Dar es Salaam. Serikali imewasilisha mahakamani pingamizi la kisheria dhidi ya maombi ya kusimamishwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma, kutokana na kesi ya kikatiba namba 28 ya mwaka 2014 iliyofunguliwa na mwanahabari, Said Kubenea.
Kubenea kupitia kwa wakili, Peter Kibatala alifungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiomba mahakama itoe tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo, huku akiambatanisha na maombi ya kusimamishwa Bunge hilo linaloendelea hadi kesi hiyo itakapoamuliwa.
Maombi hayo namba 29 ya mwaka 2014, yalitajwa jana mahakamani hapo, lakini Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju aliiarifu Mahakama kuwa, Jamhuri imewasilisha pingamizi hilo.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Dk Fauz Twaib na Aloysius Mujulizi.
Wakili Kibatala alilieleza jopo hilo kuwa tayati ameshapokea nakala ya hati ya pingamizi na yuko tayari kuanza kusikiliza pingamizi hilo. Jaji Mwarija alisema pingamizi hilo litasikilizwa leo.
Wakili Kibatala aliiomba Mahakama ikubali kusikiliza pingamizi hilo leo na maombi ya kusimamisha vikao vya Bunge kwa pamoja, kulingana na umuhimu na uharaka wa maombi hayo.
Mahakama ilikubaliana na maombi hayo ya wakili Kibatala na kuahirisha shauri hilo hadi leo saa tatu itakaposikiliza pingamizi hilo pamoja na maombi yenyewe.
Katika pingamizi lake, Jamhuri imeainisha hoja tatu, ikiwamo ya upungufu wa kisheria na hakuna kifungu cha sheria kinachoipa Mahakama mamlaka ya kutoa kinachoombwa na mlalamikaji.
Hoja nyingine ya Jamhuri inadai kuwa maombi hayo hayana maana na msingi wa kisheria. Pia inadai kuwa batili kisheria kwa kuwa hati ya kiapo inayounga mkono ina upungufu wa kisheria.
Pia Jamhuri ambayo ndiyo mdaiwa katika kesi hiyo kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imewasilisha pingamizi mahakamani dhidi ya maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda, huku ikiainisha hoja tatu za kisheria za pingamizi hilo.
Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba Mahakama itoe tafsiri hiyo, chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba 83 ya mwaka 2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya Bunge hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment