Friday, 12 September 2014
CUF walalamikia Tume ya uchaguzi ugawaji wa majimbo
Chama cha Wananchi CUF kimeishauri Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kuzingatia matakwa ya Katiba na kufanya kazi zake kwa uadilifu katika kusimamia zoezi la Uongezaji na Upunguzaji wa Mipaka ya Majimbo ya Uchaguzi.
Aidha CUF kimeitaka Tume hiyo kutokupokea Maagizo yoyote nje ya Mamlaka yake ili kuimarisha ustawi nzuri wa Demokrasia ndani ya Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika Ofisi ya CUF iliyopo Vuga mjini Zanzibar.
Mazroui amesema ZEC haipaswi kuangalia kigezo kimoja tu cha Takwimu ya Wakaazi katika Jimbo husika badala yake waangalie na vigezo vingine katika kugawa Majimbo.
Amedai kuwa ZEC Inapaswa kuzingatia kuwa kuwepo kwa Malalamiko ya muda mrefu ya Wadau wa Uchaguzi juu ya Utaratibu mbovu wa Ugawaji wa Majimbo Zanzibar kulipelekea uvunjifu wa Amani kutokana na baadhi ya Wananchi kutoridhika na hali hiyo.
Aidha Mazrui ameitaka tume ya uchaguzi kuzingatia mazingira ya amani na maelewano yaliyopo na kutokuwa taasisi ambayo itakuwa chanzo cha vurugu na mifarakano katika nchi.
“Tunaiomba ZEC ifahamu kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ipo na inaendelea kufanya kazi zake Vyema hivyo ZEC isijaribu kuwa kichocheo cha kuivuruga Serikali hiyo” Alisema Mazrou.
Hivi karibuni tume ya Uchaguzi ZEC ilitoa Taarifa ya kuyagawa Majimbo ya Uchaguzi lakini Chama cha Wananchi CUF kimedai Ugawaji wa Majimbo hayo umefanywa kisiasa bila kuangalia hali halisi.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment