Sunday, 28 September 2014

Mahakama ya Kadhi yalitafuna Bunge

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa Bungeni mjini Dodoma. PICHA YA MAKTABA
Suala la Mahakama ya Kadhi limechafua hali ya hewa bungeni mjini Dodoma baada ya wajumbe Waislamu kutishia kupiga kura ya hapana kama halitaingizwa katika Rasimu inayopendekezwa.

Wakati Waislamu wakishikilia msimamo huo, wajumbe ambao ni Wakristo nao wamejipanga kupiga kura ya hapana endapo Mahakama ya Kadhi itaingizwa katika Katiba inayopendekezwa.

Dalili za mpasuko huo zilianza kujitokeza jana asubuhi baada ya mjumbe mmoja, Jaku Ayub Hashim kuwasha kipaza sauti akitaka kuzungumza akisema ana jambo muhimu.

“Mheshimiwa tangu jana (juzi) ulisema utanipa nafasi ya mwanzo nizungumze,” alisema Jaku, lakini Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu alimtaka aketi chini na suala lake limesikika.

Suluhu akaendelea kuwapa wajumbe wengine kuendelea kuchangia na baadaye alimpa Jaku muda wa dakika saba ili kuwasilisha kile alichotaka kukizungumza ndani ya Bunge hilo.

Jaku alisema walipendekeza kifungu kinachotaka uamuzi unaohusu ndoa, talaka na mirathi iliyoamuliwa kwa misingi ya dini ingizwe kwenye Katiba inayopendekeza lakini hakimo.

“Ni kitu kidogo kabisa tuliomba kiongezwe lakini cha kusikitisha kikundi cha sanaa kimeingizwa. Mimi binafsi yangu sitaunga mkono wala mguu wala sitaipigia kura hii,” alisema Jaku.

Suluhu akamweleza kuwa angalizo lake limechukuliwa, na uongozi wa Bunge pamoja na kamati ya Uandishi wanajitahidi kuingiza kila kitu kinachowezekana, lakini kwa misingi na sheria za nchi.

Baadaye Sheikh Masoud Jongo alipopewa nafasi ya kuchangia, naye alitahadharisha kuwa mambo yaliyopendekezwa na Waislamu yasipoingizwa kama ilivyo kwa sasa, hawatakuwa tayari kwa lolote.

“Msimamo wetu sisi Waislamu kama mambo yetu tuliyoleta katika mapendekezo hayataingizwa, basi yatabomokea hapa na hatutakuwa tayari tena,” alisema Sheikh Jongo, kauli iliyowashtua wajumbe.

Akihitimisha majadiliano hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge alisema kamati yake imefanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kwa masilahi ya Watanzania.

Akiahirisha Bunge, Suluhu alisema kesho Bunge litaanza kwa kupitia baadhi ya mambo yaliyoibuka katika uhakiki kisha kupitisha azimio la upigaji wa kura. Kura zitapigwa kati ya kesho hadi Oktoba 2.

Baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Sheikh mwingine, Hamid Jongo alimwendea Askofu mstaafu Donald Mtetemela na kumkumbatia, kisha kumvuta pembeni na kisha kuteta kwa dakika tano.

Katika viwanja vya Bunge, hali ilikuwa tete kwani kulikuwa na makundi tofauti tofauti ya Wakristo na Waislamu kila moja likijadili na kutafakari suala la Mahakama ya Kadhi kuingizwa kwenye Katiba.

Mjumbe wa kundi la 201 Dk Aley Nassoro alisema kuwa suala la Mahakama ya Kadhi lisipoingizwa katika Katiba inayopendekezwa, atakuwa wa kwanza kuhamasisha wenzake ili wagome kupiga kura.

Dk Nassoro alisema Waislamu wamechoka kudanganywa kwani tangu kipindi cha kampeni za mwaka 2010, waliahidiwa kuwa jambo hilo lingeshughulikiwa mapema lakini watawala wamekuwa kimya.

“Hii Katiba itakuwa ni mbovu kuliko ile ya mwaka 1977 na italeta migongano baada ya miezi sita tu tangu kuzinduliwa. Bora iachwe kwani mambo mengi ya msingi kwa Wazanzibari yameachwa,”alisema.

Akiwa viwanja vya Bunge Askofu Mtetemela alionekana akishauriana na wajumbe mbalimbali na baadaye alisema analaani kauli hizo na kusema kuwa hazilengi kujenga nchi badala yake zinabomoa.

“Kinachotakiwa ni amani, sasa tukianza kutishiana mambo hayatakwenda maana na sisi Wakristo tutataka mambo yetu yaingizwe humo, tunachohitaji ni amani na si vinginevyo,” alisema Mtetemela.

Askofu Mtetemela alisema kikubwa kinachotakiwa kwa wajumbe ni maridhiano na isiwe vitisho kwa kuwa walianza pamoja hivyo wanapaswa kumaliza pamoja.

Aliitaka Kamati ya Uandishi kutoingiza kabisa jambo hilo katika Katiba na akasema hali ikifikia hapo itasababisha mgogoro wa kimasilahi kwa kila mtu kudai haki yake ndani ya Katiba.

Hata hivyo, aliitaka Serikali kutunga sheria za kutambua uamuzi wa Waislamu wa ndoa, mirathi na umiliki wa rasilimali kwa Waislamu ili yakubaliwe kwenye sheria siyo kwenye Katiba.

Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, John Cheyo, alitaka Watanzania kuendelea kuheshimu Katiba ambayo imeweka wazi kuwa Serikali haina dini bali wananchi wake ndiyo wenye dini.

“Kwa sababu ukienda njia hiyo hakuna atakayeshinda. Na sisi Wakristo tuseme bila ‘Canon Law’ (Sheria za Kanisa) hakuna hatupigi kura, tutafika wapi? Ndiyo maana tuliyatenganisha haya mambo,”alisema.

Wakati makundi hayo yakiwa na msimamo tofauti, jana katika viwanja hivyo vya Bunge walisikika Waislamu wakihamasishana kwamba kama ikifika kesho hakuna Mahakama ya Kadhi wasusie Bunge.

Suala la Mahakama ya Kadhi, linaonekana kuwapasua kichwa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ambayo juzi na jana zilikutana kutafuta njia ya kulinusuru Bunge hilo na mpasuko huo mkubwa.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe walipendekeza kuitishwa kwa Kamati ya Maridhiano ili kutafuta njia bora itakayonusuru Katiba Mpya kukwama kesho.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment