Tuesday, 23 September 2014

Bunge lapitisha upigaji kura kwa fax, email

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu la Katiba, Pande Ameir Kificho akijibu hoja za wajumbe waliochangia mjadala wa kupitisha marekebisho ya kanuni za bunge hilo mjini Dodoma jana.
Bunge la Katiba limeingia katika historia baada ya kupitisha kanuni zinazoruhusu wajumbe wake watakaokuwa nje ya nchi kupiga kura kwa njia ya nukushi (fax) na baruapepe (email).

Uamuzi huo ulifikiwa bungeni Mjini Dodoma, baada ya wajumbe wa Bunge hilo kupitisha azimio la kuzifanyia marekebisho kanuni ya 30, 36 na 38 za Bunge hilo za mwaka 2014.

Hata hivyo, wajumbe watatu kati ya 15 waliochangia azimio hilo, walipinga vikali marekebisho hayo, lakini yalipitishwa kwa wingi wa kura baada ya Mwenyekiti, Samuel Sitta kulihoji Bunge.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa raia wa Tanzania kupiga kura akiwa nje ya nchi, uamuzi ambao Sitta aliutetea akisema wanaoupinga wanachanganya kati ya kura ya uamuzi na kura ya uchaguzi.

Mwakilishi wa walimu, Ezekiah Oluoch alisema Kifungu cha 16 (6) cha Kanuni za Bunge kinamtaka mwenyekiti kuendesha Bunge kwa mujibu wa sheria walizonazo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na sheria nyingine za nchi.

“Hoja ya walioko nje ya Bunge hili kupiga kura, siiungi mkono na wengi mkiunga mkono mtakuwa mmekiuka sheria … kila raia ana haki ya kupiga, Katiba yetu inaeleza, ilimradi atimize miaka 18 lakini haki hiyo imewekewa pia utaratibu wa kisheria,” alisema.

Alisema kwa taratibu zilizowekwa nchini, hakuna unaomruhusu mtu aliyeko nje ya eneo la kupiga kura kufanya hivyo.

Hata hivyo, Sitta aliingilia kati akisema mjumbe anasema uongo, akimtaka aeleze ni kura ipi anayoizungumzia na kifungu gani kimesema hilo, naye akajibu kura anazozungumzia ni zote ikiwamo ya kufanya uamuzi ndani ya Bunge.

“Unasema uongo mtupu wewe … sheria ya uchaguzi, tunamchagua nani hapa?” alihamaki Sitta na hali kama hiyo aliionyesha pia kwa wajumbe wengine waliokuwa wakipinga marekebisho hayo.

Oluoch alisema anachoona ni kuwa si halali kwa mjumbe ambaye hayuko ndani ya Bunge kupiga kura na kutaka Bunge lisifanye mambo kwa sababu linataka kutimiza mambo ambayo si msingi wa sheria.

“Uamuzi wowote huo tunaotaka kufanya kwa lengo la kupata utashi wa kisiasa, mimi nitasimama peke yangu kukataa na itaingia kwenye hansard (kumbukumbu za Bunge) kwamba nilikataa jambo hili,” alisema.

Kwa upande wake, Said Arfi alisema hakubaliani na azimio hilo kwa sababu Kanuni ya 38 ilikuwa imeshaweka utaratibu na haoni kuwapo haja ya kufanya marekebisho.

“Jambo hili tunalofanya ni kubwa sana, kuandika Katiba ya Taifa letu ni lazima tuwe na nia zilizokuwa njema ili kulipatia Taifa Katiba ambayo itaridhiwa na Watanzania. Sioni sababu zozote za msingi kwa wajumbe ambao hawapo humu ndani kupiga kura.”

Arfi alisema uzoefu wa mabunge mengi duniani wanaopiga kura ni watu waliomo ndani ya ukumbi wa Bunge tu… “Sasa hii ya kwenda kuwatafuta watu huko waliko hauna uhakika anayepiga kura ndiye, ni shaka tupu.

Kwa kweli mheshimiwa mwenyekiti Watanzania watatutazama juu ya nia zetu na dhamira zetu juu ya kulipatia Taifa Katiba maridhawa,” alisema.

Alisema kura ni hiari na mjumbe anaweza kuwapo ndani ya Ukumbi wa Bunge na kuacha kupiga kura na kuonya kuwa kuwalazimisha na kuwatafuta watu ili wapige kura si jambo la kidemokrasia.

Wakati akiendelea, Sitta aliingilia kati na kumhoji nani anayelazimisha mtu kupiga kura? Arfi akamjibu;
“Unapotuingilia katika michango yetu Watanzania wanakupima. Watanzania wanakuheshimu mwenyekiti.”

Kwa upande wake, Ali Omary Juma alisema Katiba ni maridhiano ya nchi mbili huru na si busara kuharakisha kupiga kura kwa watu ambao hawamo ndani ya Bunge.

Alisema kama hilo litaruhusiwa itakuwa ni mgongano mkubwa wa kisheria ambao utaleta ufa mkubwa kama uliojitokeza baina yao na Ukawa … “Nashauri suala la kura tulisitishe ili kutoa fursa pana ya mashauriano na kutoa muda ili wajumbe wote tuhudhurie.”

Mjumbe Paul Makonda aliunga mkono hoja hiyo akisema wajumbe zaidi 600 kuwa mahali pamoja si jambo rahisi:

“Nakumbuka tukiwa kwenye kamati yetu siku moja mtu alilazimika kutoka hospitalini. Ni mgonjwa lakini afanyeje, lakini kama kuna uhuru wa kupiga kura pale alipolala ni jambo la heri.

“Hatutafuti kura mpya. Hapa tunatafuta kupiga kura kwa wale watu ambao walishajadili jambo hili, haina maana tunatafuta kuokotaokota kama tumepungukiwa, hatujapungukiwa hata kidogo.”

Baadaye Sitta alisimama na kusema ipo dhana inayojengeka kwamba utaratibu huo unalenga kulazimisha kila mjumbe kupiga kura ili tu theluthi mbili ipatikane, hivyo akataka wajumbe waache kupoteza muda … “Hii ni dhana ya ajabu na ina nia mbaya ndani yake. Mmoja wa watu ambao ameomba apige kura yuko hospitali India, nina mamlaka gani ya kumkatalia?”

“Tumempigia Balozi atamwapisha atapiga kura ya siri italetwa na itafunguliwa humu. Zote hizo zitafunguliwa humuhumu ndani ya ukumbi na majina yatasomwa,” alisema Sitta.

“Watakaopiga kura mbele ya mabalozi wetu kwa wazi, Record (kumbukumbu) yote italetwa hapa na mtashuhudia hapa majina yatatajwa moja moja kama kanuni zinavyotaka,” alisema Sitta na kuongeza;
“Mambo haya ni ridhaa ya mtu, hakuna mtu atalazimishwa. Kama kuna hao wanasimama hapa wanasema wanalazimishwa, kama wameshindwa kuchangia hoja hii wasipoteze muda.”

Akijibu hoja za wajumbe, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho alisema wakati wa kuhakiki mjumbe halali, wale walioko watawasilisha pasi za kusafiria.

Wasomi wapinga
Akizungumzia uamuzi huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema uamuzi huo ni dalili za kupaparika kwa sababu kila kona Watanzania wanapinga kuendelea kwa vikao vya Bunge hilo.

“Tanzania hatujafikia hatua ya kuruhusu wananchi wapige kura wakiwa nje ya nchi yao, iweje leo tukubali jambo hili kirahisi namna hii, kuna nini nyuma yake? Wanachokifanya bungeni wananchi wanakifuatilia na watambue wazi kuwa hiyo Katiba watakayoipitisha itapingwa.”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema, “Kama wamekubaliana kubadili kanuni sawa, ila lazima tujiulize kwa nini sasa. Kwa nini wabadili kanuni hizi ili kupiga kura tu?”

Dk Bana alisema hakuna ulazima wa kuharakisha mambo ili kupata Katiba Mpya kutokana na hali halisi iliyopo sasa.

“Nasubiri kwa hamu kuiona hiyo Rasimu wanayotaka kuipigia kura ili niilinganishe na iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kuanzia hapo tutaanza kuhoji kama mambo yatakuwa tofauti,” alisema.

Mwalimu wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu UDSM, Faraja Christoms alisema sheria za nchi zinatakiwa kwenda sambamba na Katiba ambayo ni sheria mama, hivyo kuruhusu upigaji wa kura wa aina hiyo ni kinyume na sheria.

Aliyekuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema, “Unaweza ukabadili kanuni lakini haitakuwa na maana kama hakutakuwa na maridhiano.”

CHANZO: MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment