Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa Bungeni mjini Dodoma. PICHA YA MAKTABA |
Wakati Waislamu wakishikilia msimamo huo, wajumbe ambao ni Wakristo
nao wamejipanga kupiga kura ya hapana endapo Mahakama ya Kadhi
itaingizwa katika Katiba inayopendekezwa.
Dalili za mpasuko huo zilianza kujitokeza jana asubuhi baada ya
mjumbe mmoja, Jaku Ayub Hashim kuwasha kipaza sauti akitaka kuzungumza
akisema ana jambo muhimu.
“Mheshimiwa tangu jana (juzi) ulisema utanipa nafasi ya mwanzo
nizungumze,” alisema Jaku, lakini Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu
alimtaka aketi chini na suala lake limesikika.
Suluhu akaendelea kuwapa wajumbe wengine kuendelea kuchangia na
baadaye alimpa Jaku muda wa dakika saba ili kuwasilisha kile alichotaka
kukizungumza ndani ya Bunge hilo.
Jaku alisema walipendekeza kifungu kinachotaka uamuzi unaohusu ndoa,
talaka na mirathi iliyoamuliwa kwa misingi ya dini ingizwe kwenye Katiba
inayopendekeza lakini hakimo.
“Ni kitu kidogo kabisa tuliomba kiongezwe lakini cha kusikitisha
kikundi cha sanaa kimeingizwa. Mimi binafsi yangu sitaunga mkono wala
mguu wala sitaipigia kura hii,” alisema Jaku.
Suluhu akamweleza kuwa angalizo lake limechukuliwa, na uongozi wa
Bunge pamoja na kamati ya Uandishi wanajitahidi kuingiza kila kitu
kinachowezekana, lakini kwa misingi na sheria za nchi.
Baadaye Sheikh Masoud Jongo alipopewa nafasi ya kuchangia, naye
alitahadharisha kuwa mambo yaliyopendekezwa na Waislamu yasipoingizwa
kama ilivyo kwa sasa, hawatakuwa tayari kwa lolote.
“Msimamo wetu sisi Waislamu kama mambo yetu tuliyoleta katika
mapendekezo hayataingizwa, basi yatabomokea hapa na hatutakuwa tayari
tena,” alisema Sheikh Jongo, kauli iliyowashtua wajumbe.
Akihitimisha majadiliano hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi,
Andrew Chenge alisema kamati yake imefanya kazi kwa uadilifu mkubwa na
kwa masilahi ya Watanzania.
Akiahirisha Bunge, Suluhu alisema kesho Bunge litaanza kwa kupitia baadhi ya mambo yaliyoibuka katika uhakiki kisha kupitisha azimio la upigaji wa kura. Kura zitapigwa kati ya kesho hadi Oktoba 2.
Baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Sheikh mwingine, Hamid Jongo
alimwendea Askofu mstaafu Donald Mtetemela na kumkumbatia, kisha kumvuta
pembeni na kisha kuteta kwa dakika tano.Akiahirisha Bunge, Suluhu alisema kesho Bunge litaanza kwa kupitia baadhi ya mambo yaliyoibuka katika uhakiki kisha kupitisha azimio la upigaji wa kura. Kura zitapigwa kati ya kesho hadi Oktoba 2.
Katika viwanja vya Bunge, hali ilikuwa tete kwani kulikuwa na makundi
tofauti tofauti ya Wakristo na Waislamu kila moja likijadili na
kutafakari suala la Mahakama ya Kadhi kuingizwa kwenye Katiba.
Mjumbe wa kundi la 201 Dk Aley Nassoro alisema kuwa suala la Mahakama
ya Kadhi lisipoingizwa katika Katiba inayopendekezwa, atakuwa wa kwanza
kuhamasisha wenzake ili wagome kupiga kura.
Dk Nassoro alisema Waislamu wamechoka kudanganywa kwani tangu kipindi
cha kampeni za mwaka 2010, waliahidiwa kuwa jambo hilo
lingeshughulikiwa mapema lakini watawala wamekuwa kimya.
“Hii Katiba itakuwa ni mbovu kuliko ile ya mwaka 1977 na italeta
migongano baada ya miezi sita tu tangu kuzinduliwa. Bora iachwe kwani
mambo mengi ya msingi kwa Wazanzibari yameachwa,”alisema.
Akiwa viwanja vya Bunge Askofu Mtetemela alionekana akishauriana na
wajumbe mbalimbali na baadaye alisema analaani kauli hizo na kusema kuwa
hazilengi kujenga nchi badala yake zinabomoa.
“Kinachotakiwa ni amani, sasa tukianza kutishiana mambo hayatakwenda
maana na sisi Wakristo tutataka mambo yetu yaingizwe humo, tunachohitaji
ni amani na si vinginevyo,” alisema Mtetemela.
Askofu Mtetemela alisema kikubwa kinachotakiwa kwa wajumbe ni
maridhiano na isiwe vitisho kwa kuwa walianza pamoja hivyo wanapaswa
kumaliza pamoja.
Aliitaka Kamati ya Uandishi kutoingiza kabisa jambo hilo katika
Katiba na akasema hali ikifikia hapo itasababisha mgogoro wa kimasilahi
kwa kila mtu kudai haki yake ndani ya Katiba.
Hata hivyo, aliitaka Serikali kutunga sheria za kutambua uamuzi wa
Waislamu wa ndoa, mirathi na umiliki wa rasilimali kwa Waislamu ili
yakubaliwe kwenye sheria siyo kwenye Katiba.
Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, John Cheyo, alitaka Watanzania
kuendelea kuheshimu Katiba ambayo imeweka wazi kuwa Serikali haina dini
bali wananchi wake ndiyo wenye dini.
“Kwa sababu ukienda njia hiyo hakuna atakayeshinda. Na sisi Wakristo
tuseme bila ‘Canon Law’ (Sheria za Kanisa) hakuna hatupigi kura,
tutafika wapi? Ndiyo maana tuliyatenganisha haya mambo,”alisema.
Wakati makundi hayo yakiwa na msimamo tofauti, jana katika viwanja
hivyo vya Bunge walisikika Waislamu wakihamasishana kwamba kama ikifika
kesho hakuna Mahakama ya Kadhi wasusie Bunge.
Suala la Mahakama ya Kadhi, linaonekana kuwapasua kichwa wajumbe wa
Kamati ya Uongozi ambayo juzi na jana zilikutana kutafuta njia ya
kulinusuru Bunge hilo na mpasuko huo mkubwa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe
walipendekeza kuitishwa kwa Kamati ya Maridhiano ili kutafuta njia bora
itakayonusuru Katiba Mpya kukwama kesho.CHANZO: MWANANCHI