Friday, 19 September 2014

Ulinzi mkali kesi ya Sheikh Farid

Kiongozi wa Jumuia ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar Sheikh Farid Had Ahmed.
ULINZI mkali wa polisi na mbwa umetawala Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, wakati kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), Sheikh Farid Hadi Ahmed (43) na wenzake ilipokuwa ikitajwa.

Askari wenye sare na wale waliovaa kiraia walitanda kila kona ya mahakama hiyo kwa ajili ya kuhakikisha usalama unakuwapo.

Ndugu wa washtakiwa walifurika mahakamani hapo, lakini hawakupata nafasi ya wote kuingia katika chumba cha mahakama kwa sababu ya udogo wake, waliofanikiwa kuingiawatano.

Kundi hilo kubwa la watu lilikaa katika banda la kusubiri hadi basi la magereza lilipotoka na watuhumiwa kwa ajili ya kuwapeleka gerezani.

“Taqbir… taqbir… taqbir…,” hayo ni maneno waliyokuwa wakitamka ndugu na jamaa wengine wa washtakiwa wakati basi hilo la magereza likipita mbele yao.

Vijana waliokuwa wakiaga kwa taqbir wengine waliamua kulifuata kwa karibu basi hilo hali iliyosababisha mbwa kuanza kuwarukia mwilini. Mmoja alidakwa suruali, akanusurika baada ya polisi kumtoa mbwa.

Akiwasilisha taarifa ya kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka, alidai upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine ya kesi kutajwa.

Wakili wa utetezi, Rajabu Abdallah, aliiomba mahakama kuifuta kesi hiyo kwa sababu hati ya mashtaka haielezi maeneo husika ambako matukio yalifanyika.

Pia hati hiyo haielezi kama mahakama hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Kweka akijibu alidai kesi hiyo iko mahakamani hapo kwa ajili ya hatua za awali na kupata taarifa wakati upelelezi ukikamilika ili jalada lihamie Mahakama Kuu.

Hakimu Hellen Riwa anayesikiliza kesi hiyo, aliiahirisha na kuahidi kutoa uamuzi Oktoba Mosi, mwaka huu na kuongeza kwamba hoja hizo wanatakiwa kuziwasilisha Mahakama Kuu.

Washtakiwa wanadaiwa kwamba wote kwa pamoja kati ya Januari mwaka 2013 na Juni 2014 maeneo mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama kuingiza watu kushiriki vitendo vya kigaidi.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wote wanadaiwa kuwaingiza watu nchini kushiriki vitendo vya ugaidi huku wakijua ni kosa.

Shtaka la tatu linamkabili mshtakiwa Farid na Sheikh Mselem Ali Mselem, ambao wanadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014, maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliwaajiri  Sadick Absaloum na Farah Omary kushiriki kutenda vitendo vya kigaidi.

Shtaka la nne linamkabili Farid, ambaye anadaiwa kuwahifadhi Sadick Absaloum na Farah Omary waliotenda vitendo vya kigaidi, huku akijua kwamba ni kosa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sheikh Faridi, Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah Hassani, Hussein Ally, Juma Juma.

Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro, Said Sharifu, Sheikh Mselem Ali Mselem na Abdallah Said Ali.


No comments:

Post a Comment