Tuesday, 16 September 2014

Mbowe atikisa Bunge na Polisi

Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe
Tamko la Mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe la kuitisha maandamano nchi nzima kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba imesababisha Jeshi la Polisi kumwita ili kutoa ufafanuzi wa kauli yake huku Bunge hilo likichepusha mjadala na kutumia muda mrefu kujadili hotuba hiyo.

Akizungumza jana na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho waliokuwa katika mkutano wa kuwachagua wajumbe wa Kamati Kuu, katibu mkuu na manaibu wake, Mbowe alisema ameitwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Isaya Mngulu, lakini hatakwenda hadi atakapomaliza vikao vya Chadema.

“Jana (juzi) nilitoa kauli ya kufanya maandamano nchi nzima, kauli hiyo imemfanya DCI kuniita…” alisema na kuongeza kuwa msimamo wake na Ukawa uko palepale.”

Mapema jana, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paulo Chagonja alionya kuwa endapo Mbowe atafanya maandamano kama alivyotangaza polisi hawatasita kumchukulia hatua za kisheria kwani hiyo ni mara ya pili kutoa onyo dhidi yake.

“Ni wazi kwamba siasa zina mipaka yake na zinapovuka na kwenda kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi zinageuka kuwa jinai na wala siyo siasa tena,” alisema.

Juzi, katika Mkutano Mkuu wa Chadema, Mbowe alitoa maazimio sita mazito ukiwamo utaratibu wa kuandamana nchi nzima kupinga Bunge linaloendelea.

Bunge lahama mjadala
Mjadala wa Bunge jana, ulipoteza mwelekeo baada ya wajumbe kadhaa waliopewa nafasi kuchangia, kuacha kujadili Katiba badala yake ‘kurusha makombora mazito’ dhidi ya hotuba hiyo, kwa wana Ukawa na Mbowe mwenyewe.

Baadhi ya wajumbe waliomzungumzia Mbowe na Ukawa ni pamoja na John Komba, Amos Makalla, Fahmy Dovutwa, Dk Mary Nagu na Mwenyekiti Samuel Sitta ambaye alikwenda mbali na kusema iwapo wajumbe hao wa Ukawa walimpigia kura ili awabebe katika mambo aliyoyaita ya kipuuzi, basi wasahau.

Kauli hiyo ya Sitta ilitokana na kauli ya Dovutwa kueleza kile alichodai ni kiini cha Sitta kushambuliwa na wajumbe hao wa Ukawa katika mikutano yao.

“Baada ya kuunda Ukawa, Mwenyekiti wa kikao Freeman Mbowe akasema jamani mgombea wetu ni Samuel Sitta. Huyu atalinda masilahi yetu. Tumekubaliana, lakini baadaye akasema yeyote tutakayemwona anashirikiana na CCM tutamfanyizia,” alisema Dovutwa.

Hata hivyo, Mjumbe wa Bunge hilo, Vicent Mzena aliomba mwongozo wa mwenyekiti akihoji inakuwaje Bunge hilo linajadili mambo yaliyotokea nje ya Bunge badala ya kujikita kujadili utungaji wa Katiba inayopendekezwa.

Akijibu mwongozo huo, Sitta alisema utayarishaji wa Katiba Mpya lazima mambo yote yanayohusiana na utungaji huo yasemwe bayana.

“Nashukuru sana Mheshimiwa Fahmy Dovutwa kwa kutupa undani wa mambo kwa sababu kama hao watu walidhani kwa kunipigia kura basi nitakubali upuuzi wowote basi kwa lugha ya siku hizi imekula kwao,” alisema Sitta.

Makala ambaye ni Naibu Waziri wa Maji, aliwafananisha Ukawa na kamati ya harusi inayogombania kupanga tarehe ya sherehe badala ya kujikita kwenye kukusanya michango kutoka kwa wajumbe.

“Nimpongeze Spika kwa kuweza kukaa na Ukawa kwa sababu kuishi na hawa ni sawa na kubeba gunia la misumari kwa namna wanavyodeka. Wamepotosha kila jambo tulifanyalo ili waonekane wana jipya licha ya ukweli kwamba wanapigania katiba ya wachache. Tunaopigania katiba ya wengi ni sisi tuliobaki.

“Nimesikia pale Profesa Lipumba (Mwenyekiti wa CUF-Ibrahim) akisema kuna ufisadi mkubwa lakini yeye mbona alipokuwapo hapa na alichukua posho? Kila tukikutana hapa anasema Makalla naona mambo yanakwenda vizuri. Wao kutoka tu imekuwa ni nongwa.”

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mbinga Mashariki, John Komba alisema, “Jana Mbowe amekuwa amiri jeshi na tayari ametangaza vita kwa kuandaa maandamano ya nchi nzima bila kibali cha polisi hata kama jeshi hilo litalazimika kutumia risasi za moto. Huyu ni mtu wa aina gani?

“Aliwasalimu wanachama wake kwa kusema ‘Ukawa…’ na wao wakajibu ‘Tumaini letu…’ Naomba nitangaze personal interest (masilahi binafsi) katika hili kwa sababu mimi ni Mkatoliki na tunaposema hivyo huwa tunamaanisha imani ya hali ya juu. Kwa hili nasubiri kauli ya maaskofu… wanapaswa kulikemea hili kwa nguvu.”

Komba amvaa Warioba
Komba aliendeleza mashambulizi yake kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kumwita mchochezi akisema amekuwa akiingilia mambo ya wajumbe kuwa wanakula fedha za wananchi bila ya kukumbuka kuwa hata yeye (Warioba) alikula fedha nyingi kuliko wabunge hao.

No comments:

Post a Comment