Tuesday, 5 April 2016

Zanzibar kinakaribia kunuka


Viongozi wa CUF, akiwepo Maalim Seif Sharrif Hamad wakizungumza na waandishi wa habarikatika ofisi za chama hicho Vuga mjini Unguja.

MAALIM Seif Shariff Hamad, anayeaminika kuwa ndiye mshindi halali wa uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba, amegoma kufanya mazungumzo yoyote na Dk. Ali Mohamed Shein, aliyetangazwa kuwa mshindi wa urais.

Akizungumza na waandishi wa habari Vuga mjini Unguja, Maalim alisema, “siwezi kukutana na Dk. Shein na kujadiliana naye kwa lolote kuhusu mustakabali wa Zanzibar.”

Amesema,“…nikutane na Dk. Shein kwa lipi? Nakutana naye kama nani? Siwezi kufanya mazungumzo juu ya mustakabali wa Zanzibar na mtu ambaye yuko madarakani kwa kuvunja katiba.”

Maalim ameeleza hayo wakati akijibu swali la mmoja wa waandishi wa habari Visiwani. Ni muda mfupi baada ya Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Twaha Taslima, kusoma maazimio ya Baraza Kuu la Taifa la chama hicho.

Seif alikuwa i na kuweka msisitizo kwamba hakutakuwa na mazungumzo yoyote na kiongozi huyo ambaye kwa msimamo wa CUF hakupata ridhaa ya wananchi ya kuongoza Zanzibar.

Mwanasiasa huyo machachari Visiwani amesema, msimamo wake pamoja na CUF, ni kutomtambua Dk. Shein kama rais na kutoshirikiana naye kwa lolote na serikali atakayaoiunda.

Akijibu madai ya kwa nini anaendelea kutumia rasimali za serikali wakati haitambui serikali iliyopo, Maalim amesema, “nitaendelea kutumia walinzi na gari za serikali kwa sababu ni stahiki zangu.

“Situmii huduma hizi kama zawadi. Hapana. Hizi ni haki zangu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka (1984), Toleo la 2010.

Maalim Seif alikuwa makamo wa rais katika serikali iliyopita. Kabla ya kuanza mfumo wa vyama vingi, Maalim aliwahi kushika madaraka ya waziri kiongozi.

Amesema, kwa msingi huohuo, ni haki yake kutibiwa na kugharamiwa matibabu ndani na nje ya nchi.
“Ni stahiki zangu kikatiba. Mimi ni kiongozi tena mkubwa tu. Kwa yale yanayonistahiki kufanyiwa kisheria, isionekane kuwa siitambui serikali kwa hivyo nisihudumiwe. Ni haki yangu… isitoshe hizi fedha ni za wananchi nami nachangia kodi ama anavyochangia wengine. Hizi fedha hazitoki mfukoni mwa viongozi wa CCM,” ameeleza.

Kwa sehemu kubwa Maalim Seif alijibu maswali yaliyoelekezwa moja kwa moja kwake binafsi; na alitoa ufafanuzi kidogo kwa yale yaliyohusu zaidi uchaguzi wa Zanzibar na hatima ya mgogoro uliotengenezwa na Chama Cha Mapinduzi.

Akijibu maswali juu ya msimamo wa Baraza Kuu, Taslima ambaye aliteuliwa Oktoba mwaka jana kuongoza kamati ya uongozi ya chama baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu.
CHANZO: MWANAHALISI ONLINE.

No comments:

Post a Comment