Miche ya |Mikarafuu. |
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema haina Ubaguzi wa aina yoyote katika kugawa Miche ya Mikarafuu badala yake inaangalia namna ambavyo Mkulima katayarisha mashamba yake kwa ajili ya kupanda zao hilo.
Afisa kutoka Kitengo Dhamana cha Utoaji wa Miche ya Mikarafuu Badru Kombo Mwenvura ameyasema hayo wakati alipokuwa akijibu tuhuma zilizotolewa na Wakulima wa Karafuu katika kijiji cha Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema si kweli kuwa Miche hiyo hutolewa kwa misingi ya itikadi ya Vyama na kwamba Kitengo husika cha kutoa Miche ya Mikarafuu huitoa kwa Mkulima yoyote aliyekamilisha masharti.
“Kwa kweli lazima tuweke wazi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijadhamiria kuwabagua wananchi wake na hasa Wakulima wa Zao la Karafuu katika kuwapatia Miche.
Miche inapotolewa Mtu haulizwi ni Mfuasi wa CCM au CUF badala yake wanakaguliwa Mashamba yao kama yamekidhi Vigezo”alifahamisha Mwenvura.
Afisa Mwenvura amesema Sharti kubwa la kupatiwa Miche hiyo ni Wakulima kuyatayarisha vyema Mashamba yao ili bwanaShamba watakapoenda kukukagua Mashamba yaonekane yapo katika hali nzuri.
Ameongeza kuwa kwa sasa Ari ya Upandaji wa Karafuu imeongezeka kutokana na Serikali kupandisha Bei na Hadhi ya Karafuu hivyo Wakulima wengi wameshajihika kulima hali inayoifanya Miche kuonekana Michache.
“Kwa Mazingira ya sasa lazima Miche ionekane kidogo maana Inatolewa bure na Karafuu thamani yake imepanda sana kila mtu anataka kulima karafuu lakini changamoto hii lazima tuishughulikie vyema mwakani” Alisema Afisa Mwenvura.
Afisa Mwenvura amewashauri Wakulima wanaojiweza kutayarisha Vitalu vyao binafsi vya Miche ya Mikarafuu ili visaidie badala ya kusubiri kutoka Serikalini.
Hata hivyo amewaahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizotolewa na Wakulima hao na kusema kuwa ataongeza jitihada binafsi ili kupatikana kwa Miche ya kutosha kwa Msimu wa upandaji unaokuja katika kijiji cha Mkwajuni.
Awali Wakulima hao walipokuwa wakitoa Maoni yao baada ya kumaliza Onesho la Sinema la kuimarisha Karafuu lililoandaliwa na Shirika la Biashara ZSTC kijijini hapo, waliishutumu Serikali kwa Kugawa Miche ya Mikarafuu kwa Misingi ya Ubaguzi wa Kivyama.
“Lazima ukweli usemwe kuwa Ubaguzi unaofanywa kwa Misingi ya uCCM na uCUF si pahala pake tupo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa,haina maana kabisa kuwa mtu akiwa Chama Pinzani akoseshwe Miche ya Mikarafu” Alisema mmoja wa Wakulima wa Mkwajuni Masoud Khatibu.
Shirika la Biashara la Taifa ZSTC linaendelea na Programu yake ya Sinema ya kuliimarisha Zao la Karafuu katika Vijiji Kisiwani Unguja ambapo Wananchi hupewa nafasi ya kuchangia na kuuliza maswali yanayolenga kuliimarisha Zao hilo la kibiashara nchini
Licha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuweka Sera ya kutoa miche ya Mikarafuu Milioni Moja kila Mwaka lakini kuna manung’uniko mengi kutoka kwa Wakulima wa Zao hilo kwamba Miche haiwafikii hasa katika Vijiji vya Kisiwa cha Unguja.
No comments:
Post a Comment