Chama cha NCCR Mageuzi Zanzibar kimetangaza mpango wa kufungua kesi
Mahakama Kuu kupinga kazi ya kurekebisha mipaka ya majimbo inayofanywa
na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Msimamo huo ulitangazwa na makamu mwenyekiti wa NCCR, Ambari Khamis
Haji, akidai utaratibu huo haujazingatia uwiano wa idadi ya watu katika
miji mikubwa na midogo. Chama cha Wananchi (CUF) nacho tayari kimeshatoa
tamko la kupinga utaratibu huo kwa sababu hizohizo.
Haji alisema iwapo kazi hiyo itafanyika, inaweza kuibua migogoro
mikubwa ya kisiasa na kuvuruga amani wakati Taifa likijiandaa na
Uchaguzi Mkuu 2015. Alifafanua kuwa majimbo kisiwani Pemba hayana uwiano
wa watu kulinganisha na majimbo ya kisiwani Unguja kwa vile harakati za
uchumi eneo hilo ni kubwa kuliko Pemba.
Alisema Serikali ilipaswa kuimarisha miundombinu ya usafiri kama
bandari, uwanja wa ndege na barabara na kusogeza huduma za maji na umeme
ili kuvutia wawekezaji Pemba, hali ambayo ingepunguza wimbi la watu
kuhama na kusababisha majimbo kubaki na idadi ndogo ya watu.
“Kupunguza majimbo upande mmoja na kuongeza upande mwingine, kunaweza kuvuruga amani na umoja wa kitaifa,” alisema.
“Umoja huu wa kitaifa umepatikana kwa tabu kubwa, kwani baadhi yetu wamepoteza maisha na wengine wamebaki na ulemavu wa maisha.”
Alisema NCCR Mageuzi imeamua kwenda kortini ili kuzuia Kisiwa cha
Pemba kupoteza viti vingi vya ubunge na kuitaka tume iongeze majimbo
badala ya kupunguza.
“Kama wameamua kwenda mahakamani ni haki yao kisheria lakini ZEC
tumewapa nafasi wadau wote wa uchaguzi kutoa maoni kuhakikisha zoezi
linafanyika kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwakani” alisema Jecha.
Zoezi hilo la ukataji wa mipaka ya majimbo linatarajiwa kutumia kiasi
cha shilingi milioni 400 ingawa chama cha CUF kinachounda serikali ya
umoja wa kitaifa kimesema zoezi hilo limelenga kuibeba CCM iweze
kuongeza viti katika uchaguzi wa mwakani.
No comments:
Post a Comment