Saturday, 20 September 2014

Jeshi la Polisi lalaaniwa kwa kuwashambulia Waandishi

Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda (kulia) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani). Kushoto ni Katibu wake, Neville Meena.
Wadau mbalimbali wa habari nchini wamelaani vikali kitendo cha Jeshi la Polisi kuwashambulia na kuwajeruhi Wandishi wa habari wakiwa kazini juzi mbele ya Makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es salam.

Wandishi hao kutoka vyombo tofauti walishambuliwa wakati wakifuatilia taarifa za Mwenyekiti wa chama cha Demokrasi na Maendeleo Chadema Freeman Mbowe aliyekuwa akihojiwa na Jeshi la Poloisi kufuatia kauli yake ya kuitisha maandamano na migomo isiyo na kikomo nchi nzima kupinga kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.

Mbowe alitoa kauli hiyo wakati akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Chadema mwishoni mwa wiki iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salam.

Wandishi walioshambuliwa ni Josephat Isango wa gazeti la Tanzania Daima, Shamimu Ausi wa gazeti la Hoja na Yussuf Badi ambae ni mpiga picha wa magazeti ya serikali (TSN) ambapo Issango alijeruhiwa mguuni na Ausi usoni karibu na jicho la kulia.

Miongoni mwa wadau waliyolaani kitendo hicho ni Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Umoja wa klabu za Wandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Bodi ya Taasisi za kutetea haki za binadamu (THRDC) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Katika kulaani kitendo hicho Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania Absalom Kibanda alisema Jukwaa la Wahariri linalaani kitendo cha kushambuliwa kwa wandishi wa habari kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na haki za binadamu.

Aidha Kibanda amemtaka Mkuu wa jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu kulifumua Jeshi la Polisi na kuliunda upya kwani limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kikazi kutokana na kuendelea kuwashambulia wanahabari badala ya kukabiliana na uhalifu.

Pia TEF wamemwandikia barua IGP juu ya kulaani tukio hilo na kumtaka kuchukua hatua dhidi ya polisi waliotekeleza vitendo hivyo kutokana na kujulikana kupitia picha za video na za mnato zilizopigwa.

“Jeshi la Polisi linapaswa kufanya kama kile kilichofanywa na polisi wenzao wa Brazil, Julai mwaka huu ambako askari polisi wanne walionaswa katika mikanda ya video wakiwashambulia waandishi wa habari, walisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kufanyika,” alisema Kibanda.

Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari alisema MCT inaamini mashambulizi hayo hayakuwa bahati mbaya kwa kuwa ni mfululizo wa Jeshi hilo kuwanyanyasa waandishi wakati wakiwa katika kazi.

Aidha, Baraza hilo limeeleza kuwa mashambulizi hayo siyo tu yamelenga kuficha ukatili uliokusudiwa kufanywa, bali unaibua chuki baina ya taasisi hiyo na vyombo vya habari bila sababu za msingi.

“Unyanyasaji huu wa polisi ulifanyika mbele ya viongozi wakuu wa Jeshi akiwamo Kamishna wa Opereseheni na Mafunzo, MCT tunalishauri jeshi la polisi kuacha waandishi wa habari kufanya kazi zao badala ya kutumia nguvu kupita kiasi ikiwa ni pamoja na kuharibu vitendea kazi vyao,” ilisema taarifa hiyo.

Katika hatua nyengine Mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Kutetea Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Saed Kubenea alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za waandishi wa habari kuendelea kushambuliwa na polisi wakati wakitimiza wajibu wao.

Alisema kama hatua stahiki zisipochukuliwa vyombo vya habari na waandishi washikamane kwa pamoja kushinikiza mkuu wa jeshi hilo awajibike mwenyewe kwa kujiuzulu.

Nazo Klabu za waandishi habari nchini (UTPC), zimetoa tamko la kulaani kitendo cha polisi wa jijini Dar es Salaam kuwapiga baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri kufanya mahojiano na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Akizungumza na wanahabari jijini Mwanza jana, Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Abubakar Kassan, alisema kitendo cha polisi kurudia vitendo vile vile vya kuwanyanyasa waandishi wa habari wanapokuwa kazini, hakina budi kulaaniwa.

Alisema inawezekana kitendo cha polisi kuwafukuza wafuasi wa Chadema kilikuwa sahihi, lakini wanapaswa kukumbuka wanahabari walikuwa kazini kutoa taarifa kwa jamii kuhusu mahojiano ya polisi na Mbowe.

Nacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema kimemtaka Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, ajitokeze hadharani na atoe kauli kama alitoa maelekezo mengine kwa vyombo vya dola dhidi ya vyombo vya habari mara baada ya kukutana na wahariri wa vyombo hivyo.

Pia Chadema kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, atoe kauli mbele ya umma ni hatua gani watachukua dhidi ya askari waliofanya tukio hilo baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paulo Chagonja.

“Chagonja alisimamia operesheni mbele ya jeshi na kuhakikisha kupigwa kwa waandishi wa habari, licha ya waandishi kuonyesha vitendea kazi vyao vikiwamo kamera lakini waliumizwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment