Thursday, 11 September 2014

Ukawa wapaza sauti: Hapana! Hapana! Haikubaliki

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa akizungumza na wenyeviti wenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia (kulia) na Ibrahim Lipumba baada ya kumaliza kuzungumza na waandishi wahabari kuhusu mchakato wa Katiba na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), Samuel Sitta kusitisha vikao vya Bunge sasa mpaka mwafaka utakapopatikana kwa kuwa kuendelea kwake kunahalalisha ulaji wa fedha za walipakodi.

Akisoma tamko la vyama hivyo mbele ya wanahabari jana, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema: “Ukawa tunapaza sauti zetu, tukisema hapana! Hapana! Haikubaliki.”

Alisema kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wameafikiana kuahirishwa kwa Bunge hilo kupisha maandalizi ya Bunge la Muungano wa Tanzania, kuendelea kwa BMK hadi Oktoba 4 ni ufujaji wa fedha za umma.

Mbatia alisema TCD walikubaliana kuwa mchakato wa Katiba hauwezi kufikia mwisho sasa kutokana na mambo kadhaa kutokwenda sawa.

Mwenyekiti huyo wa NCCR-Mageuzi, aliongeza kuwa mchakato huo unapita katika kipindi kigumu na tete ambacho kama hatua madhubuti hazitachukuliwa, Tanzania inaweza kuingia katika machafuko yatakayochafua taswira yake duniani.

Alisema wajumbe wa TCD walikubaliana kufanya mabadiliko ya 15 ya Katiba ya sasa na pia kutoa nafasi kwa mazungumzo yanayoendelea ya kupata maridhiano ya kisiasa juu ya Katiba itakayowafaa Watanzania na inayoakisi maoni yao kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Amvaa Sitta 
“Samuel Sitta asiendelee kuwachezea Watanzania, kwani yeye ni mtu gani huyo? Yuko juu ya nani? Anaogopeka na nani? Namwambia Sitta endapo atasababisha vurugu yoyote baada ya maafikiano tuliyofikia na Mheshimiwa Rais, endapo damu yoyote itamwagika kwa sababu ya ubabe wake, itabidi alipe usaliti huo.

“Wasije wakaona yanayotokea Kenya…Sitta chochote kitakachotokea watakuja kumkamata na kumpeleka The Heague (Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai) … ole wake machafuko yoyote yatokee.”

Profesa Lipumba 
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema hakukuwa na sababu kwa Bunge Maalumu kuongeza siku 60 kwa kuwa hakukuwapo na maridhiano ya vyama vya siasa wakati uamuzi huo ulipochukuliwa.

Alisema hatua ya kuliongezea muda Bunge hilo, imelisababishia Taifa hasara kubwa na kumtaka Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua hesabu za fedha zilizotumika.

“Tunasikia walikuwa wanakunywa chai ya asubuhi na jioni ya Sh10,000 na chakula cha mchana Sh25,000 hata wajumbe ambao hawapo wanalipiwa… hata wakati tunajadili Katiba, mambo ya msingi ya uwazi, uwajibikaji na uadilifu waliyakataa yasiwemo ndani ya tunu za Taifa,” alisema Profesa Lipumba.

Dk Willibrod Slaa 
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema amebaini kuwa siku 60 za kwanza hazikuwekwa na Sheria, bali zilitolewa kama Tangazo la Serikali (GN) ambayo ni taarifa inayotangazwa katika gazeti la Serikali na Rais na Waziri.

Hivyo alisema, Rais angeweza kuliahirisha wakati wowote kwa kuwa kauli yake haikuwa sheria kama ambavyo amenukuliwa akisema mara kwa mara kuwa sheria inambana kuliahirisha.

“Rais alipaswa kwenda tena kwenye Gazeti la Serikali kufuta tangazo lake, haihitaji kwenda kwa wabunge, hahitaji kupiga magoti, hahitaji kubembeleza mtu, ni utashi wa Rais mwenyewe,” alisema Dk Slaa na kuongeza:

“Anaogopa kuchukua hatua kwa sababu wale watalalamika, maana yake Rais anajali zaidi malalamiko ya watu 600 kuliko malalamiko ya Watanzania milioni 40 ambao hawana mlo wa siku,” alisema.

Alisema pamoja na makubaliano waliyofikia kati ya vyama vya siasa na Rais Kikwete, bado Sitta ameendelea kuwahadaa wananchi kuwa Katiba Mpya itapatikana kabla ya Oktoba 4, mwaka huu.

Freeman Mbowe 
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema Ukawa hawako tayari kuona Bunge hilo likiendelea na vikao vyake hadi Oktoba 4, mwaka huu.

“Hatuwezi kukubali ubadhirifu wa fedha unaoendelea Dodoma hadi Oktoba 4, tutawaeleza vijana wetu tuingie barabarani, kwani tumechoshwa na dhuluma zinazofanywa na CCM na Serikali yake,” alisema na kuongeza:

“Kama Rais anashindwa kuzuia ubadhirifu wa fedha unaoendelea Dodoma eti kwa sababu sheria haimruhusu na kuwaacha waendelee kwa wiki tatu zaidi, hatuwezi kukubali tutakutana barabarani.”

Mbowe alisema wamevumilia vya kutosha na kuwapa nafasi ya kutafakari lakini wamewapuuza, jambo ambalo wameeleza hawatalikubali liendelee.

“Katika uchaguzi ngazi ya Taifa Chadema, (Septemba 14), kutakuwa na wajumbe mbalimbali kutoka Ukawa, nitatumia hadhara hiyo kuwaeleza ni lini vijana wetu tutaingia barabarani.”

CHANZO: MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment