Monday, 22 September 2014

CCM wafanya vurugu mkutano wa CUF

Wafuasi wa CUF wakiwa katika Mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama hicho Buguruni jijini Dar es salam ambao ulivamiwa na CCM.
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na wafuasi wao wanadaiwa kuvamia eneo la mkutano uliokuwa umeandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), eneo la Buguruni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano wao wa hadhara.

Akizungumza na Tanzania Daima, Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya, alisema, viongozi wa CUF walikuwa wameshafuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kutoa taarifa polisi na kupewa ruhusa kwa maandishi, lakini cha kushangaza walikuta eneo hilo waliloomba kukiwa na mabanda yaliyoandaliwa kwa ajili ya mkutano wa hadhara wa CCM.

“Baada ya kukuta kuna viongozi wa CCM wameweka mabanda yao wanataka kuhutubia mkutano, niliwataarifu vijana wa CUF kuondoa kwa sababu tulikuwa tumefuata sheria, CCM walikaidi hivyo kukatokea fujo, polisi wakaanza kufyatua risasi… ndipo alipokuja RCO wa Ilala, alikuja kuwakutanisha viongozi wa CUF na CCM ikabainika kuwa CCM hawakuwa hata na barua, hivyo waliambiwa waondoke wakagoma hadi polisi walipowatawanya kwa mabomu ndio nikaanza kuhutubia mkutano,” alisema Kambaya.

Taarifa zaidi kutoka eneo hilo zilisema, polisi baada ya kubaini kuwa CCM hawakuwa na barua, walianza kuwabembeleza, tofauti na kama ingekuwa chama cha upinzani kingevamia mabomu yangeanza mara moja.

Katika mkutano huo, Kambaya alivialika vyama vya CUF, NCCR, CHADEMA na NLD kujenga misingi ya kuweka bendera kwenye eneo la ofisi ya Ofisa Mtendaji Kata ya Buguruni kwa madai kuwa CCM tayari wameshajenga, na kwa kuwa hilo ni eneo la serikali ambalo hawapaswi kujenga misingi ya vyama hapo, itabidi vyama vingine navyo vipewe eneo hilo, au CCM wabomoe kwani hairuhusiwi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Mary Nzuki hakupatikana kuelezea fujo hizo zilizodaiwa kuzua tafrani kubwa kwa wakazi wa Buguruni kutokana na milio ya mabomu na risasi.

No comments:

Post a Comment