Monday, 8 September 2014

Zanzibar kufungua ofisi ya utalii India

Jengo la Ngome Kongwe lililopo Mji Mkongwe wa Zanzibar ambalo ni kivutio kikubwa kwa Watalii wanaotembelea Zanzibar.
Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kufungua ofisi maalumu nchini India itakayofanya kazi ya kujitangaza kimataifa na kutafuta masoko ya utalii kwa lengo la kuiongezea tija na uchumi wake .

Mpango huo umeelezwa na Mshauri wa Rais wa Mambo ya Utalii, Issa Ahmed Yussuf baada ya kubainika kuwa watalii kutoka India na China wanaingia kwa idadi ndogo.

Issa alisema mkakati huo ni katika utekelezaji wa Mpango wa Utalii kwa Wote unaolenga kutangaza utalii wa ndani na nje ili Zanzibar iweze kufikia lengo lake la kupokea watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020.

“Ofisi hiyo maalumu itafanya kazi ya kutangaza utalii, utafutaji wa masoko na kuiongezea Serikali mapato pamoja na kujitangaza kimataifa,” alisema Issa.

Alieleza kuwa hivi karibuni ujumbe maalumu ulifanya ziara katika nchi za India na China kwa ajili ya kuangalia masoko ya utalii na kuona ipo haja ya kuwapo kwa ofisi katika nchi hizo haraka ili kuitangaza sekta hiyo.

Alizitaja sababu zitakazoongeza watalii kuwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, miundombinu ya bandari na kuimarika kwa hali ya usalama kama ilivyo sasa.

Mshauri huyo wa rais alisema wageni kutoka China na India wamekuwa wazito kuitembelea Zanzibar kutokana na kukosekana kwa ndege za moja kwa moja kuja Zanzibar na tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza mazungumzo na mashirika mawili ya usafiri wa anga kimataifa.

Alisema tatizo lililopo China na kukosekana kwa watalii ni uwapo wa ofisi chache za ubalozi wa Tanzania katika miji ya Beijing na ubalozi mdogo Hong Kong huku kwenye miji mingine ya Shanghai na Gwanzou ikikosa ofisi za kibalozi.

Issa alisema Zanzibar imeishauri Serikali ya Muungano kufungua ofisi ndogondogo za utalii kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wageni wanapotaka visa za kuitembelea Zanzibar na Tanzania.

Alisema pamoja na sekta ya utalii kuwa tegemeo la kukuza uchumi wa Zanzibar bado soko la watalii linakabiiwa na kutojitosheleza kwa vyakula. maki,nyma,kuku na mbogamboga kutokana na uzalishji wa ndani kuwa mdogo.

Watalii takriban 170,000 hutembelea Zanzibar kila mwaka wakichangia asilimia 83 ya fedha za kigeni na pato la Taifa kwa asilimia 25 wakati nmwaka huu Zanzibar ikikadiria kupokea watalii 250,00 kutokana na kazi kubwa iliofanyika kuitangaza sekta hiyo nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment