MBUNGE wa viti Maalum, Mariam Msabaha (CHADEMA), amemuonya mbunge
mwenzake wa Mpendae kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Turky na
kumtaka aache tabia ya kutumia madaraka na kinga za kibunge kunyanyasa
wananchi katika masuala yasiyohusiana na siasa.
Mbali na kumuonya kwa tabia ya unyanyasaji, pia Msabaha amesema
mbunge huyo anapaswa kuwaomba radhi wabunge wenzake wa kutoka Zanzibar,
kwa kile alichoeleza kuwa tabia ya kujisifu, kukebehi na kuonyesha jeuri
wananchi, kwani si asili na utamaduni wa wazanzibari.
Kutokana na hali hiyo, Msabaha alisema anajiandaa kukabidhi CD za
vitisho vilivyofanywa na Turky, ofisi ya Spika wa Bunge kwa ajili ya
hatua zaidi.
Msabaha, alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana, wakati
akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea taarifa mbalimbali
zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari
vinavyomuonesha Mbunge Turky, akitoa lugha ya kuudhi kwa wananchi mbele
ya askari Polisi.
Katika mitandao hiyo, pamoja na CD iliyogawiwa kwa waandishi wa
habari na Msabaha, Turky, anakaririwa akiwaeleza washindani wake katika
mgogoro wa msikiti wa Sunni, kuwa ni sawa na CHADEMA huku akiwaeleza
kuwa hawana jambo lolote watakaloweza kufanya zaidi ya kupiga kelele.
Msabaha, alisema kuelezea kuwa CHADEMA haiwezi kufanya jambo lolote
ni matusi na kukengeuka kwa mbunge huyo, kwa kuwa hata wananchi
waliomchagua hawaujui msaada wake zaidi ya kusikia akiongoza migogoro
katika matukio tofauti.
“Kwanini Turky atumie ubunge wake kama fimbo ya kuwanyanyasa wengine
katika masuala ya kijamii, mfano ni hivi karibuni alipowajaza askari
katika ukumbi wa uchaguzi pale Blue Pearl wakati waumini wa madhehebu
ya Sunni walipokuwa wakifanya uchaguzi, lengo lake likiwa ni kuwatisha
na kuwaweka watu anaowataka yeye, huku akiwatambia wapinzani wake kuwa
hawana sauti kama CHADEMA, hapa anakiingizaje chama chetu katika masuala
binafsi ya kiimani,” alisema Msabaha.
Aliongeza kuwa watu wanaopewa mamlaka ya kuwaongoza wananchi na
kuamua kuyatumia vibaya mamlaka hayo kwa kuwatisha waliompa nafasi hiyo,
mwisho wake huwa ni machafuko makubwa na kwamba Mbunge Turky anataka
kuleta hayo machafuko.
Alisema kiburi cha Turky kimepitiliza hata kwa mamlaka za Umma, kwa
kile alichoeleza kuwa hivi karibuni ofisi ya msajili wa vizazi na vifo
(RITA), iliagizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania ithibitishe wapiga kura wa
baraza la wadhamini wa msikiti wa Sunny, lakini Mbunge huyo
akalazimisha kufanyika kwa uchaguzi na kujaza polisi idadi ambayo
haikutegemewa.
Jitihada za kumpata Turky kuelezea tuhuma za kutumia madaraka yake ya
kibunge kuwanyanyasa wananchi na kukidhalilisha CHADEMA, zilishindikana
baada ya simu yake ya kiganjani kutokupokewa na hata alipotumiwa ujumbe
wa maneno hakujibu
CHANZO: TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment