Katibu Mkuu wa CCM Mh. Abdul-rahman Kinana |
Akitoa maoni yake kuhusiana na matokeo ya kura iliyopigwa wiki
iliyopita nchini humo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema
sababu zilizoifanya Scotland kutaka kujitenga zinafanana na zile za
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema ni vyema wananchi wakajifunza kuwa masuala kama hayo hayapaswi kujadiliwa kwa papara.
“Waandishi wengi wamenipigia simu wakitaka kujua maoni yangu…mimi
nasema kuwa suala hili limetufundisha kuwa jambo jema ni kubaki katika
Muungano,” alisema Kinana alipohutubia mkutano wa hadhara katika Mji
Mdogo wa Mlandizi, wilayani Kibaha Vijijini, Mkoa wa Pwani.
Kinana alisema wakati wa kampeni, Waziri Mkuu wa Scotland, Alex Salmon aliwashawishi watu kupiga kura ya kujitoa.
“Kulingana na kura za maoni watu wengi waliamini Scotland itajitoa
katika himaya ya ufalme wa Uingereza, lakini matokeo ya kura yamekuwa
tofauti. Hili ni funzo kwetu kuwa wanasiasa hawapaswi kuwa wasemaji wa
wananchi au kuwafanyia uamuzi,” alisema na kuongeza kuwa wananchi wana
haki ya kufanya uamuzi kwa mambo yanayohusu maisha yao.
Alisema kila Muungano una matatizo na suluhu ni kuyajadili kwa umakini ili kuyapatia ufumbuzi wenye manufaa kwa wananchi.
Kinana alisema matokeo ya kura hiyo yanaonyesha kuwa duniani kote watu wanapenda umoja kama ambavyo Watanzania wameudumisha.
Aliwataka wanaozungumzia kuuvunja Muungano, kujifunza kutoka Scotland ambayo imekuwa mshirika na Uingereza kwa miaka 307 sasa.
Awali, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema
matokeo ya kura ya Scotland yamethibitisha kuwa Muungano wa hapa nchini
utaendelea kudumu. “Kura hii imewakata kidomodomo wale wanaopigania
kuuvunja Muungano wetu. Wameshaonyeshwa kuwa watu duniani kote wanapenda
umoja,” alisema.CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment