Sunday, 14 September 2014

Mwalimu madrasa adaiwa kumdhalilisha mwanafunzi

Madina Issa na Khamisuu Abdallah

Wakati Serikali na taasisi za kiraia zikiendelea kukemea vitendo vya udhalilishaji, bado viunaendelea kushamiri.

Katika tukio la hivi karibuni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 11 (jina linahifadhiwa) anadaiwa kudhalilishwa na mwalimu wake wa madrasa.

Mtuhumiwa wa tukio ametajwa kwa jina la Seif Nassor anaefundisha chuo cha Almadrasatu Ayatul- Atfar, kilichopo Mpendae.

Mwalimu huyo anadiwa kumuingilia mtoto huyo kinyume cha maumbile.

Akizungumza na ZanzibarLeo katika kitengo cha mkono kwa mkono hospitali kuu ya Mnazimmoja ambako alifikishwa kupatiwa matibabu, mtoto huyo alisema mwalimu wake amekuwa na tabia ya kumchukua ofisini na kumwambia avue nguo zote na alale chini na baadae kumpitishia uume wake.

“Mwalimu Seif huwa ananiita ofisini kabla wanafunzi hawajatolewa na kukomea mlango kwa juu kisha ananambia nivue nguo zote na nilale chini kisha ananiingiza uume wake nyuma kisha ananambia nivae nguo,” alisema.

Alisema mbali na yeye pia kuna watoto wengine wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo na mwalimu huyo.

Alisema siku ya mwisho kufanyiwa kitendo hicho ilikuwa Jumapili kabla ya mwalimu huyo kuondoka.

Mama mzazi wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa) alisema taarifa ya mtoto wake kudhalilishwa, alizipata kutoka kwa jirani yake ambae watoto wake wanasoma chuo hicho.

Alisema alipokwenda kumuuliza mtoto wake alikiri kufanyiwa vitendo hivyo.

Alisema mwalimu huyo amekuwa na tabia ya kwenda nyumbani kwa mtoto huyo kila kunapokucha ambapo siku ya Septemba 7 alikwenda kuwaaga na kuelekea kisiwani Pemba.

Hata hivyo, alisema anashindwa kutoa taarifa kwa uongozi wa chuo kwa sababu wanamuwekea kifua mwalimu huyo.

Aliiomba serikali kutoa adhabu kali kwa wafanyaji wa vitendo hivyo kwani vinaongezeka siku hadi siku.

Daktari wa kitengo hicho ambae alimfanyia uchunguzi mtoto huyo, Salum Omar Mbarouk, alisema alimpokea mtoto huyo na kumchunguza na kugundua kwamba sehemu zake za siri zipo salama.

Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa waangalifu na watoto wao wanapotoka majumbani kwani vitendo vya ubakaji vimezidi.

No comments:

Post a Comment