Nembo ya Jeshi la Magereza. |
Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo (Wafungwa) na Mahabusu wameiomba Serikali kutafutiwa adhabu mbadala za kutumikia jamii kwa wanafunzi wanaopatikana na hatia kwa makosa madogo madogo ili kupunguza msongomano wa wanafunzi pamoja na Mahabusu gerezani .
Wakizungumza katika ziara ya Mahakimu wa Mahakama huko kiinua miguu Kilimani Zanzibar mwanafunzi Muhammed Hamza kwaniaba ya wezake amesema katika kuzingatia haki za binaadam yako makosa mengi ambayo Serikali ingalikaa na kuyatizama upya na kuyatafutia adhabu zitakazolingana na makosa hayo.
Hamza aliyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni wizi wa mazao, kuku ambapo alitoa mfano wa nazi mbili mtu anawekwa rumande miezi sita wakati kifungo chake inawezekana ikawa miezi miwili na mengine kama hayo.
Mwanafunzi huyo alitaja kutokuwepo kwa usawa wa sheria na kudai kwamba mara nyingi kunakuwa na viashiria vya rushwa katika upatikanaji wa haki na chuo cha mafunzo ni sehemu ya asokuwa nacho na mwenye nacho hastahiki, Sheria kutizama upande mmoja na mwengine kutofanyakazi wakati sheria haina mkubwa.
Alisema kuhusu upatikanaji wa mwenendo wa kesi mara zinapomalizika kwa kesi bado limekuwa tatizo sugu na kuchukuwa muda mrefu na hata waombaji kukata tamaa ya kukosa haki zao za msingi kupitia Mhimili huo wa Mahakama.
Kuhusu utaratibu wa upatikanaji wa dhamana ya rufaa kwa wanafunzi (wafungwa) wanaohukumiwa adhabu gerezani kuwa bado ni shida kupatikana wakati sheria ipo mtuhumiwa anaweza kubaki njee hadi rufaa yake yake itakapomalizika.
Akizungumzia dhamana za kawaida kwa kesi zilizopo Mahakamani Washitakiwa waliopo Rumande wamedai kuwa upo ubaguzi kwa wazanzibari na wazanzibara na vigezo wanavyowekewa ni vile ambavyo vinalenga kuwapa adhabu na sio haki za kisheria zilivyo.
Muhammed Hamza akitoa baadhi ya mifano kuwa kutolewa dhamana kwa Mansoor Yussuf Himid kwa kosa aliloshitakiwa nalo na wengine kubaki mahabusu kwa makosa ya aina moja ni ubaguzi, kutakiwa wadhamini watumishi wa Serikali wakati mwengine kunawanyima haki watuhumiwa walio wengi ambao hawana jamaa ambao ni watumishi wa serikali.
Madai mengine yaliyotolewa ni kuchelewa kwa kuanza kwa kesi Mahakamani na Mahakimu kutofanyakazi siku za Ijumaa wakati Mahabusu wanateseka gerezani na utaratibu wa kuwaita mashahidi hauko mzuri na kuchangia kesi kuwepo kipindi kirefu.
Gangira Charles ambae ni Mahabusu alitilia mkazo suala la haki ya dhamana kwa watuhumiwa na kunukuu Nakala ya gazeti la Mwananchi lililoandikwa kesi ya aliyekuwa Waziri wa SMZ Mansoor Yussuf Himid kupewa dhamana kwa kosa aliloshitakiwa nalo na wengine kubaki mahabusu kesi nyengine ni kesi za dawa za kulevya ambazo watuhumiwa wanamaliza Miaka bila kesi zao kumalizika kwa wakati na watuhumiwa kukaa ndani zaidi ya mwaka mmoja.
Gangira alishauri kwa Serikali kuandaliwa utaratibu utakaowezesha kesi zikasikilizwa kwa wakati ili haki zipatikane kwa wenye haki tena kwa wakati na dhamana zikitolewa kisheria mrundikano gerezani utaisha na Serikali haitakuwa na mzigo wa kuhudumia watu ambao wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa kwa kufanyakazi na kulipia kodi.
Wanafunzi hao wa rumande wakizungumzia vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Watuhumiwa wanapokamatwa na kufikishwa vituo vya Polisi wamedai kufanyiwa vitendo ambavyo haviendani na haki za binaadamu pamoja na kupoteza mali zao ambazo wanaziweka Polisi.
Gangira alisema kuwa vitendo vingine wanavyofanyiwa Polisi ni mateso bila ya kupatiwa matibabu wanapopata majeraha na vitendo vya udhalilishaji kinyume na haki za binaadamu.
Aidha wamemuamba mrajisi wa Mahakama kuandaa utaratibu wa Kamishna wa Polisi Zanzibar kutembelea gerezani na watendaji wake kusikia kilio chao ili kuweza kupatiwa ufumbuzi utakaosaidia kupatikana kwa haki.
Mahabusu hao kwa pamoja wametaja matarajio yao makubwa ya kufanyiwa kazi malalamiko yao ili kuona kilio chao cha muda mrefu kinaisha na sheria kufuata mkondo wake na wamesema hawana lengo la kujenga chuki kati ya watendaji hao na Mahakimu lengo lao ni kujenga misingi imara ya kuendeleza kazi zao.
Akijibu baadhi ya malalamiko ya Wanafunzi(Wafungwa) na Mahabusu Mrajis wa Mahakama Kuu Georg Kazi alisema ziara yao wamejifunza mambo mengi ikiwemo kuona hali halisi ya Wafungwa na Mahabusu wanavyoishi gerezani.
Mrajis alisema amepokea malalamiko yao na atayafanyia kazi ambapo kuhusu dhamana ya Mansoor kuwa imefunguwa mlango kwa watuhumiwa wengine kutumia kifungu cha 150(4) kuomba dhamana na wao waone Mahakama itafanyaje kutokana na kifungu hicho hakijawahi kutumiwa hapa Zanzibar na Mansoor ameanza na wengine wafanye.
Kuhusu malalamiko ya shutuma kwa Mahakimu na kujihusisha na vitendo vya rushwa na kutotenda haki ameahidi kulifanyia kazi kuyaondosha malalamiko hayo na suala la dhamana litaangaliwa, kupatikana kwa mwenendo wa kesi Proceed amesema tatizo ni miundombinu finyu kunachangia kuchelewa lakini tayari tatizo hilo linafanyiwa kazi.
Georg Kazi amewaomba kuisaidia Mahakama ili kuzimaliza changamoto ambazo zipo na kuonekana kuwa ni kero kwa jamii ambapo Wanafunzi(Wafungwa) na Mahabusu ndio wadau wakuu ambao wanazifahamu kasoro zilizokuwepo.
Amewataka kupeleka malalamiko yao wale ambao kwa muda mrefu kesi zao hazijatolewa hukumu na tayari zimemalizika na kwa muda hazijatolewa hukumu.
Awali Kamishna wa Vyuo vya Mafuzo Khalifa Haji Chum alisema ujio wa Mahakimu kutasaidia kuleta ufanisi na mashirikiano katika taasisi hizo muhimu ambazo zimebeba jukumu kubwa la kusimamia sheria za nchi.
Kamishna Khalifa amesema ziara za watendaji wanaohusika na moja ya majukumu yao kunasaidia kuona wapi kwenye mapungufu na kuyafanyiakazi ili kudumisha amani katika nchi ambayo ndio dira ya maendeleo.
Mapema Msaidizi Kamishna wa Vyuo vya Mafunzo Haji Vuai Usi alisema wapo wanafunzi 169 na Mahabusu 234 wakiwepo mfungwa mmoja mwanamke na watano mahabusu, watoto watano.
Nao Mahakimu waliotembelea gereza kuu la Kiinua Miguu wamesema wamejifunza mambo mengi katika ziara hiyo na kuiomba serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa taasisi hizi ili kupunguza au kuondosha kabisa matatizo yaliyopo ikiwemo miundombinu.
No comments:
Post a Comment