Thursday, 4 September 2014

Dk Shein: Tanzania inaunga mkono mpango wa hifadhi ya mazingira wa visiwa vya ukanda wa magharibi wa bahari ya hindi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akitoa hutuba yake katika Uzinduzi wa Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi ya Changamoto za Ukanda wa Pwani na mabadiliko tabianchi jana katika Orator Hotel,Apia Samoa ambapo Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa unaendelea.
Tanzania imewahakikishia wanachama wa Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa Changamoto za Ukanda wa Pwani na Mabadiliko ya Tabianchi kuwa inaunga mkono mpango huo kwa kuwa inaamini kuwa mpango huo ni chombo muafaka katika kuleta maendeleo endelevu katika eneo hilo.

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo uliofanyika jana mjini Apia katika visiwa vya Samoa, Rais wa Zanzibar na Mwenyeiti wa Barala la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema mpango huo unatoa fursa kwa washiriki kufanyakazi kwa pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadilko ya tabianchi.

“changamoto tunazokabiliana nazo zinafanana na ni sahihi kufanyakazi pamoja kukabiliana nazo. Mpango huu ni wa manufaa sana katika eneo letu” alieleza Dk. Shein na kusisitiza kuwa katika hali hiyo “Tanzania tunauunga mkono kikamilifu”

Katika hotuba yake fupi kwenye hafla hiyo Dk. Shein ambaye yupo hapa pia kumuwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa unaoendelea sasa alieleza pia umuhimu wa taasisi za kikanda za maeneo ya visiwa kusimama pamoja na kuwa na msimamo mmoja katika mkutano huo ili uweze kuweka msingi madhubuti wa ushikiriano.

Alibainisha kuwa kufanyika kwa uzinduzi wa mpango huo sambamba na mkutano wa nchi za visiwa wenye kuhimiza maendeleo endelevu ni fursa nyingine kwa nchi wanachama wa mpango huo kufanya masuala yao kueleweka miongoni mwa jumuiya ya kimataifa.

Aliongeza kuwa ushiriki wa wadau wengi katika uzinduzi wa mpango huo ni ishana kuwa mpango huo umepokelewa vyema na wadau hao wako tayari kushirikiana na wanachama kutekeleza malengo ya mpango huo.

Hata hivyo alihimiza mpango huo kuchukua hatua za haraka kutekeleza programu zake za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa muda hausubiri hivyo kila wakitekeleza mapema itakuwa ni manufaa zaidi kwa uhai na ustawi wa ukanda wa magharibi wa bahari ya Hindi.

Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein pia aliwasilisha salamu za Rais Kikwete kwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ya uzinduzi ambayo ilihudhiriwa na viongozi mbalimbali wa nchi za visiwa kutoka pande zote za dunia.

Miongoni mwa viongozi walihudhuria na kupata fursa ya kuzungumza ni pamoja na Rais wa Visiwa vya Palau Tommy E. Remengesau Jr., Rais wa Serikali ya Shirikisho la Visiwa vya Micronesia Emanuel Mori na Rais wa visiwa vya Marshall Christopher Loeak.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Samoa Tuilaepa Lupesoliai Sailele Malielegaoi, Waziri Mkuu wa Grenada Dr. Keith Mitchell, Waziri wa Mambo ya Nje wa Seychelles Jean-Paul na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Lapo Pistelli.

Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa Changamoto za Ukanda wa Pwani na Mabadiliko ya Tabianchi ni mkakati mpya wa kiutekelezaji miongoni mwa nchi za visiwa vidogo vya eneo la ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi katika kusimamia malengo ya maendeleo endelevu kwa nchi hizo.

Malengo makubwa Mapango huo yamejikita zaidi katika uhifadhi na usimamizi wa pamoja wa mazingira ya visiwa, fukwe, na bahari zake pamoja na mabadiliko ya tabianchi.

Visiwa vinavyoshiriki mpango huu ni pamoja na Shelisheli, Comoro, Mauritius, Reunion na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment