Friday, 15 April 2016

Mapya ya Lugumi


IGP Ernest Mangu.

WAKATI leo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ikitarajiwa kupokea mkataba tata wa Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd, mapya yameibuka katika sakata hilo.

Kampuni hiyo inadaiwa kupewa tenda na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 vya polisi pekee na tayari kampuni hiyo imelipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha za mkataba.

Kamati ya PAC ambayo ilibaini kuwapo viashiria vya ufisadi katika zabuni, iliwaagiza watendaji wa jeshi hilo kuwasilisha taarifa za mkataba huo, lakini mkataba huo ulihamishwa na kupelekwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Hata hivyo mfanyabiashara anayemiliki kampuni ya Lugumi Enterprises, Said Lugumi anadaiwa kukimbia nchi, huku mkataba wake na Jeshi la Polisi ukipigwa danadana katika Kamati za Bunge.

Taarifa za kukimbia kwa mfanyabiashara huyo anayetajwa kuwa na ukwasi wa kupindukia katika kipindi kifupi, zilielezwa na baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola, ambapo anadaiwa kuwa alitoweka nchini usiku wa Jumatatu ya wiki hii.

Wakati Lugumi akidaiwa kukimbia nchi, taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili jana zinaeleza kuwa, mfanyabiashara huyo amekwenda nje ya nchi kununua mashine 94, ambazo bado hazijafungwa katika vituo vilivyosalia, ili kukamilisha idadi ya vituo 108.

Lugumi anayetajwa kuwa na uhusiano wa kifamilia na baadhi ya vigogo nchini, aliingia mkataba tata na Jeshi la Polisi mwaka 2011, kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi, lakini kazi hiyo haikufanyika kwa ufanisi licha ya kulipwa mabilioni ya fedha.

Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa mfanyabishara huyo amekwenda nje kununua mshine zilizosalia, kama njia ya kuzima mjadala kuhusu utata wa mkataba huo, ambao unaelezwa kumhusisha kigogo mmoja katika Serikali ya Rais Dk. John Magufuli.

“Lugumi amekwenda nje lakini hakutaka watu wajue na kaenda kununua vifaa ili wamalize kazi kwa Supersonic Speed and put (kwa kasi) kama njia ya kufunga mjadala,” kilisema chanzo chetu.

Juzi chanzo kimoja kililiambia MTANZANIA kuwa, mfanyabiashara huyo amekuwa akitembea na msafara mkubwa wa magari ya kifahari, huku akilindwa na walinzi maalumu wa kukodi alitoroka nchi wakati vyombo vya dola vikimuwinda.

“Ninashangaa vyombo vya habari mnashupalia Lugumi, Lugumi… mbona sasa ana siku ya tatu ameondoka nchini. Na inaweza kuwa amekwenda mafichoni.

“Pamoja na hali hiyo, lakini bado tunaendelea kumsaka ingawa baadhi ya idara zinazohusika na vyombo vya dola zimefanikiwa kufanya mahojiano naye ya kina kuhusu suala la mkataba wake wa kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi,” alisema mtoa habari huyo.

Licha ya Kampuni ya Lugumi kuingia mkataba na Jeshi la Polisi wa Sh bilioni 37, lakini bado mfanyabiashara huyo alilipwa Sh bilioni 46 nje ya mkataba, jambo linalozidi kufikirisha na kutilia shaka juu ya zabuni hiyo.

Sakata hili lilibainika wiki iliyopita baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kukutana na maofisa wa jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Utata
Katika sakata hilo inadaiwa kuwa Kampuni ya Lugumi Enterprises ilipewa zabuni ya kufunga mashine za ‘Biometric Access’ kwa ajili ya kuchukua alama za vidole ikiwa haina uzoefu wa kazi hiyo.

“Wamepewa mkataba sawa, lakini mbona taarifa zinaonyesha kuwa kampuni hii haijasajiliwa kama Biometric Access Company na haijawahi kufanya kazi zozote zinazohusiana na Biometric Access Control?,” alihoji mmoja wa wataalamu ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Pamoja na PAC kutaka mkataba huo, lakini katika hali ya kustaajabisha hoja hiyo iliandaliwa mazingira ya kuhamishwa na kupelekwa katika Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, ambapo mwenyekiti wake, Balozi Adadi Rajabu, alikiri mkataba huo kuwasilishwa mbele ya kamati yake.

“Mimi kama mwenyekiti wa kamati ninapenda kukiri kwamba tumepokea mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi na tutaufanyia kazi kwa kina.

“Tunahitaji kuona kama kuna wizara zilizohusika na mkataba huu na kama tutaukuta ni mbaya, tutatoa taarifa kwa umma. Kikubwa tunawaomba Watanzania wawe watulivu, hatuko kwa ajili ya kumlinda mtu wala kikundi cha watu, tunasimamia masilahi ya Watanzania wote,” alisema Balozi Adadi alipozungumza na gazeti hili juzi.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wamekuwa wakihoji sababu za mkataba huo kuhamishwa, wakati Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama haihusiki na masuala ya fedha.

“Ukitazama sakata hili, the main issue (jambo la msingi) ni fedha zilizochukuliwa ukilinganisha na kazi iliyofanywa, suala hapa si mashine za vidole hoja ni fedha.

“Kwa msingi huo, Kamati ya PAC ndiyo yenye jukumu la kukagua hesabu za Serikali, tangu lini Kamati ya Mambo ya Nje ikashughulika na hesabu?

“Wao kazi yao ni kuangalia diplomasia na masuala ya usalama, sisi hatuko huko shida yetu tunataka kujua kuhusu fedha za umma zilizopigwa mchana kweupe,” alisema mchambuzi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
CHANZO: MTANZANIA.

No comments:

Post a Comment