Mahakama haina mamlaka ya kuamua ni kwa kiwango gani cha maboresho au marekebisho ambayo Bunge la Katiba linaweza kuyafanya katika Rasimu ya Katiba.” Mahakama |
Badala yake, mahakama hiyo imesema hayo ni masuala ya kisiasa zaidi
kuliko kisheria. Mahakama hiyo ilitoa msimamo huo jana wakati ikitoa
amri kuhusiana na kesi ya kuhoji mamlaka ya Bunge la Katiba, chini ya
kifungu cha 25(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Hata hivyo, haikutoa sababu za amri hiyo na badala yake ilisema kuwa
itatoa sababu hizo Oktoba 7. Kesi hiyo ilifunguliwa na mwanahabari, Saed
Kubenea dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa niaba ya
Serikali.
Katika kesi namba 28 ya mwaka 2014, Kubenea alikuwa anaiomba Mahakama
hiyo itoe tafsiri sahihi ya kifungu hicho kuhusu mamlaka ya Bunge na
pia, itamke kama lina mamlaka ya kuacha maudhui ya Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa bungeni.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Wakili wa Kubenea, Peter
Kibatala akisaidiana na Mabere Marando walisema kwa mujibu wa kifungu
hicho, bunge hilo lina mipaka na halina mamlaka ya kuacha maudhui ya
Rasimu hiyo.
Akijibu hoja hizo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju
alidai kuwa bunge hilo lina mamlaka ya kufanya mabadiliko yoyote na
kwamba, halifungwi na Rasimu hiyo kwa kuwa ni nyaraka ya kazi tu kwa
bunge hilo.
Katika amri yake jana, Mahamaka ilisema imebaini kuna utata na
mkinzano wa maana katika kifungu hicho katika lugha ya Kiswahili na
lugha ya Kiingereza.
Hivyo, mahakama kupiti jopo la majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo,
Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo), Dk Fauz Twaib na Aloysius
Mujulizi, ilitoa tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hilo baada ya kusoma
Sheria yote ya Mabadiliko ya Katiba
Ilisema licha ya utata huo, mamlaka ya kutengeneza masharti ya Katiba
Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamaanisha mamlaka ya kuandika
na kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupigiwa kura na
wananchi wa Tanzania.
Pia, ilisema mamlaka hayo yatatekelezwa kwa msingi wa Rasimu ya
Katiba baada ya kuwa imewasilishwa mbele ya Bunge la Katiba na
mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa kufanya hivyo, Bunge la Katiba linaweza kuboresha au
kuirekebisha Rasimu ya Katiba,” alisema Jaji Mwarija alipokuwa akisoma
amri hiyo.
Aliongeza: “Mamlaka hayo yana mpaka tu kama ilivyokuwa kwa shughuli
za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, katika misingi ya kitaifa na maadili
yaliyotolewa katika kifungu cha 9 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.”
Ilisisitiza kuwa hayo ni masuala zaidi ya kisiasa kuliko ya kisheria, isipokuwa tu bila kukiuka kifungu cha 9 (2).
Kifungu hicho kinasema: “Tume ya Mabadiliko ya Katiba itaongozwa na
misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya Jamii na kinataja mambo ambayo
ni sharti yahifadhiwe na kudumishwa, ikiwamo Jamhuri ya Muungano.”
Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Kibatala alisema wameridhishwa na
jinsi Mahakama ilivyoweza kutekeleza jukumu lake kwa wakati na
wamefurahi kuwa imeitambua Rasimu ya Katiba tofauti na mdaiwa alivyodai
kuwa hiyo ni nyaraka ya kazi tu kwa bunge hilo.
Alisema bado Mahakama haikuweza kukata kiu yake na ya mteja wake.CHANZO: MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment