Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad. |
ALIYEKUWA mgombea urais wa Chama cha
Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, ndiye ambaye ataamua mwelekeo wa siasa za
Zanzibar katika kipindi cha muda mfupi na wa kati ingawa matatizo ya visiwa
hivyo yanatakiwa kwenda mbali zaidi ya mtu mmoja, Raia Mwema limebaini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Marudio, wakati wa uchaguzi wenyewe na baada ya uchaguzi huo uliofanyika Machi 20 mwaka huu, umebaini kwamba katika wakati huu, hakuna suluhisho linaloweza kupatikana pasipo Hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, kuhusishwa kwa namna yoyote.
Tayari CUF kimetangaza kutomtambua Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, katika taarifa ambayo ni wazi imeanza kuwakumbusha Wazanzibari katika nyakati za giza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 uliomwingiza madarakani Rais Amani Karume.
Hamad ambaye ni maarufu kwa jina la Maalim Seif mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 katika siasa za Tanzania ndiye mwanasiasa pekee visiwani Zanzibar anayekubalika katika pande zote mbili za visiwa hivyo; Unguja na Pemba na ushawishi umeonekana katika chaguzi zote za vyama vingi zilizofanyika Zanzibar tangu mwaka 1995.
“ Zanzibar kuna matatizo ya kisiasa lakini hayawezi kumalizwa bila ya kumshirikisha Maalim Seif. Mtu yeyote anayedhani kwamba anaweza kuleta mwafaka Zanzibar kwa kumtenga Maalim atakuwa anajidanganya tu.
Yeye ndiye pekee ambaye
anayekubalika Pemba na Unguja, alisema mzee Salim Rashid, Katibu Mkuu wa kwanza
wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar katika mazungumzo yale aliyoyafanya na Raia
Mwema mwezi uliopita nyumbani kwake Unguja.
Takwimu za chaguzi mbalimbali zilizokusanywa na Raia Mwema zinaonyesha kwamba tangu mwaka 1995, CCM imekuwa ikipunguza idadi ya viti vyake na kura katika ngome yake ya Unguja wakati CUF imekuwa ikijiimarisha zaidi visiwani Pemba. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Maalim alipata kura 163,706 na kura hizo ziliongezeka mwaka 2005 wakati alipopata kura 207,733.
Ingawa taarifa rasmi za matokeo ya uchaguzi uliofutwa wa Oktoba 25, 2015 hazijawekwa hadharani, CUF kinaamini kwamba kilipata viti vyote vya Baraza la Wawakilishi Pemba na walau viti vinane kisiwani Unguja ambako kwa muda mrefu ni ngome ya CCM.
Kihistoria, Pemba imekuwa ngome ya upinzani tangu wakati wa utawala wa Sultan na kilipokea vema vyama vya Zanzibar Nationalist (ZNP) na Zanzibar and Pemba Peoples (ZPPP). CCM ni zao la chama cha Afro Shiraz kilichoanzishwa Unguja ambako ndiko iliko ngome ya CCM.
Katika kitabu kinachoeleza maisha ya Maalim Seif na Ali Sultan Issa kiitwacho “Race, Revolution and the fights for Human Rights in Zanzibar”, Wapemba walipokea vema upinzani wakati huo kwa sababu ingawa Pemba ndiyo ilikuwa mzalishaji mkubwa wa zao kuu la kibiashara la Zanzibar, faida walikuwa wanapata watu wa Unguja.
Maridhiano
Jambo linalotakiwa Zanzibar katika kipindi kirefu ni maridhiano ya watu badala ya wanasiasa kutokana na historia ya miaka 50 iliyopita ya visiwa hivyo. Kwenye miaka ya kwanza iliyofuata mapinduzi ya Zanzibar, kuna familia ziliuliwa kikatili, watu kufilisiwa mali zao na mambo yasiyo ya kibinadamu yaliyowafanya watu wawe na kinyongo.
Baadhi ya wanasiasa na wasomi wa Zanzibar wanapendekeza kwamba Wazanzibari wanatakiwa wapate jukwaa la kuzungumza mambo yao na kusameheana kwa yaliyotokea baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ili kujenga jamii isiyo na kinyongo.
CHANZO: RAIA MWEMA.
No comments:
Post a Comment