Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Rashid Seif wakati akilijaribu moja ya gari hilo zilizotolewa na UNFPA katika hafla ilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar. |
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu (UNFPA) limekabidhi msaada wa magari manne ya Ambulance kwa Wizara ya Afya ya Zanzibar ambayo yatatumika katika Hospitali nne.
Mwakilishi wa UNFPA Tanzania Dkt. Natalia Kanem alimkabidhi Waziri wa Afya Rashid Seif Suleiman magari hayo katika sherehe zilizofanyika Wizarani Mnazimmoja.
Dkt. Natalia alitaka magari hayo yatumike kwa uangalifu ili kufikia malengo ya millennia ya kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto wanaozaliwa hasa katika maeneo ya vijijini.
Alisema moja ya sababu inayopelekea vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga ni tatizo la usafiri ambalo linachangiwa na uwezo mdogo wa baadhi ya familia hasa katika maeneo ya vijijini.
Aliongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya Mpango maalum wa Shirika la Umoja wa Mataifa ulioanza mwaka 2011 na kumalizika Juni 2015 ambao huenda ukaendelea hadi mwaka 2016 kusadia masuala ya Afya na Lishe.
Amesema mpango huo wa miaka minne ambao unahusisha maeneo makuu saba unaendeshwa kwa pamoja na Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa ambayo ni WHO, UNFPA, UNICEF na WFPA.
Mwakilishi huyo wa UNFPA amewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kkwete na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Muhamed Sheina kwa juhudi kubwa wanazochukua katika kuimarisha huduma za mama wajawazito na watoto wachanga.
Aliesema UN inathamini juhudi hizo na juhudi za kuimarisha uchumi hivyo aliahidi kuwa wataendelea kuunga mkono kuhakikisha mama wajawazito na watoto wanaozaliwa wanaendelea kuishi katika mazingira yaliyo salama.
Waziri wa Afya Rashid Seif Suleiman, alilishukuru Shirika la UNFPA kwa misaada mbali mbali inayotoa kwa Wizara hiyo na ameahidi kuwa magari hayo yatatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Amekiri kuwa tatizo la usafiri kwa mama wajawazito Zanzibar limekuwa likiwasumbua wananchi wengi na inafikia wakati akinamama hujifungua wakiwa kwenye gari wakati wa kupelekwa Hospitali ambazo hazina stara wala hazifai kwa kazi hiyo.
Alieleza matarajio yake kuwa tatizo hilo kwa sasa litapungua kwa kiasi kikubwa baada ya kupatiwa msaada huo ambao umekuja wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelekeza juhudi zake kuimarisha huduma za afya mijini na vijijini.
Gari hazo za ambulance ambazo zitapelekwa katika Hospitali ya Kivunge, Mwembeladu, Mkoani na Micheweni zimegharimu shilingi milioni 245,000,000 za kitanzania.
CHANZO: ZANZINEWS.
No comments:
Post a Comment