Friday, 26 September 2014
Balozi Seif akanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mtanzania
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekanusha Habari iliyochapishwa katika Gazeti litolewalo kila siku la Mtanzania iliyotolewa siku ya Jumatano ya tarehe 24 Septemba, 2014 likiwa na Kichwa cha Maneno kisemacho
“SIRI ZAVUJA ZA AG ZANZIBAR KUJIUZULU “.
Kanusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa Vyombo mbali mbali vya Habari katika Ukumbi wa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mjini Dodoma.
Balozi Seif alisema Serikali inakanusha suala la sintofamu lililoandikwa na gazeti hilo ambayo imedai kwamba Viongozi wa juu wa CCM walikutana kwa dharura na kuazimia kufukuzwa kazi kwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ kwa kile walichodai kwamba amekisaliti Chama cha Mapinduzi
Alifahamisha kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatakiwi kuwa muumini wa Chama chochote cha siasa na ndio maana hata vikao vya chama hatakiwi kuhudhuria. Hivyo uteuzi wa Kiongozi huyo anayesimamia masuala ya kisheria hufanywa na Rais wa Zanzibar ambae ndie mwenye maamuzi ya kumuweka na kumuondoa.
Akigusia hoja 17 za Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alizotaka ziingizwe katika Katiba Balozi Seif alisema suala hilo ni kweli na Mjumbe huyo alitakiwa aziwasilishe katika Kamati jambo ambalo alilitekeleza.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziar alielezea faraja yake kutokana na masuala hayo kuingizwa katika Rasimu ya Katiba ambapo hadi sasa Hoja 4 kati ya hoja hizo 17 bado zinafanyiwa kazi.
Alieleza kwamba kuchaguliwa kwa Mjumbe katika Kamati na kukataa kuhudhuria kama alivyofanya Mwanasheria Mkuu huyo wa SMZ ni maamuzi yake binafsi kwa vile hakuna ulazima wa mjumbe kuchaguliwa huko ikaonekana kama kifungo ingawa atakuwa na wajibu wa kuendelea kufanya kazi katika kamati hadi mwisho wake.
Balozi Seif alisema kwamba Mh.Othman Masoud alitakiwa ashiriki katika kamati kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wa Zanzibar.
Alisema hata hivyo kutokuwemo kwake katika kamati sio kikwazo cha kupatikana kwa rasima ya katiba, kwa vile waliokuwamo ndani ya kamati kwa upande wa Zanzibar walitosheleza kuiwakilisha Zanzibar kikamilifu.
Akigusia upotoshaji mwengine ulioandikwa na gazeti hilo la Mtanzania juu ya masuala 17 aliyotaka Mwanasheria Mkuu wa SMZ yaingizwe katika Rasimu ya Katiba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Taarifa hiyo si ya kweli kabisa.
Balozi Seif alisema Mawaziri wa Chama cha Wanachi {CUF } hawamo katika Bunge Maalum la Katiba sasa inakuaje washiriki kuchangia masuala ambayo wao kama sehemu ya { Umoja wa Katiba ya Watanzania } UKAWA hawakubaliani na kuendelea kwa Bunge hilo.
“Wapo baadhi ya waandishi wa Habari hawafahamu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeshwa katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa ulioundwa na Vyama vya CCM na CUF na kama inavyoeleweka CUF hawamo ndani ya Bunge hilo sasa itakuaje washiriki kuchangia masuala hayo? “ Aliuliza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba suala hilo liliripotiwa sambamba na upotoshaji mwengine wa gazetui hilo la mwanasheria huyo kuwasiliana na Rais wa Zanzibar alisema ni uzushi mtupu usio na maana.
Alisema Mh. Othman Masoud kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wowote na uwezo wa kuwasiliana na Rais au Makamu wa Pili wa Rais kwa mashauriano ya jambo lolote analoona linafaa.
Balozi Seif alithibitisha wazi kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati anaamua kujiuzulu wadhifa wa Ujumbe wa Kamati ya Uandishi Rais wa Zanzibar Dr. Shein alikuwa nje ya Nchi kwa kiziara rasmi ya Kiserikali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi pamoja na Chama cha Mapinduzi bado kinawaamini wana Habari wa vyombo vyote, hivyo amewaomba waandhishi kujiepusha na tabia ya kuzusha baadhi ya mambo ambayo hayana ukweli wowote.
Balozi Seif aliwataka Wana Habari wote Nchini kujitahidi kutumia kalamu zao vyema kwa kuwaelimisha wananchi masuala ya ukweli badala ya kuwapotosha kwa kuwalisha mambo ya kubabaisha.
Akijibu baadhi ya maswali ya wana Habari hao Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitegemei kuchukuwa hatua yoyote ya kisheriaadhidi ya Gazeti hilo. Lakini ikauomba Uongozi wa Gazeti hilo kuzingatia maadili ili kuendelea kutoa Habari zenye usahihi.
Wakati mwengine tunaelewa kwamba kalamu za waandishi huwaponyoka wakati wanapoandika Habari zao. Lakini kuponyoka huko kusiwe ndio muendelezo wa uchapishaji wa Habari zisizo na nuchunguzi “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameiasa mitandao ya kijamii kujiepusha na tabia ya kuendeleza vitisho wanavyovielekeza kwa wajumbe wa Kamati za Bunge Maalum la Katiba hasa kutoka Zanzibar kwa visingizio vya kuizamisha Zanzibar.
Balozi Seif alisema kilichofanyika na kuendelea kufanywa na Kamati hizo chini ya Bunge hilo ni kutekeleza jukumu walilokabidhiwa na watanzania na inapaswa kuheshimiwa na kila Mwanadaamu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wajumbe wa Kamati hizo kwamba Serikali kupitia vyombo vya Dola vitazingatia usalama wao na vitakuwa tayari wakati wowote kumchukulia hatua za kisheria mtu ye yote atakayetishia maisha ya wananchi wakiwemo wajumbe hao.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed aliwaeleza Wanahabari hao wa vyombo mbali mbali Nchini kwamba Katiba ni mchakato ambao masuala yote yanafanyiwa uhakiki wa kina.
Mh. Aboud alifahamisha kwamba suala lolote zito linalohusu mambo ya Muungano haliwezi kutekelezwa bila ya kuhusishwa viongozi na wataalamu wa pande zote mbili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment