Monday, 8 September 2014

TCD, JK kukutana leo Dodoma

Rais Jakaya Kikwete
Dodoma. Masikio ya Watanzania leo yanaelekezwa mjini hapa kusikia kile ambacho Rais Jakaya Kikwete alisema ni hatima ya mchakato wa Katiba, atakapokutana na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
TCD inaundwa na vyama vya siasa vyenye wabunge kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Mazungumzo hayo yaliyopangwa kuanza saa 6.00 mchana Ikulu ndogo, ndiyo yatakayotoa mwelekeo wa Bunge Maalumu la Katiba lisitishwe kupisha uchaguzi mkuu kwa kutumia Katiba ya mwaka 1977 au la.
Habari kutoka ndani ya TCD zinaeleleza kuwa mazungumzo hayo yanatarajiwa kutanguliwa na kikao cha juu cha taasisi hiyo kilichopangwa kufanyika jana katika Hoteli ya St.Gasper kuanzia saa 10.00 jioni.

“Kikao cha leo (jana) cha Summit ya TCD ni kwa ajili ya kupokea na kuidhinisha maazimio ya Kamati Ndogo ya watu wanne iliyoundwa kupitia mambo yaliyojitokeza katika kikao cha kwanza na Rais Kikwete,” alisema mtoa habari wetu.

Kamati hiyo inamjumuisha katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katibu mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia. “Hiyo kamati iliundwa kufanyia kazi mapendekezo ya Rais baada ya kukutana naye. Tunaamini kwa kusaidiana na wataalamu wake, Rais alikwenda kuyafanyia kazi yale tuliyoyapendekeza kama TCD,” alisema mmoja wa viongozi.

Akihutubia Taifa kupitia wazee wa Mkoa wa Dodoma wiki iliyopita, Rais Kikwete alisema leo ndiyo itakuwa hatima ya mazungumzo hayo.

Chanzo kingine cha habari ndani ya TCD inayojumuisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uliosusia vikao vya Bunge hilo, kimedokeza kuwa suala la kufanya uamuzi mgumu kuhusu mustakabali wa Bunge kwa masilahi ya Taifa, lipo mikononi mwa vyama vya siasa badala ya wajumbe.

“Ukiwauliza wajumbe kama Bunge liahirishwe au la, watataka lisiahirishwe kwa sababu wanafikia ukomo na baadhi hawana uhakika wa kurudi,” alisema mpashaji huyo.

No comments:

Post a Comment