Friday, 5 September 2014

Kikwete: Hatima Bunge la Katiba Jumatatu

Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia wazee wa mkoa wa Dodoma kwenye Ukumbi wa Chuo cha Mipango alipokuwa akimaliza ziara ya siku sita mkoani humo jana.

Dar/Dodoma. Rais Jakaya Kikwete amesema mkutano wake na viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) utakaofanyika Jumatatu Septemba 8, mwaka huu ndiyo utakaotoa mwelekeo wa namna ya kulinusuru Bunge Maalumu la Katiba.

Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dodoma jana, Rais Kikwete alisema baada ya kukutana na viongozi hao wa TCD Jumapili, iliyopita walipeana majukumu ya kutekeleza na kukubaliana kukutana siku hiyo kwa ajili ya majadiliano ya mwisho.

“Nilieleza utayari wangu wa kufanya kila liwezekanalo kuona mchakato wa Katiba Mpya unaendelea. Nimeendelea na moyo huohuo na nilipoombwa na Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo ambaye ana jina lake maarufu, silitaji kwa sasa, nilikubali kukutana nao,” alisema.

Rais Kikwete alikutana na viongozi wa TCD inayokutanisha vyama vyote vyenye wabunge ambavyo ni Chadema, CCM, CUF, NCCR-Mageuzi na TLP pamoja na Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa anayewakilisha vyama visivyo na wabunge.

Katika hotuba yake ya jana, Rais Kikwete alisema alipokutana na viongozi hao walifanya mazungumzo mazuri na kupeana kazi za kufanya kwa ajili ya kunusuru Bunge hilo.

Bunge hilo linaendelea Mjini Dodoma huku wabunge wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vikiwa vimekataa kushiriki kutokana na kutotimizwa kwa kile wanachoamini kwamba ndiyo msingi wa kupatikana kwa Katiba bora kwa ajili ya wananchi wa kada zote.

Migogoro ya wakulima, wafugaji
Rais Kikwete pia alisema ameshajadiliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na wanafanya mpango wa kuhakikisha migogoro ya wakulima na wafugaji inapatiwa ufumbuzi.

Alisema katika ziara yake amewaeleza viongozi na wananchi hasa kwenye mikoa ya Morogoro na Dodoma kuwa na mipango ya matumizi ya ardhi kwa kugawa maeneo maalumu ya wafugaji na wakulima na kila upande uheshimu eneo la wengine.

“Nimewaeleza wakulima na wafugaji watambue kwamba ardhi haiongezeki lakini watu wanaongezeka, hivyo ongezeko la watu linasababisha shughuli za matumizi ya ardhi kuongezeka. Ni vyema kupanga matumizi ya ardhi kwamba kipande hiki tutafanya shughuli ipi,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Viongozi wa wilaya na mikoa wawe na mipango ya matumizi ya ardhi yao. Kwa wafugaji pia wanatakiwa watambue uwezo wa ardhi waliyo nayo katika kusimamia na kuhudumia mifugo yao, hivyo wawe na mifugo inayoweza kutunzwa kwa ukubwa wa ardhi yao.”

Zaidi alisema ni vyema wafugaji wahakikishe mifugo yao haili mazao ya wakulima kwa kuwa hicho ndicho chanzo cha ugomvi baina ya makundi hayo mawili.

Alieleza kwamba matatizo ya aina hiyo yaliyojitokeza katika Wilaya ya Kiteto baina ya wakulima na wafugaji ni moja ya mambo ambayo yeye na Waziri Mkuu wanayafanyia kazi kwa karibu.

Ugonjwa wa Ebola
Akizungumzia ugonjwa wa ebola, Rais Kikwete alisema tayari hatua madhubuti zimechukuliwa katika maeneo yote muhimu, hasa kwenye viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani, ili kuzuia kuingia kwa ugonjwa huo nchini.

Alisema tayari hospitali zote za mkoa zimeshapewa maagizo ya kuandaa vituo maalumu kwa ajili ya kuwahifadhi watu watakaobainika kuwa na ugonjwa huo ili kuzuia maambukizo kwa watu wengine iwapo itatokea kuwa na mgonjwa wa aina hiyo.

“Kwa Dar es Salaam tayari kituo maalumu cha kuhifadhi wagonjwa wa ebola kimeandaliwa kwenye Hospitali ya Temeke, pia tumechukua tahadhari kwenye viwanja vya ndege ambako imefungwa mitambo maalumu ya kubaini watu wenye dalili za ugonjwa huo. Mitambo mingine 45 imeshaagizwa na itapelekwa kwenye mikoa ya pembezoni,” alisema.

Akielezea ugonjwa huo, Rais Kikwete alisema ni ugonjwa hatari kwa kuwa unaua zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaoambukizwa kwa kuwa hauna kinga wala tiba, hivyo ushirikiano wa wananchi katika kuepusha maambukizo ni muhimu hivi sasa.

No comments:

Post a Comment