Friday, 15 April 2016

Rais tumbua majipu lakini usisahau…..(1)



Joseph Mihangwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli.

Na Joseph Mihangwa.
SI siri tena kwamba Tanzania imegubikwa na ufisadi wa kutisha, mkubwa na wa aina yake Afrika Mashariki kama si barani Afrika.

Ufisadi huu, ulioanzia Serikali ya Awamu ya Pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi kwa kubinafsisha kila kitu kilichokuwa cha umma, kwa usiri mkubwa, mizengwe na kwa bei ya kutupa, uliongeza kasi wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya Rais Benjamin William Mkapa.

Walifanya hivi kwa njia ya uwekezaji tata na usiojali, ambapo wawekezaji walipewa (kukalia) kiti cha mbele katika uchumi wa taifa, kwa mikataba ya uwekezaji mibovu iliyowaruhusu kupora watakavyo, kiasi cha nchi yetu kugeuzwa “Shamba la Bibi”

Kipindi hicho, tumeshuhudia kashfa kubwa kubwa za ufisadi zenye kuatamiwa kwa machukizo ya Umma, kama ile ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL/TANESCO), ambapo nchi imeporwa mabilioni ya fedha kwa mkataba wa umeme tata wa miaka 20 kuanzia mwaka 1999.

Chini ya mkataba huu, nchi imetupwa gizani kwa kukosa umeme, lakini inaendelea kuilipa IPTL zaidi ya Shs. 5bn/= kwa mwezi bila kujali, umeme uwepo au usiwepo; tutumie au tusitumie, kwa sababu mkataba huo mbovu uliofikiwa mwaka 1995 unaelekeza hivyo.

Walioliingiza Taifa katika “mkenge” huu wanafahamika kwa vyeo na kwa majina; lakini wapo huru wanapeta.

Kashfa zingine zenye kuangamiza ustawi wa taifa ni pamoja na zile za EPA, ununuzi wa rada na ndege ya Rais; ubinafsishaji wa NBC na uuzaji wa nyumba za serikali; Mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, Richmond/Dowans, mikataba mibovu ya madini; Loliondo, na ufujaji wa zaidi ya bilioni 800/= za mfuko wa kuwezesha uagizaji bidhaa (CIS), kwa kutaja kashfa chache tu.

Na kama tusingeshtuka, manyang’au hawa walikuwa wamepania pia kuhujumu mifuko ya akiba ya wafanyakazi kwa kujichotoa mabilioni ya fedha kwa njia ya ushiriki katika vitega uchumi vya mifuko hiyo

Na ingawa ufisadi huu unafahamika vizuri, na wahusika wanajulikana kwa serikali (ikiwamo serikali ya awamu ya nne), juhudi zimeendelea kufanywa kuatamia uchafu huo, na wahusika kuoshwa kwa sabuni kali ili, kwa hadaa kubwa, waweze kumeremeta machoni mwa umma.

Kwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii, tunayo mifano kadhaa: mwaka 1996 Waziri Mkuu wa wakati huo, kwa kutumia nafasi yake, aliweza kukopeshwa shs. 57m/= kutoka Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PPF) nje ya sera na taratibu za ukopeshaji za mifuko ya hifadhi ya Jamii nchini na duniani kote.

Vivyo hivyo, mwaka 2006, mfanyabiashara mmoja maarufu Jijini Dar Es Salaam (jina tunalo), alikopa kutoka Shirika la Hifadhi ya Jamii Nchini (NSSF) kwa taratibu za kutatanisha, Shs. 9bn/= kwa ajili ya kukarabati maghala yake, na baadaye kuiuzia NSSF maghala hayo kwa bei ya shs. 47bn/=, bei ambayo hata wathamini majengo wa serikali iliwaacha mdomo wazi.

Hakuishia hapo; mwaka huohuo, na katika kipindi hicho hicho; mfanyabiashara huyo, aliuuzia Mfuko wa Pensheni wa Watumishi Serikalini, maghala mengine kwa bei ya Shs. 39bn/= ambayo, kwa mujibu wa wathamini wa serikali, ilikuwa juu maradufu ya bei halisi ya mghala hayo.

Hizo ndizo zilikuwa enzi za mwanzo kabisa za utamaduni wa kukwapua mali ya umma mingoni mwa wanasiasa na watawala, kwa kushirikiana na kada ya wafanyabiashara, kuota mizizi.

Utafiti makini umeonesha kwamba, katika juhudi za kujiponya, wahujumu hao ama walikimbilia kunyakua (kupora) nafasi za kisiasa wapate kinga ya kisiasa, au waligeuka kuwa wafadhili wakubwa wa chama tawala na kampeni za uchaguzi ili walindwe na kusafishwa. Janja yao hii imeweza kufanikiwa japokuwa kwa muda; wakajiona wako salama wakati usalama wa kweli haupo.

Lakini pamoja na hayo, licha ya chama na serikali kujitahidi kuzisafisha kashfa mbalimbali za ufisadi ziweze kumeremeta, kashfa moja kabambe nchini, ya mradi wa Mgodi wa Meremeta imeshindwa kumeremeta, na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitaka Serikali iwasilishe hesabu za kampuni hiyo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zikaguliwe ili kukata mzizi wa fitina.

Kampuni ya Meremeta, ambayo inadaiwa kutosajiliwa chini ya Ofisi ya Hazina kama kampuni au shirika, ilichota malipo tata zaidi ya Shs. 155bn/= zilizolipwa na Benki Kuu (BOT) kwa kampuni ya Nedcor Trade Service, baada ya udhamini wa kampuni yenye hisa ya Triennex (PTY) Limited ya Afrika Kusini. Malipo haya na mengine, kama tutakavyoona badaye, ndiyo yaliyozua utata na Bunge kuagiza mahesabu yakaguliwa.

Katika makala haya, tutaona na kufahamu kama ni kweli kampuni ya Meremeta ni ubia wa serikali na kampuni ya Triennex, unaohusisha Jeshi letu la Ulinzi, kama inavyodaiwa, na pia kuhusisha usalama wa taifa. Tutaona ni kwa vipi, makampuni mengine kama Deep Green Finance na Tangold (yanavyoguswa na kashfa hii) yalivyoingia; na kwa nini serikali inajiuma mdomo na kukunja mikono yanapotajwa.

Lakini ifahamike kwa misingi ya sheria kwamba, kitendo cha mtu kufunika kombe au kuatamia kosa lililotendwa na mtu mwingine, kwa lengo la kumwepusha mtu huyo mwingine sheria isichukue mkondo wake dhidi ya mtu huyo; au kosa alilotenda lisijulikane, kinamfanya mtu huyo mwenye kutaka kumwokoa huyo mtu mwingine na yeye kuwa mshiriki wa kosa hilo kwa kiwango sawa na cha mtuhumiwa halisi wa kosa.

Kwa hiyo, viongozi wanaowalinda au kuwasafisha mafisadi wana hatia ya ufisadi uleule wa wale wanaojaribu kuwaokoa.

Huu ndio utamaduni wa kulindana kwa maovu, unaoshika kasi nchini kwa machukizo ya umma; kana kwamba viongozi na washirika wao wana kinga ya kimsahafu (Luka 12:32) kwamba, “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa baba yenu (mfumo wa kifisadi) ameona vema kuwapa ule ufalme - (wa ulaji?)”

Kampuni ya Meremeta iliandikishwa na kusajiliwa nchini Uingereza Agosti 9, 1999 (kwenye kisiwa cha Isle of Man) na kupewa namba ya Usajili 3424504; lakini serikali yetu inadai ni ubia kati ya serikali ya Tanzania yenye asilimia 50 ya hisa, na Kampuni ya Triennex ya Afrika Kusini, inayomiliki hisa asilimia 50 pia.

Utata unaongezeka pale inapodaiwa kuwa, Makampuni ya London Law Serivices Ltd, na London Law Secretarial Ltd, nayo ni wanahisa wa Meremeta.

Madhumuni ya kampuni hiyo yalielezewa kuwa ni kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogowadogo nchini, pamoja na kuwasaidia zana za kufanyia kazi. Swali linalojitokeza hapa ni kwa vipi kampuni inayomilikiwa na serikali, na ambayo shughuli zake zinafanyika hapa hapa nchini na kwa misingi ya usalama wa taifa, iandikishwe na kusajiliwa katika nchi ya kigeni?.

Kati ya mwaka 2003 na 2005, kampuni hii ilitelekeza wajibu na “madhumuni” ya kuanzishwa kwake na kuanza kuchimba dhahabu yenyewe huko Buhemba, Musoma. Hapo ndipo hadithi ya Meremeta kuhusisha usalama wa taifa ilipoanza; hapo ndipo hadithi ya Meremeta kujihusisha kusaidia kiwanda cha magari cha Jeshi cha Nyumbu (Pwani) ilipoanza kupikwa na kusikika.

Ikumbukwe kuwa, katika kipindi hicho (2003 – 2005), kiwanda cha Nyumbu kilipangiwa fedha kutoka serikalini jumla ya Sh. Milioni 950 kwa ajili ya kutengeneza magari 21 ya kijeshi, kwa wastani wa 45.2m/= kwa kila gari, na hakukuwa na fedha zaidi zilizoingia kutoka vyanzo vingine kipindi hicho.

Ukweli juu ya kwamba mradi wa Meremeta haukuhusika kwa namna yoyote ile na Jeshi la Wananchi, unathibitishwa pia na Waziri wa Ulinzi, Philemon Sarungi, katika hotuba yake ya bajeti ya 2004/2005, aliposema: “Mradi wa Buhemba umejengwa katika eneo lililokuwa Kambi ya Jeshi, na shughuli za uchimbaji na uzalishaji zinasimamiwa na Idara ya Madini”.

Kile tu kwamba mradi huo ulijengwa mahali ambapo zamani ilikuwa Kambi ya Jeshi, hakiufanyi uwe mradi wa Jeshi wenye kuhusishwa na Usalama wa Taifa. Ukweli ni kwamba, mgodi mpya wa Buhemba ulijengwa kwa Rand milioni 240 (dola 56m) na Kampuni ya WBHO (Pty) Ltd ya Afrika Kusini, na ulikamilika mwaka 2000. Ujenzi huo ulifanywa kwa niaba ya Meremeta na Triennex (kampuni zote tata), na si kwa niaba ya Serikali ya Tanzania. Ulizihusisha pia kampuni za Kigeni za Jefferies and Green na Time Mining, zote za Afrika Kusini.

Niharakishe kusema hapa kwamba, mmoja wa wanahisa wakubwa wa kampuni ya Time Mining ™, alikuwa Anna Muganda, mke wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Daudi Balali, ambaye ndiye pia aliyeileta kampuni hiyo nchini kuja kusimamia na kuendesha mgodi wa Meremeta, eti kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.

Cha kushangaza hapa pia ni kwamba, wengi wa watumishi wa nje (expatriates) wa kampuni ya Ukaguzi ya Alex Stewarts ya mjini Washington, iliyoletwa Tanzania na Daudi Balali kukagua mauzo ya nchi za nje ya dhahabu kwa makampuni ya madini nchini, ndio haohao waliokuwa watumishi pia wa kampuni ya Time Mining ya Anna Muganda.

Kama kweli serikali ilikuwa na maslahi katika Meremeta, kwa nini iliruhusu mtu binafsi (Anna Muganda) kusajili kampuni binafsi ya kigeni kusimamia mradi huu? Na Daudi Balali alikuwa na mamlaka gani kuajiri kampuni binafsi kukagua uzalishaji na uuzaji nchi za nje, madini ya nchi hii, na kwa manufaa ya nani?.
…..Itaendelea toleo lijalo…..

No comments:

Post a Comment