Thursday, 21 April 2016

Ya Mwajuma na kina Msekwa


Pius Msekwa.

Na Ahmed Rajab.
KATIKA uhai wangu nimekutana mara moja tu na Pius Chipanda Msekwa. Sijui kama yeye anakumbuka. Kwa hakika, hana sababu ya kwa nini akumbuke au anikumbuke ingawa pengine hatopasahau nilipomkuta Jumatatu ya Machi 11, 2002 jua lilipokuwa limekwishatua.

Ama mimi siwezi kusahau mahala tulipokutana. Wala siwezi kumsahau.
Msekwa na mimi tulikutana sipo. Ninasema hivi hasa ukizingatia alikotoka na nilikotoka. Tulijikuta katika mazingira mageni yasiyo ya kawaida kwetu sote wawili, watoto wa visiwani — mtoto wa Ukerewe, Tanganyika, na mtoto wa Vuga, Zanzibar.

Tulikuwa katika ukumbi uliojaa mazulia kwenye Kasri ya Buckingham ya Malkia wa Uingereza, jijini London. Tulialikwa na Malkia Elizabeth katika hafla aliyoiandaa yeye na mumewe, Prince Philip, kuadhimisha miaka 50 tangu malkia huyo awe Mkuu wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth).

Nilizungumza na Msekwa kwa muda mfupi baada ya kumkabili na kujitambulisha kuwa mhariri wa jarida la Africa Analysis. Yeye hakuwa na haja ya kujitambulisha kwani nilikwishamtambua Spika wa Bunge la Tanzania. Kama sikosei, siku hizo alikuwa anamaliza muda wake wa miaka mitatu wa kuwa mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya Jumuiya ya Wabunge wa Jumuiya ya Madola (CPA).

Kazi kubwa ya Jumuiya hiyo ya CPA ni kuunga mkono jitihada za kupatikana utawala bora, demokrasia na kuheshimu haki za binadamu katika nchi za Jumuiya ya Madola. Mlezi wake ni Malkia wa Uingereza akiwa Mkuu wa Jumuiya ya Madola na ndio maana Msekwa alialikwa katika hafla ya kwenye kasri ya Buckingham.

Shughuli nyingine ya CPA ni kuandaa kila mwaka mkutano wa wabunge wa Jumuiya ya Madola.

Kwa hivyo, tunaweza kusema kwa uhakika kwamba Msekwa si mgeni wa dhana za utawala bora, demokrasia na haki za binadamu kwa vile amekuwa akihusika na dhana hizo katika kazi zake alipokuwa mmoja wa viongozi wa CPA.

Hata tukiiacha CPA, Msekwa lazima alikuwa akiyaelewa vizuri mambo yanayohusika na utawala bora na demokrasia kwa jumla.

Lakini labda kinachomchongea ni uzoefu wake wa kufanya kazi kwa muda mrefu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake akianzia na wadhifa wa Katibu wa Bunge. Wakati huo umri wake ulikuwa wa miaka 25.

Msekwa ametoka mbali na CCM toka uanaharakati wake ndani ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) alikolelewa kisiasa na ambako alikuwa Katibu Mtendaji Mkuu akiwa na umri wa miaka 32. Alizipanda ngazi za chama mpaka akafika kuwa naibu mwenyekiti wa CCM. Aliwahi pia kuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya CCM. Kuna wenye kusema kwamba yeye si kigogo wa chama bali ni gogo lenye kuzikalia siri nyingi za CCM na za vigogo wenzake wa chama hicho.

Zaidi ya yote yeye ni msomi kuliko kuwa mwanasiasa mwenye kupigana vikumbo na wanasiasa wengine mitaani. Kwa hivyo, binafsi alinishangaza aliponukuliwa akisema kwamba Rais John Magufuli hana uwezo wa kikatiba kuingilia sakata la Zanzibar na kwa matamshi yake mengine yenye kuashiria kwamba anawatetea walioibaka demokrasia Zanzibar.

Tuseme ni kweli kwamba Dk. Magufuli hana nguvu hizo na tuombe iendelee kuwa hivyo kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hana mamlaka au uwezo wa kikatiba au wa kisheria kuingilia kati migogoro ya Zanzibar kwa sababu hatua kama hiyo ina mushkili wake kwa uhuru na uungwana wa Zanzibar.

Hata hivyo, kuna mambo ambayo Magufuli angeliweza kuyafanya. Angeshindwa kikatiba lakini kwa kuyatekeleza mambo hayo angelishinda kwa uadilifu au tuseme kwa utu.

La kwanza ambalo angeliweza kulifanya ni kuipaza sauti yake kukemea yaliyokuwa yakifanywa na watawala wa huko Zanzibar. Kadhalika asingetoa idhini ya majeshi kutoka Bara kupelekwa Zanzibar, hatua ambayo ilionekana na wengi kwamba ilikuwa na lengo la kuwatia hofu wananchi.

Hatua nyingine ambayo angeliweza kuichukuwa, kama yeye kweli ni mpenda haki aliyechoka na usanii wa chama chake, ni kukishinikiza chama hicho kisijiaibishe na kuliaibisha taifa pamoja naye mwenyewe kwa kulazimisha kwamba lazima kionekane kuwa kinaibuka na ushindi huko Zanzibar.

Tumeona kwamba Magufuli aliweza kuchukuwa hatua kama hiyo kuhusika na uchaguzi wa umeya wa Dar es Salaam.

Angelichukuwa hatua kama hizo kuhusu Zanzibar basi tungeamini ya kuwa kweli ana nia ya dhati ya kutukwamua hapa tulipo si kwa Zanzibar tu lakini kwa taifa zima. Kwa sasa hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba anayo nia ya kuijenga Tanzania mpya.

Tunachokishuhudia ni mbwembwe zenye kuuficha usanii unaoendelea ndani ya CCM. Ni usanii huo unaowafanya wengi wasiamini kwamba ndani ya chama hicho kuna kiongozi mwenye nia safi na mustakbali wa taifa hili.

Juu ya mbwembwe na vishindo vya Magufuli si Watanzania wote wanaoamini kwamba serikali yake kweli imeazimia kuijenga Tanzania mpya. Mmoja wa wasiohadaika na dhamira za CCM ni Mwajuma binti Kishana (silo jina lake la kweli). Yeye haamini kabisa kwamba mfumo wa utawala utabadilika chini ya uongozi wa CCM.

Kiasi aamini hivyo kwa sababu kwa vitendo na matamshi yao viongozi wa juu wa CCM wameuthibitishia ulimwengu kwamba wao ni watu wasio na insafu wala uadilifu, hususan kuhusu suala la Zanzibar. Hawanishangazi kwa wayafanyao na wayasemayo.

Wanaonishangaza na kunikanganya ni wapambe wao walio wasomi, kama Msekwa, na wale wasomi wetu ambao kama mimi wanafuata siasa za mrengo wa kushoto.

Kwa nini nao wakawa wanakosa uadilifu wanapolijadili sakata la Zanzibar? Nimekuwa nikijiuliza swali hilo kwa muda mrefu lakini bado sijapata jawabu yenye kuniridhisha.

Sidhani kwamba wasomi hao hawautambui ukweli au kwamba hawaamini, kwa mfano, ya kuwa haki haikutendeka pale watawala walipoufuta uchaguzi wa Zanzibar wa Oktoba 2015.

Wanalielewa hilo vizuri. Lakini wamehiyari kujipendekeza kwa watawala. Na ndio maana tunawaona wakijitolea wakiwa katika safu za mbele wakishika majembe, wakichimba makaburi na wakijaribu kuuzika ukweli, haki na demokrasia yetu iliyochanga.

Wako tayari kuzipuuza athari za kiuchumi ambazo zitaikumba Tanzania nzima kwa vitendo vya wachache vinavyolifanya taifa zima lijivunjie heshima yake.

Jambo moja wanalolifanya hawa watawala wetu na wasomi wao wenye kujaribu kuwakinga kwa hoja zao ni kuukimbilia uzalendo kwa kuuponda ubeberu.

Kuulaumu ubeberu na kuukimbilia uzalendo ni njia rahisi inayotumiwa na watawala wakishirikiana na baadhi ya wasomi kujaribu kuwapa wananchi sura isiyo ya kweli ya hali ya mambo ilivyo. Wakati huohuo huwa ni jaribio la kukataa kujikosoa kwa kuukanya ukweli.

Wanafikiri kuwa ni njia ya mkato ya kujitoa kimasomaso lakini kwa kweli huwa ni njia ya kujidanganya na kuuhadaa umma. Haitupi uelewa wa hali halisi ilivyo.

Wenye kufanya hivyo wanakuwa wanauficha udhaifu wao. Kadhalika wanakuwa wanawaacha na hawawajali watawala wa ndani ya nchi na maslahi yao.

Tabia nyingine mbaya waliyo nayo baadhi ya wasomi wetu, hasa wa mrengo wa kushoto na wale wenye kujitia kuuweka mbele uzalendo, ni yale mazoea yao ya ukasuku. Badala ya kuwa watu makini, wenye kupima mambo na kufanya uchambuzi halisi wa hali halisi ilivyo wasomi wa aina hii hupendelea kujifanya kasuku kwa kukariri kikasuku mawili matatu waliyoyaokota vitabuni.

Tunafanya kosa kubwa sisi wa mrengo wa kushoto tunapokuwa tunaidekeza hii hulka tuliyo nayo baadhi yetu ya kuukwepa ukweli unapotukabili usoni. Hali hii hujitokeza zaidi pale mahasimu zetu wa kiitikadi wa kutoka nchi za Magharibi wanapowafuma viongozi wetu wanapokuwa wanazipora haki za wananchi.

Nadhani hii ni moja ya sababu kwa nini wananchi wenzetu wasiofuata itikadi zetu za mikondo ya fikra za kushoto huwa wanatutoa maanani, wanatufanya watu tusio na thamani. Wakituangalia na kutusikiliza wanatushangaa na wanazidi kuwa baidi na sisi, kuwa mbali na fikra yetu.

Hawaelewi kwa nini tuwe tunajali ubeberu unapofanya njama za kuipora demokrasia, kwa mfano, nchini Venezuela na tukapuuza kama hakuna lililotokea pale watawala wetu wanapoipora demokrasia kwetu.

Sikatai kwamba ubeberu upo, u hai, ni muovu na unaendelea na njama zake za kuwanyonya wanyonge. Sikatai pia kwamba ulibirali mamboleo unaendelea kuzikoroga akili za wenye kutunga sera za nchi yetu, sera ambazo haziwezi kuwapatia wananchi maendeleo wanayostahiki kuyapata bila ya kuwaumiza kiuchumi.

Wala sikatai kwamba tunapaswa kuwa wazalendo na kuupiga vita ubeberu popote pale duniani unapojitokeza na mwisho sikatai kwamba tunawajibika kuzikosoa sera za ulibirali mamboleo kwani sera hizo, kwa jumla, hazina kheri nasi.

Ninachokikataa ni kuukimbilia uzalendo na kuufanya ngao ya kujihami kila serikali zetu zinaposhambuliwa na nchi za Magharibi kwa maovu ya serikali zetu wenyewe. Wenye kufanya hivyo wanaugeuza uzalendo na huufanya uwe kimbilio la waovu na wakorofi wa kisiasa wenye kuhalalisha madhambi ya kisiasa.

Kila wanapofanya makosa wakakosolewa au wanapodhulumu haki za wananchi na wakaambiwa kwamba wanadhulumu huanza kuwapaka tope wenye kuwalaumu na kuwasingizia kuwa eti wanatumiwa na watu wa nje wasiolitakia mema taifa.

Na kila watawala waovu wanapochukuliwa hatua na wafadhili wao huwakimbilia wananchi na kuwaambia wajikaze, wajitegemee, wawe wazalendo na wasikubali kushurutishwa na mataifa ya nje.

Sidhani kama hamna kabisa watu wenye busara ndani ya CCM kama Mwajuma anavyodhania ila, nafikiri, hao waliopo na wenye ujasiri wa kusema kweli ni wachache mno. Wengi wao wanakijali zaidi chama chao kushinda uzima wa taifa.

No comments:

Post a Comment