Thursday, 4 September 2014

Bandua, bandika Bunge la Katiba

Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa kwenye kikao cha Bunge hilo Mjini Dodoma
TAARIFA za Kamati za Bunge Maalum la Katiba zinazoendelea kuwasilishwa bungeni, zimetoa taswira ya dhamira ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ya kuifutilia mbali rasimu iliyowasilishwa kwa Bunge hilo na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Tanzania Daima limebaini.

Rasimu hiyo iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba, inapendekeza muundo wa muungano wa Shirikisho la Serikali tatu, lakini CCM imeipindua na kurejesha muundo wa sasa wa Serikali mbili, licha ya kwamba Bunge hilo bado halijafanya uamuzi wa kura kwa sura ya kwanza na ya sita zinazohusu muundo wa muungano.

Katika taarifa hizo ambazo zinaendelea kuwasilishwa na wenyeviti wa Kamati za Bunge hilo, maoni ya wajumbe walio wengi yamefuta ibara nyingi za mapendekezo ya rasimu na kuingiza mpya, kurekebisha zingine na kuingiza Sura mpya kuhusu masuala kadhaa ambayo Tume ya Jaji Warioba iliyaacha yashugulikiwe na serikali za nchi washirika za Tanganyika na Zanzibar.

Sura mpya zilizoingizwa ni kuhusu Ardhi, Rasilimali na Mazingira, Serikali za Mitaa wakati suala la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kamati zimetofautiana kwa wajumbe wengine kutaka iingizwe katika Sura ya kumi na tatu ya rasimu inayohusu Taasisi za Uwajibikaji.

Baadhi ya Ibara muhimu za rasimu ambazo wajumbe wanapendekeza ama zifutwe na kuandikwa upya au zibadilishwe ili zisomeke tofauti na zilivyo sasa katika rasimu ni pamoja na 80 (1) (6) inayosomeka kuwa mgombea wa nafasi ya madaraka ya Rais, atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa Rais iwapo atapata kura zinazozidi asilimia 50 ya kura zote halali kwa nafasi ya madaraka ya Rais.

Maoni ya kamati nyingi, yanataka ibara hiyo sasa isomeke kwamba; mgombea wa nafasi hiyo atakayepata kura nyingi kuliko wengine, atatangazwa kushika madaraka ya urais.

Pia baadhi ya kamati zinataka ibara ya 81.-(1) inayompa haki mtu aliyekuwa mgombea urais na kushindwa kuwasilisha malalamiko yake Mahakama ya Juu kupinga uhalali wa msindi wa kiti cha urais, na sasa wanataka ifutwe na kuandikwa upya wakidai ni kuepusha nchi kuingia kwenye machafuko.

Taarifa hizo za wajumbe, zinapendekeza pia kufutwa maneno, “Serikali za nchi washirika” na kuweka “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika aya zote za Ibara yanapotajwa kwa kuwa muundo wanaopendekeza ni wa Serikali mbili.

Vile vile, wajumbe wanapendekeza Ibara ya 101.- (2) inayozuia mawaziri kutokuwa wabunge ifutwe kwa maelezo kwamba ili waweze kujibu hoja moja kwa moja zinazotolewa ndani ya Bunge.

CCM katika kuhakikisha wanayazika mapendekezo ya rasimu ya muundo wa serikali tatu, kamati zote zilizowasilisha maoni yake, zimependekeza Ibara ya 90 inayohusu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, ibara ndogo ya (1) irekebishwe kwa kufutwa na kuandikwa upya.

Kwa muundo wa serikali mbili wanaousimamia, CCM, wanarekebisha ibara hiyo ili kumrejesha Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Pili wa Rais, ambapo sasa itasomeka; “Kutakuwa na Makamu wawili wa Rais ambao watajulikana kama Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.

Shibuda na UKAWA
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), jana aliwafurahisha CCM kwa kuwashambulia wajumbe wa Bunge hilo wanaotambulika kama kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), akidai hawaungi mkono kwa sababu hawasimamii maslahi ya wananchi.

Shibuda ambaye alikuwa akiwasilisha maoni ya wajumbe walio wachache katika kamati namba nane, alianza kwa kumwomba Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan ampe dakika chache za kuleza kwa nini hakuungana na UKAWA kususia Bunge.

Alisema kuwa aliwauliza viongozi wa UKAWA, Freeman Mbowe (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), akitaka wamweleze maslahi ya makundi ya wakulima, wavuvi na wafugaji ndani ya UKAWA lakini wakashindwa.

Katika hali iliyoonesha kuwa Shibuda alilenga kuwashambulia viongozi wa CHADEMA, ambao wametangaza kumchukulia hatua kwa kusaliti msimamo wa Kamati Kuu, alitamba kuwa akiondoka CHADEMA atakwenda chama chenye nguvu ya kushika madaraka.

Huku akitumia misemo mbalimbali ya wahenga, Shibuda alijigamba kupambana na yeyote ambaye anamwandama kisiasa na kusisitiza kwamba, hakichukii CHADEMA bali utendaji wa viongozi wake.
Wakati Shibuda akiendelea kuwashambulia UKAWA huku akishangiliwa na wajumbe wengi ukumbini, Makamu Mwenyekiti, alimtaka ajitahidi kujiegemeza katika mjadala unaoendelea lakini yeye akajibu kuwa aliomba ruhusa kwake.

CHANZO: TANZANIA DAIMA.

No comments:

Post a Comment