Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 19 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dar es Salaam jana. |
Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya viongozi wa umma,
madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na muungano. “Tutakutana
mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na wao wawaeleze wananchi
kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika Rasimu ya Pili ya
Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam jana, Jaji Warioba
alisema rasimu hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa na rasimu
iliyotolewa na tume hiyo Desemba mwaka jana.
“Sina hakika kama tutapata Katiba Mpya labda Katiba iliyoboreshwa.
Rasimu au Katiba itakayopendekezwa na Bunge Maalumu haitapigiwa kura
hadi 2016. Sina hakika kama kura hiyo itapigwa kwa kuwa hakuna
maridhiano hasa kuhusu muungano, rasimu hiyo itaanza kupingwa tangu
siku ya kutolewa kwake,” alisema.
Aliongeza, “Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka kesho Katiba Mpya
itakuwa agenda, na agenda hiyo inaweza kuigawa nchi. Kuna uwezekano
mkubwa kwamba mwaka 2016 badala ya kupiga kura mchakato ukaanza upya.”
Jumatano wiki hii Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge
aliwasilisha rasimu hiyo bungeni na kueleza kuwa kamati yake imefuta
ibara 28 zilizokuwa katika rasimu ya Jaji Warioba na kuacha ibara 47,
kuongeza ibara 42 na kurekebisha ibara 186.
Alisema rasimu hiyo ina sura mpya mbili ambazo ni Mamlaka na Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi, Maliasili na
Mazingira ambayo haikuwekwa katika rasimu ya Warioba kwa kuwa si mambo
ya muungano.
Rasimu hiyo ilirejesha muundo wa Serikali mbili kama ilivyo sasa na
kutupilia mbali muundo wa Serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Jaji
Warioba.
Huku akiwa makini, Jaji Warioba ambaye alitumia saa 1:02 kufafanua
umuhimu wa mambo manne yaliyoachwa katika rasimu iliyotolewa na Bunge la
Katiba, alisema hivi sasa wajumbe wa Bunge la Katiba wana msemo wao
kuwa “Warioba ni shida”, kufafanua kuwa watakapomaliza vikao vya Bunge
hilo Oktoba 4, mwaka huu na kurejea mtaani walipo wananchi ndiyo watajua
nani ni ‘shida’, kati yake na wao.
Akizungumzia kitendo cha Bunge hilo kubadili kanuni ili kuruhusu
wajumbe wake kupiga kura za kupitisha rasimu hiyo kwa baruapepe (e-mail)
na nukushi (fax) wakiwa nje ya nchi, Jaji Warioba alisema, “Utaratibu
huu hauwezi kutuletea Katiba ya maridhiano. Hata mimi nimeanza kukata
tamaa.”
Huku akishangiliwa kila mara na mamia ya watu waliohudhuria kongamano
hilo, wakiwamo wasomi na baadhi ya waliokuwa wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema kila mjumbe wa tume hiyo
alikuwa na mawazo yake juu ya Katiba, lakini waliweka kando mawazo yao
baada ya kusikia kauli za Watanzania juu ya Katiba wanayoitaka.
Katika maadhimisho hayo, Jaji Warioba pia alizindua kitabu cha
marehemu Dk Sengondo Mvungi kiitwacho ‘Mvungi anapumua Katiba’. Dk
Mvungi aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na mmoja wa waanzilishi wa
LHRC, alifariki dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini alikopelekwa
kutibiwa baada ya kujeruhiwa na majambazi akiwa nyumbani kwake.
Maadili ya Viongozi wa umma
Kuhusu maadili ya viongozi wa umma alisema, “Wananchi walitoa maoni
mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili ya viongozi. Kutokana na
maoni ya wananchi Tume iliimarisha misingi mikuu ya taifa iliyo katika
Utangulizi wa Rasimu. Misingi iliyo katika katiba ya sasa ni uhuru,
haki, udugu na amani.”
Alisema kutokana na maoni ya wananchi misingi mipya iliongezwa ambayo
ni; utu, usawa, umoja na mshikamano na kwamba wananchi pia
walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye katiba ambazo ni utu,
uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa
(Kiswahili ).
“Bunge Maalumu limeondoa uadilifu, uzalendo, umoja, uwazi, na
uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na kuziweka kwenye
misingi ya utawala bora. Kila Mtanzania anatakiwa awe mzalendo, kila
Mtanzania anatakiwa kuwa mwadilifu, kila Mtanzania anatakiwa aenzi
umoja. Inakuwaje mambo haya yahusu utawala tu?” alihoji.
Alisema tunu za taifa ndiyo msingi wa utamaduni na maadili ya taifa,
kwamba mwelekeo wa taifa utategemea jinsi wananchi wanavyoenzi misingi
mikuu na tunu.
Aliponda kitendo cha Bunge la Katiba kutoweka miiko ya uongozi kwenye
Katiba wakati kila siku viongozi wanalalamika juu ya rushwa na ufisadi,
pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti za benki nje ya nchi.
“Katika bara la Afrika, nchi kama Afrika Kusini, Namibia na Kenya
zimeweka misingi ya maadili na miiko katika Katiba. Hapa kwetu sheria
tulizonazo haziwezi kupambana na rushwa na ufisadi. Sijui kwa nini Bunge
la Katiba wameondoa hili,” alisema.
Madaraka ya Wananchi
Jaji Warioba alipinga kitendo cha Bunge la Katiba kuondoa kipengele
cha wananchi kuwa na madaraka ya kumwondoa mbunge wao kama hawaridhishwi
na uwakilishi wake bungeni, mbunge kutokuwa waziri ili aweze
kuwawakilisha vizuri na ukomo wa mbunge kuwa vipindi vitatu .
“Bunge lina kanuni za kuwawajibisha wabunge na wananchi nao wanapenda
kuwa na madaraka hayo. Vyama vya siasa vina madaraka ya kuwaondoa
wabunge wao katikati ya kipindi. Wananchi nao wanataka watumie madaraka
yao,” alisema.
Mgawanyo wa madaraka
Akizungumzia mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili ya Bunge, Serikali
na Mahakama, alisema pendekezo lao la kumwondoa rais na mawaziri kutoka
kwenye Bunge linakataliwa kwa sababu nchi imezoea mfumo wa kibunge kama
ilivyo kwa nchi nyingi za jumuiya ya madola.
“Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge. Kwenye mfumo wa kibunge
mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji. Madaraka hayo yako mikononi mwa
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge. Hivyo ndivyo ilivyo kwa Uingereza, India,
Canada, Australia, New Zealand,” alisema.
Akitolea mfano mwingiliano huo alisema wakati wa kutunga Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba, bunge lilitunga sheria lakini baadaye Rais
alifanya mazungumzo na watu nje ya bunge na baadaye bunge likalazimika
kubadili uamuzi.
“Tanzania ina mfumo wa urais ambapo rais ni mkuu wa nchi, mtendaji
mkuu na amiri jeshi mkuu. Rais na mawaziri wake kuwa sehemu ya bunge ni
kuchanganya mamlaka. Hali hii inafanya Serikali kuingilia mamlaka ya
bunge na pia bunge kuingilia mamlaka ya Serikali,” alisema.
Aliongeza, “Nchi nyingi zimebadili Katiba zao ili kutenganisha
madaraka ya mihimili. Jirani zetu wa Msumbiji na Kenya wamefanya hivyo.
Kenya imefanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na zile ambazo
wananchi wa Tanzania walitoa.”
Muungano
Huku akitaja kero 20 za muungano, 11 za Zanzibar na 10 za Tanzania
Bara zilizotajwa na wananchi wakati wa kukusanya maoni, Jaji Warioba
alisema, “Ingawa Rasimu ya Bunge Maalumu limerudisha madaraka ya rais
kuigawa nchi hiyo peke yake haitoshi. Mambo haya ni magumu kubadilika
kwa upande wa Zanzibar.”
Aliongeza kuwa ili kufanya mabadiliko kwenye Katiba ya Zanzibar ni
lazima mabadiliko yapitishwe kwa theluthi mbili au zaidi ya Wawakilishi.CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment