenyewe itabidi ibadilishwe. Rais atakayekuja akiwa
makini hawezi kukubali kuanza na Katiba iliyowagawa Watanzania. Rais
gani atakubali kuanza na migogoro ya kisiasa?” alihoji Lipumba.
“Waziri wa Katiba wa SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) hashiriki,
AG (Mwanasheria Mkuu) wa Zanzibar hashiriki Katiba ya nchi, watu wa
Zanzibar hawashiriki utasemaje ina uhalali wa kisiasa?”
Mbatia alisema anamshangaa Sitta kujigamba kutoka na Katiba
inayopendekezwa wakati itakwenda kukaa kabatini kusubiri utashi wa rais
ajaye.
“Hatuna kura ya maoni kwa hiyo haiwezi kutumika. Kwa hiyo
ikishapokewa inawekwa kabatini. Rais ajaye ni mwingine, sisi tunaendelea
na mikakati yetu ya marekebisho ya 15 ya Katiba,” alisema.Kuahirishwa kwa kura ya maoni kunatokana na makubaliano kati ya viongozi wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Jakaya Kikwete yaliyofikiwa Septemba 8, mwaka huu.
CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment