Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya OIC. |
Rais wa Uturuki Tayyip Recep Erdogan
anahitimisha mkutano wa viongozi wa nchi za kiislamu unaolenga kupunguza
tofauti za kimadhehebu hasa kuhusu mizozo ya Syria na Yemen na kushughulikia
kitisho cha ugaidi.
Katika dhifa ya chakula cha jioni
hapo jana aliyowaandalia viongozi wa nchi za kiislamu wanaohudhuria mkutano huo
wa kilele wa jumuiya ya ushirikiano ya mataifa ya Kiislamu OIC, Rais Erdogan
amekariri haja ya kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa waislamu wote.
Erdogan amesema lengo ni kuwapa
waislamu matumaini kuhusu siku za usoni na kutokana na mkutano huo, wanatarajia
ukurasa mpya utafunguliwa.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria
mkutano huo wa OIC ni Mfalme Salman wa Saudi Arabia na Rais wa Iran Hassan
Rouhani ambao nchi zao zimekuwa zikitofautiana vikali na kuchukua misimamo
tofauti kuihusu mizozo ya Yemen na Syria.
Wasunni na Washia wahimizwa kupendana
Rais Rouhani ambaye pia alizungumza
katika mkutano huo amesema hakuna ujumbe ambao unachochea mgawanyiko miongoni
mwa Waislamu unapaswa kutolewa katika mkutano huo.
Uturuki inayoutazama mkutano huo
kama jukwaa la kuinua hadhi yake katika ulimwengu wa kiislamu pia nchi hiyo
imepata fursa ya kuwaleta pamoja waislamu takriban bilioni 1.7 kutoka duniani.
Erdogan ambaye nchi yake inashikilia
wadhifa wa uenyekiti wa OIC kwa kipindi cha miaka miwili ijayo anatarajiwa
kuongoza kikao cha mwisho cha mkutano huo ulioanza tangu jana leo kabla ya
kufanya mkutano na wanahabari.
Viongozi hao wa nchi takriban 30 za
kiislamu wamekubaliana kushirikiana zaidi katika kupambana dhidi ya ugaidi na
uhalifu mwingine na kuundwa kwa kituo cha kushughulikia ushirikiano zaidi wa
polisi wa nchi wanachama wa OIC ambacho kitaanzishwa Istanbul.
OIC ina nchi wanachama 57
Mkutano huo wa OIC unakuja wakati
ambapo Uturuki inaonekana kutafuta ushirikiano zaidi na Saudi Arabia. Hapo jana
mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili walitia saini makubaliano ya
maelewano kuhusu kuundwa kwa baraza la ushirikiano wa nchi hizo mbili.
Uturuki, Saudi Arabia na Qatar
zinawaunga mkono waasi wanaompinga Rais wa Syria Bashar al Assad. Kwa upande
mwingine Iran na Urusi ambayo ina uhusiano mbaya katika siku za hivi karibuni
na Uturuki zinauunga mkono utawala wa Rais Assad.
Wachambuzi wameonya kuwa Uturuki
inapaswa kutahadhari kuhusu ushirikiano wake na Saudi Arabia ili isije
ikaonekana kuwa na uhusiano wa misingi ya kimadhehebu unaoilenga Iran.
Katika hatua ya Uturuki kujaribu
kusawazisha hali, Rais Rouhani anatarajiwa kuanza ziara rasmi Uturuki ya
kuimarisha uhusiano kati ya Iran na Uturuki punde baada ya kukamilika kwa
mkutano huo wa kilele wa OIC. Shirika hilo la ushirikiano wa mataifa ya
kiislamu lina wanachama 57.
CHANZO: DW.
No comments:
Post a Comment