Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai. |
WABUNGE wamepania kuwaweka
kikaangoni Spika wa Bunge, Job Ndugai na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa
sababu tofauti katika Mkutano wa Bunge ulioanza Jumanne wiki hii, Raia Mwema
limeambiwa.
Wabunge hao wanatarajiwa kumbana Ndugai kutokana na kile kinachodaiwa kuwa “amekuwa upande wa serikali kuliko wabunge” katika kipindi chake kifupi cha kuwa Spika wa Bunge.
Mmoja wa wabunge waandamizi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema ingawa yeye hatashiriki katika mpango wowote wa kutaka kumuondoa Ndugai katika wadhifa wake huo, anafahamu kwamba kuna kitu “kinaendelea”.
“Mimi Ndugai ni rafiki yangu na kusema kweli siwezi kushiriki katika jambo lolote linaloweza kumuweka katika nafasi ngumu. Hata hivyo, ninazungumza na wabunge wengi wa CCM na upinzani lakini picha ninayoipata si nzuri.
“ Hawamzungumzi vizuri kusema kweli na mimi inaniuma kwa kweli. Kuna kina kitu nadhani kinaendelea lakini kwa sababu siko kwenye mipango ya kumshughulikia, siwezi kujua nini kimepangwa,” alisema mbunge huyo ambaye hata hivyo hakutaka kutajwa jina lake gazetini.
Raia Mwema limeambiwa kwamba mpango wa kumshughulikia Ndugai unaandaliwa kwa siri na kikundi cha wabunge wa CCM wakishirikiana na wengine kutoka katika vyama vilivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mtoa taarifa wa gazeti hili ambaye ni mmoja wa wabunge wapya katika Bunge la Tanzania, alisema wabunge wameudhiwa na mambo makubwa matatu katika utawala wa Ndugai ambaye amechukua nafasi ya Anne Makinda aliyekuwa Spika katika Bunge lililopita.
Ndugai, kwanza, anadaiwa kuwa amekubali kinachoitwa “mkakati wa serikali kulidhibiti Bunge” kwa kuruhusu Kamati za Uwajibikaji za Bunge kama ile ya Hesabu za Serikali (PAC) kuongozwa na wabunge wa upinzani wanaodaiwa kuwa na uwezo mdogo.
Vyama vilivyo ndani ya Ukawa, vikiongozwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (PAC), Freeman Mbowe, havijaridhika na ukweli kwamba wabunge ambao wao waliwataka kuwa wenyeviti wa kamati hizo za usimamizi, wamepelekwa katika kamati ambazo hazina ushawishi kwa jamii.
Kwa mujibu wa taratibu za kibunge kwa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, kamati za usimamizi zinatakiwa kuongozwa na wabunge kutoka katika vyama vya upinzani.
Hata hivyo, Kambi ya Upinzani Bungeni imekataa kushiriki katika uchaguzi wa kuchagua wenyeviti wa kamati hizo safari hii kwa maelezo kuwa ilitakiwa yenyewe ndiyo ipendekeze majina ya wajumbe wa kwenye kamati hizo wanaofaa kuwa wenyeviti.
Katika utetezi wake, Ndugai ameeleza kuwa alichofanya yeye ni kuwaweka wabunge katika kamati walizoomba kupangiwa na hawezi kulaumiwa kwa kufanya hivyo.
Kwa sasa, PAC na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zinaongozwa na Makamu Wenyeviti ambao ni wabunge kutoka CCM.
Lawama ya pili kwa Ndugai inatokana na wabunge wanne kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa; ambapo wapo wabunge wanaodai kuwa Bunge halikuwalinda dhidi ya tuhuma hizo.
Wabunge ambao tayari wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa ni Richard Ndassa, Suleiman Sadiki, Kangi Lugola na Victor Mwambalaswa; huku baadhi ya wabunge wakihamishwa kutoka kamati moja kwenda nyingine kwa tuhuma za rushwa.
Mmoja wa wabunge ambao wamefikishwa mahakamani alizungumza na gazeti hili Jumamosi iliyopita na kudai kwamba kwa wao kufikishwa mahakamani, taasisi nzima ya Bunge inaonekana kuwa haifai.
“Spika atasababisha wananchi watuone sisi hatuna maana. Sisi tunadhani kwamba hilo ndilo lengo kuu la serikali kwamba tuache kuisimamia ipasavyo kwa kuonekana ni wala rushwa.
“ Kama wabunge wataonekana ni wala rushwa, watakuwa na nguvu gani ya kuinyooshea kidole serikali kwamba iwajibike? Ndugai anaona hili ni jambo la kisheria lakini natamani angejua zaidi ya kinachoonekana kwa nje,” alisema mbunge huyo mashuhuri.
Sababu nyingine ya tatu inayodaiwa kuwafanya wabunge hao wajipange dhidi ya Ndugai ni kitendo cha Bunge kubana matumizi yake na kupeleka Ikulu shilingi bilioni sita ambazo Magufuli tayari amesema zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa madawati.
Kuna kundi la wabunge wanaoamini kwamba fedha hizo bado zingeweza kutumika kwa ajili ya shughuli za Bunge na wabunge; hata kama matumizi ya ununuzi wa madawati yatawanufaisha kwa vile yatapelekwa majimboni kwao.
Majaliwa
Uwezekano wa Majaliwa kuwa na wakati mgumu bungeni unajengwa na hoja zilizoanza kuibuka kwamba Rais Magufuli anafanya kazi za kugawa fedha ambazo kikatiba ni majukumu ya Bunge.
Mifano inayotolewa ni hatua ya Magufuli kuamuru fedha zilizopangwa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru kutumika kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha barabara mpya ya Bagamoyo (New Bagamoyo) kati ya Morocco na Mwenge na zile zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za Muungano zitumike kwa ajili ya upanuzi wa kipande cha Barabara ya Makongoro ya jijini Mwanza kati Nera na Uwanja wa Ndege.
Mtu wa kwanza kuhoji kuhusu jambo hilo alikuwa ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyezungumzia jambo hilo wakati akizungumzia utawala wa Magufuli.
Lowassa alidai kwamba kazi ya kupanga matumizi ya fedha ni ya Bunge na kwamba ni hatari kwa jambo hilo kufanywa na Rais. Raia Mwema limeambiwa kwamba ule ulikuwa ni ujumbe kwa wabunge wa Ukawa.
“ Kwa sababu Magufuli hatakuwa bungeni, mtu ambaye ataulizwa maswali ni Majaliwa. Yeye ndiye atajibu maswali kumhusu Magufuli. Nakuahidi kwamba sasa Majaliwa ndiyo atajua Uwaziri Mkuu si lelemama,” chanzo chetu kilisema.
Akizungumzia hoja hizo za dhidi ya serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, alisema hoja zote ambazo zitaletwa zitajibiwa ipasavyo.
“ Hakuna ambacho kimefanyika kisicho na maelezo. Walete hoja zao mezani na zitajibiwa kwa maelezo fasaha. Hatuna la kuficha na wananchi ni mashahidi wetu.
“ Ila wafahamu kwamba Rais Magufuli kwa sasa ni kipenzi cha wananchi wanyonge na walio wengi hapa nchini. Kila anachofanya wananchi wanamuona na kumuelewa na ndiyo maana wanamuombea kila siku,” alisema Simbachawene.
CHANZO: RAIA MWEMA.
No comments:
Post a Comment