Rais Jakaya Mrisho Kikwete. |
Hiyo ni kutokana na muda uliopangwa kwenye ratiba ya bunge hilo kuzua
utata wa kisheria na kuwapo uwezekano wa mwingiliano na Bunge la
Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar.
Ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba inaonyesha kuwa limepanga
kuhitimisha vikao vyake mwishoni mwa Oktoba, tofauti na tarehe
iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete Julai 28, mwaka huu ambayo
ilitangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 254 la Agosti Mosi.
Tangazo la Rais linaonyesha kuwa awamu ya pili ya Bunge Maalumu
ingeanza Agosti 5, 2014 na kumalizika Oktoba 4, lakini ratiba ya Bunge
hilo inaonyesha kuwa litamalizika Oktoba 31, siku ambayo mwenyekiti wa
Bunge hilo atakabidhi kwa Rais Katiba inayopendekezwa.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hadi sasa Serikali
bado haijatoa tangazo (GN) lingine kuongeza muda hadi mwishoni mwa
Oktoba kama alivyosema Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta wakati
akitoa ufafanuzi wa siku 60 zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo, Agosti
5 mwaka huu.
Sitta alisema kwa kadiri ya tafsiri, siku za kazi ni Jumatatu hadi
Ijumaa ambazo wajumbe wanapaswa kufanya kazi na kwamba Jumamosi na
Jumapili siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na Rais.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hadi
sasa hawajapata maelekezo ya ziada kutoka serikalini ambako waliandika
barua ya kuomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo.
“Tulimwandikia barua, Katibu Mkuu Kiongozi (Ombeni Sefue) kuomba
ufafanuzi wa siku hizo kama ambavyo sisi tungependa iwe, lakini hadi
sasa bado hatujajibiwa lakini bado siku zipo nadhani tutajibiwa tu
wakati mwafaka,” alisema Hamad ambaye pia ni Katibu wa Baraza la
Wawakilishi.
Sefue alikiri ofisi yake kupokea barua kutoka Bunge Maalumu ikiomba
ufafanuzi ambao ungeliwezesha kuongeza siku kwa lengo la kukamilisha
kazi ya kujadili na kuandika Katiba inayopendekezwa na kwamba maombi yao
bado yanafanyiwa kazi.
“Bado tuna muda wa kutosha tu, ni kweli tulishayapokea maombi ya
Bunge Maalumu kuhusu suala hilo na Mheshimiwa Rais akikamilisha kazi
yake watajulishwa tu,”alisema Sefue.
Utata wa kisheria
Licha ya ahadi iliyotolewa na Sitta ni dhahiri kwamba suala hilo lina
utata wa kisheria kutokana na kauli iliyowahi kutolewa na Mwanasheria
wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema wakati akitoa ufafanuzi wa maana
ya siku 70 ambazo Bunge lilikaa mara ya kwanza.
Baada ya kusoma hati ya Rais ya kuitishwa kwa Bunge hilo, Februari
mwaka huu, Jaji Werema alisema siku 70 zilizotolewa kwa mujibu wa
tangazo la Serikali ni za kikalenda na siyo siku za kazi kwa sababu
wajumbe wa Bunge Maalumu siyo watumishi wa kuajiriwa.
Maelezo ya Jaji Werema yalitokana na swali lililoulizwa na Mjumbe wa
Bunge Maalumu, Ezekiah Oluoch ambaye alitaka ufafanuzi huo kutokana na
siku zilizotengwa kuonekana kwamba ni chache na zisingetosha kukamilisha
kazi ya kutunga Katiba.
Kauli ya Jaji Werema haijawahi kutenguliwa na Mahakama au yeye
mwenyewe na kwa msingi huo, kwenda kinyume chake ni kuvunja Sheria ya
Kazi na Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya 2005.
Vifungu vya 22 (1) na (2) vya sheria hiyo vinazungumzia ushauri wa
kisheria wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu suala lolote analotakiwa
kulitolea ufafanuzi, wakati Kifungu cha 23 (1) kinasema ushauri huo
unabaki kuwa msimamo wa Serikali katika suala husika, vinginevyo
ubatilishwe ama na Mahakama au na AG mwenyewe katika utekelezaji wa
wajibu wake.
Jana katika maelezo yake, Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue alisema Jaji
Werema alikuwa sahihi katika tafsiri aliyoitoa kuhusu siku zilizotolewa
na Rais wakati wa awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu.
“Jaji Werema yuko sahihi kabisa, kwa hiyo hata Rais atakapokuwa
akitoa majibu ya maombi yaliyofikishwa kwake kuhusu nyongeza ya siku
atazingatia sheria za nchi,” alisema.
Bunge la Muungano na BLW
Mgogoro mwingine unaojitokeza ni ratiba za vikao vya Bunge la Muungano ambalo limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la Wawakilishi ambalo limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22, mwaka huu.
Mgogoro mwingine unaojitokeza ni ratiba za vikao vya Bunge la Muungano ambalo limepangwa kuanza Novemba 4, 2014 na Baraza la Wawakilishi ambalo limepangwa kukutana kuanzia Oktoba 22, mwaka huu.
Kwa kawaida, vikao vya Bunge hutanguliwa na wiki mbili za vikao vya
kamati za kudumu na ikiwa ratiba itabaki kama ilivyo, basi vitaingiliana
na vikao vya Bunge Maalumu ambalo ratiba yake imepangwa kuendelea hadi
Oktoba 31, mwaka huu.
Katibu wa Bunge la Muungano, Dk Thomas Kashililah alisema vikao vya
Kamati za Bunge hilo vinatarajiwa kuanza Oktoba 13, mwaka huu kutokana
na kuwapo kwa miswada mingi ya Serikali inayopaswa kufanyiwa kazi.
“Tuna miswada ya Serikali kama 12 hivi ambayo mingine imekaa muda
mrefu, kwa hiyo kamati zetu nyingi zinapaswa kukutana mapema ili
kuifanyia kazi vinginevyo tutakwama,” alisema Dk Kashililah ambaye pia
ni Naibu Katibu wa Bunge Maalumu.
Alipoulizwa kuhusu mwingiliano wa ratiba baina ya taasisi hizo mbili
ambazo yeye ni mtendaji wake, Dk Kashililah alisema suala hilo
litatafutiwa ufumbuzi kabla ya muda huo kuwadia.
“Nadhani wakati tunafikiria suala la muda wa Bunge la Katiba,
hatukufikiria ratiba hizi nyingine, kwa hiyo ni dhahiri kwamba pengine
tutalazimika kuangalia jinsi ya kutoka hapo,” alisema.
Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai mwishoni mwa wiki
iliyopita alisema kwa jinsi ratiba ya Bunge Maalumu ilivyopangwa lazima
itaingilia shughuli za Bunge la Muungano, hivyo uamuzi unapaswa ufanywe
ili kuepusha mgongano huo.
“Sisi tumeishaliona hilo kwamba ni changamoto, tulikuwa tukijaribu
kujadiliana kuona kama baadhi ya vikao vya kamati vinaweza kuanza mapema
hapa Dodoma, lakini uamuzi bado haujafanyika,” alisema Ndugai.
Naye Hamad alikiri kwamba kalenda ya vikao vya Baraza la Wawakilishi
inaingiliana na ratiba ya Bunge Maalumu na kwamba wanafikiria jinsi ya
kuondoa kasoro hiyo.
“Kuna njia nyingi za kuondoka hapo, pengine tunaweza kumwomba Rais
asogeze mbele vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa wiki mbili, maana hiyo
inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba. Hata hivyo, tutalifanyia kazi ili
kufahamu jinsi ya kulitatua,”alisema Hamad.
Akizungumzia changamoto hiyo ya mwingiliano wa ratiba za kazi za
taasisi hizo, Balozi Sefue alisema jambo hilo ni miongoni mwa
yatakayozingatiwa wakati wa kufanya uamuzi.
“Tutakapokuwa tunafanyia kazi suala hilo, tutazingatia hayo yote na
tutahakikisha kwamba hakutakuwa na mwingiliano wa aina yoyote,” alisema
Sefue.CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment