Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI Bw. James Mbatia. |
Bw. Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa kuteuliwa, aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Ghalani, ulioko Himo, Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.
“Hatima ya Tanzania na Katiba Mpya, iko mikononi mwa CCM hasa kwenye kikao ambacho kitafanyika leo kikishirikisha vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na Rais Jakaya Kikwete,” alisema.
Aliongeza kuwa, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka CCM, hawana budi kutanguliza uzalendo wa nchi yao kwanza na vyama baadaye kwani hivi sasa, Taifa linakabiliwa na mambo mengine muhimu kama utoaji wa vitambulisho vya Taifa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Uchaguzi Mkuu 2015.
“Tanzania ni yetu sote, hakuna mwenye hati miliki ya kuiongoza milele, kama kuna mtu mweye dhana hiyo atuonyeshe hati inayomruhusu kufanya hivyo,” alisema Bw. Mbatia.
Akizungumzia mkutano wa viongozi wa upinzani na Rais Kikwete, alisema wana imani utafanikiwa kuivusha Tanzania hasa kutokana na hali ya mchakato wa Katiba Mpya unavyoendelea.
“Naamini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, tutavuka salama kama wazee wenzangu wa CCM watatumia hekima na busara kulivusha salama Taifa letu kwenye kikao chetu cha kesho (leo),” alisema.
Bw. Mbatia alisema hapingani na wananchi waliomuomba agombee ubunge kwenye Jimbo la Vunjo katika Uchaguzi Mkuu 2015 kwani yuko tayari kuwatumikia kama watampa ridhaa hiyo.
“Natoa wito kwa wanachama wenzangu wa NCCR-Mageuzi, jitokezeni kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi za vitongoji ili tushike nafasi zote na kukaa kwenye vikao ambavyo vinahusu masuala ya maendeleo,” alisema.
Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa (Bara), Bw. Moses Machali, aliwataka wakazi wa jimbo hilo kutokumchagua tena Mbunge wa sasa. Bw. Augustino Mrema akidai ameshindwa kuwahudumia.
Bw. Machali ambaye pia Mbunge Jimbo la Kasulu Mjini, mkoani Kigoma, alisema katika kipindi chote cha ubunge wake. Bw. Mrema amekuwa msaliti kwa wananchi wake ambapo kutokana na uzee alionao ni vyema akaachia ngazi kwa heshima.
“Miaka 50 ya uhuru na changamoto zake, hatuhitaji wabunge wa aina ya Mrema kwanza ni mtu asiye na msimamo, pili amepoteza mwelekeo kwa kusaliti maoni ya wananchi katika mchakato wa Katiba Mpya ambao unaoendelea,” alisema.
No comments:
Post a Comment