Saturday, 6 September 2014

Hatima ya Bunge la Katiba kujulikana Sept 15

Wakili wa Said Kubenea, Peter Kibatara (kushoto) akijadiliana jambo na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Hatima ya kuendelea au kusimama kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma, sasa itajulikana Septemba 15, wakati Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi wa pingamizi la Jamhuri (Serikali), kuhusu maombi ya kusimamishwa kwa vikao vya Bunge hilo.

Maombi hayo namba 29 ya mwaka 2014, yaliwasilishwa mahakamani hapo na Mwanahabari Saed Kubenea, kutokana na kesi ya kikatiba namba 28 ya mwaka 2014, aliyoifungua dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akihoji mamlaka ya Bunge la Katiba.

Hata hivyo, baada ya Kubenea kupitia kwa Wakili wake Peter Kibatala kuwasilisha maombi hayo mahakamani hapo, Jamhuri kupitia kwa AG, iliwasilisha pingamizi la awali la kisheria likiiomba mahakama iyatupilie mbali maombi hayo huku ikiainisha hoja tatu za pingamizi hilo.

Pingamizi hilo lilisikilizwa jana, ambapo jopo la Mawakili wa Serikali likiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG), lilitoa hoja zake kwa kina ili kupinga maombi hayo, kisha Wakili Kibatala alijibu hoja hizo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jopo la Majaji watatu wa mahakama hiyo wanaosikiliza maombi hayo pamoja na kesi ya msingi, liliahirisha hadi Septemba 15 itakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo la Jamhuri.

Jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo linaongozwa na Jaji Augustine Mwarija akisaidiana na Jaji Dk Fauz Twaib na Jaji Aloysius Mujulizi.

Uamuzi wa pingamizi hilo ndiyo utakaotoa hatima ya Bunge hilo. Iwapo Mahakama Kuu katika uamuzi wake itakubaliana na hoja za pingamizi hilo la Jamhuri, basi maombi hayo ya Kubenea kusimamisha Bunge hilo kwa muda kusubiri uamuzi wa kesi yake ya msingi, yatatupiliwa mbali.

Hata hivyo, ikiwa maombi hayo yatatupiliwa mbali, basi mtoa maombi anaweza kujipanga na kuwasilisha tena maombi hayo upya, baada ya kufanya marekebisho ya kasoro za kisheria ambazo mahakama itakuwa imeziainisha katika uamuzi wake, au anaweza kuachana nayo, hivyo kusubiri kusikilizwa kwa kesi ya msingi.

Ikiwa mahakama itatupilia mbali pingamizi la Jamhuri, basi inaweza kuamuru Bunge hilo lisitishe shughuli zake mpaka hapo kesi ya msingi itakapoamriwa.

Hoja za pingamizi la Jamhuri zilizosikilizwa jana ni pamoja na inayoeleza kwamba maombi hayo mbele ya mahakama yana upungufu wa kisheria kwa kuwa hayakutaja kifungu cha sheria kinachoipa mamlaka ya kutoa kinachoombwa.

Katika hoja nyingine, Jamhuri inadai kuwa maombi hayo hayana maana, bali ni ya maudhi na kwamba hayana msingi kisheria. Pia inadai kuwa ni batili kisheria kwa kuwa hati ya kiapo inayoyaunga mkono, ina upungufu wa kisheria.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, pamoja na mambo mengine, DAG Masaju alidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuamuru Bunge hilo lisimamishe shuguli zake kwa kuwa Bunge hilo liko kwa mujibu wa Katiba, ambayo pia mahakama inatokana nayo.

Pia wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, uliibuka mvutano mkali wa hoja kati Jamhuri na Wakili Kibatala, ambaye alipinga madai ya Jamhuri wakati akijibu hoja zake, ambapo pamoja na mambo mengine alidai mahakama hiyo ina mamlaka ya kusimamisha vikao vya Bunge hilo.

Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri hiyo, chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.

Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria, pia itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.

Kwa mujibu wa hati hiyo, uamuzi wa kufungua kesi hiyo kuomba tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, umetokana na mjadala na mvuto wa kisheria na nje ya misingi ya kisheria, ndani na nje ya Bunge hilo kuhusu mamlaka ya bunge hilo.

Mjadala na mvutano huo ni kama bunge hilo katika utekelezaji wa majukumu yake lina mipaka au halina mipaka kwa mujibu wa vifungu hivyo 25 (1) na 25 (2) vya sheria hiyo, kiasi kwamba linaweza kuacha mapendekezo ya Rasimu ya Katiba na kuweka mapendekezo mapya.

Katika kusisitiza mjadala kuhusu mamlaka ya bunge hilo, hati hiyo inatoa mfano wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika mkutano wake wa mwaka, ambacho kilisema kuwa vifungu hivyo halipi Bunge hilo mamlaka ya kubadili rasimu hiyo.

Inaongeza kuwa wakati TLS wakitoa msimamo huo, kuna wataalamu wengine washeria wanadai kuwa Bunge hilo linaweza kubadilisha na kuongeza ibara kadiri itakavyoona inafaa bila kujali rasimu hiyo.

Kesi ya msingi ya tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo imepangwa kutajwa Septemba 15, 2014.

Wakati huo huo, kesi ya nyingine ya kupinga Bunge Maalumu la Katiba iliyofunguliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), nayo imepangwa kutajwa leo.

Kesi hiyo pia imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji hao watatu, Mwarija, Dk. Twaib na Mujulizi.

Kwa mujibu wa TLS katika kesi hiyo pia inaomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Tume ya Marekebisho ya Katiba na amri ya zuio la muda kusimamisha Bunge hilo, mpaka utatuzi wa masuala tata yaliyoanishwa kwenye kesi hiyo yatakapotatuliwa.

Pia kinaomba mahakama iamue kama mabadiliko ya Kanuni yaliyofanywa na Bunge hilo hayavunji Sheria ya Tume ya Marekebisho ya Katiba na kama ni sahihi katika falsafa ya uandishi wa Katiba, misingi ya sheria, mila na desturi zinazoliongoza Bunge hilo.

CHANZO: MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment