Wednesday, 3 September 2014

Sitta amshambulia Kubenea bungeni

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta.
Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amemshambulia Mkurugenzi Mtendaji wa HaliHalisi Publishers, Saed Kubenea kwa kitendo chake cha kufungua shauri mahakamani kupinga Bunge hilo.

Sitta alikwenda mbali na kumfananisha Kubebea na mchekeshaji wa mfalme huku akimtuhumu kuwa wapo wafadhili nyuma yake katika hatua yake hiyo.

“Karne za nyuma, karne ya 15, 16 na 17 wafalme kule Ulaya walikuwa na watu wao wanaitwa court jesters (wachekeshaji). Eneo la mfalme lilikuwa kama mahakama halafu kuna mchekeshaji,” alisema.

“Sasa wafalme wa Ulaya walikuwa wanaajiri wachekeshaji kwa malengo mawili. Moja ni kumsifia mfalme kwa kila kitu na jingine ni kuwasema wote wale ambao mfalme anahisi ni wabaya wake.

“Kwa hiyo kuna watu wa aina hiyo, tunawaona hadi sasa kama kina Kubenea, ni mchekeshaji wa mfalme tu. Yeye kuna mfadhili na wafadhili wako nyuma yake.”

Alisema wafadhili hao wanamsogeza kwa sababu wamemwona ana vipaji vya kufanya kazi kama hizo. Tuwaone nao kuwa kuna njia nyingi za kupata riziki tuwasamehe tu waendelee na shughuli zao”.

Akijibu madai hayo, Kubenea alisema: “Nimemsikia Sitta, lakini sijafahamu kama alikuwa anazungumzia kesi niliyofungua mahakamani au kazi zangu za uandishi wa habari, lakini madai kwamba natumika, yeye (Sitta) anajua kwamba sijawahi na sitawahi kutumika. Ninafanya kazi zangu kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwa masilahi ya umma.”

Alisema hata pale gazeti lake lilipokuwa linamwandika Sitta vizuri si kwa sababu alikuwa amewalipa, bali wakati huo alikuwa anasimamia haki na hata sasa anapomwandika upande wake wa pili, ndiyo ukweli wa jinsi alivyo.

Kubenea alisema Sitta anapingwa wakati huu kutokana na kitendo chake cha “kutumia Bunge la Katiba kunyofoa maoni ya wananchi katika kazi takatifu iliyofanywa na Tume ya Jaji Warioba.”
Sitta ajipigia debe urais
Sitta alitumia nafasi hiyo kujibu hoja zinazotolewa dhidi yake kuwa jinsi anavyoendesha Bunge Maalumu, amepungukiwa sifa za kuwania urais mwaka 2015 huku akijipigia debe kiaina katika nafasi kuwania nafasi hiyo.

Muda mfupi kabla ya Kamati 12 za Bunge hazijaanza kuwasilisha taarifa za kuhusu Rasimu ya Katiba, Mwenyekiti huyo aliweka wazi kuwa iwapo Watanzania watahitaji rais makini na mwadilifu mwaka 2015 basi wamfikirie pia yeye.

Alisema watu wanaojaribu kumpima kama anafaa kugombea urais 2015 kwa kuangalia yale yanayotokea katika Bunge Maalumu la Katiba wanampima kwa hoja duni.

“Wengine wananikejeli, wanasema kwa shughuli hii naonyesha sifai urais, mimi sijaomba urais. Naifanya kazi hii kama Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,” alisema Sitta na kuongeza: “Haya mengine rafiki yangu Juma Duni Haji (Makamu Mwenyekiti wa CUF) ananipima kwa hoja zilizo duni kabisa. Anajaribu kunipima eti... lakini nasema wanaochagua rais ni wananchi. Inawezekana mwakani wananchi wa Tanzania wakatamani mtu mzima, aliyetulia, asiyewaogopa wapuuzi, wakatamani hilo. Kama watahitaji mtu makini, mwadilifu basi wajue tu kuna sisi wengine tunaweza kufikiriwa kwa mambo kama hayo.”
Kuhusu Tume ya Warioba
Sitta alisema wananchi wengi wameonyesha shauku ya wajumbe kuendelea na vikao vya Bunge Maalumu la Katiba tofauti na inavyotangazwa.

“Makundi mbalimbali ya wananchi walioisoma rasimu yamebaini ina upungufu kama sisi, ndani ya kamati zetu tumeona hivyo na hilo siyo jambo la ajabu na wala si kupuuza kazi ya Tume,” alisema.

Sitta alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba ilifanya kazi yake vizuri lakini kama ilivyo hulka ya mwanadamu hakukosekani upungufu.
“Tukumbuke kuwa Tume ilipokea maoni kutoka kwa wananchi 334,000 na mabaraza zaidi ya 700.

Walichokileta ni tafsiri yao kuhusu maoni hayo, mnielewe vizuri,” alisema Sitta na kuongeza: “Walikaa wakachambua, mengine wakayaacha mengine wakayarekebisha. Ingekuwa kuleta maoni yote ingekuwa likitabu likubwa ambalo tusingeweza kulibeba.”

Sitta aliwasihi wajumbe wanaoendelea na bunge hilo kutofadhaishwa na matusi na kejeli wanazorushiwa huku akisisitiza kuwa yuko imara na hayumbi.

Kauli hiyo ya Sitta imekuja wakati makundi mbalimbali ya jamii wakiwamo wasomi, wanasiasa, viongozi wa dini na wanaharakati wakipaza sauti kutaka Bunge lisitishwe. Msingi wa kutaka kusitishwa kwa Bunge hilo ni kutaka kutafutwa kwanza kwa maridhiano kati ya CCM na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao wamesusia Bunge hilo.

Wajumbe wa Ukawa walisusia Bunge hilo tangu Aprili mwaka huu, wakipinga kitendo cha Bunge kuacha kujadili rasimu iliyobeba maoni ya wananchi na kuingiza mambo mapya waliyosema yana nia ya kubeba masilahi ya CCM.

CHANZO: MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment