Thursday, 21 April 2016

Rais Magufuli tumbua majipu lakini…(2)



Joseph Mihangwa
Joseph Mihangwa
Joseph Mihangwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiteta jambo na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa.

Na Joseph Mihangwa.
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya wiki iliyopita, tuliona namna kampuni tata ya Meremeta “ilivyoingia” nchini kwa ubunifu wa vigogo wa serikali na Benki Kuu na hatimaye kuchota kijanja mabilioni ya fedha na “kutoweka” kwa “kusindikizwa” na vigogo hao hao wa serikali.

Utata huo, kama tu ulivyokuwa utata wa kampuni ya Richmond iliyochota mabilioni ya fedha kwa mfumo unaofanana, ulitokana na madai ya kampuni hiyo kusajiliwa nchini Uingereza na madai mengine ya kusajiliwa nchini mwetu na kwa kisingizio cha kufanya kazi kwa mwavuli wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na hivyo kujengewa mazingira ya kuhitaji usiri wa kiusalama ili isiguswe kwa utapeli huo na hujuma kwa nchi.

Baada ya kukomba dhahabu yote huko Buhemba na Buhemba Kusini, Nyamongo na Magunga, mwaka 2006, Meremeta ilitangazwa kuwa ilikuwa inafanya kazi kwa hasara na ikaundwa tume ya serikali ya watu watano, kuchunguza matatizo ya kampuni hiyo.

Wazito na waheshimiwa waliokuwa katika Tume hiyo, ni Daudi Balali – Gavana wa BoT na Mwenyekiti wa Tume; Gray Mgonja, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, na Patrick Rutabanzibwa, wakati huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.

Wengine walikuwa ni Mabwana Vincent Mrisho, Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Andrew Chenge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Bwana Michael G. Garner, kama mshauri huru wa tume, ambaye alikuwa pia ndiye Mshauri wa Benki ya Nedbank, yenye uhusiano na kampuni ya Nedcor Trade Service, iliyochota bilioni 155/- kutoka Benki Kuu katika mazingira ya kutatanisha.

Tume hiyo ilipendekeza kusitishwa kwa shughuli za kampuni ya Meremeta za kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, jukumu ambalo tayari ilikwishalitelekeza tangu mwaka 2003, na kujiingiza katika uchimbaji na umiliki wa migodi.

Tume ilipendekeza pia kuanzishwa kwa kampuni mpya yenye jukumu la kusimamia na kuendesha Mgodi wa Buhemba yenye kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100. Kwa lugha nyingine ni kwamba, baada ya kung’atuka kwa Meremeta, serikali iliamua kusimamia yenyewe mradi huo wa dhahabu kupitia chombo au taasisi teule.

Na kwa uzito wa mapendekezo ya tume hiyo ya Balali, Meremeta ilifilisiwa, ambapo mali na madeni yake yalichukuliwa na kampuni mpya ya “Tangold,” inayodaiwa kumilikiwa na serikali kwa asilimia 100. Na ingawa Meremeta ([halisi) ilifungwa rasmi mwaka 2006 nchini Uingereza, shughuli zake hazikukoma nchini Tanzania wakati huo, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.

Hapa kuna utata mwingine, kwamba kumbukumbu zinaonesha kuwa kampuni ya Tangold ilianzishwa katika Visiwa vya Mauritius, Aprili 4, 2005; na kupewa Leseni ya Biashara Aprili 8, 2005 kama kampuni binafsi. Lakini kumbukumbu zingine zinaonesha kuwa, Tangold ilifungua Akaunti ya Benki Namba 011103024852, Tawi la Corporate Drive la NBC, Dar es Salaam, Januari 1, 2003; kabla hata Tume ya Balali na wenzake haijaundwa kutatua tatizo la Meremeta.

Taarifa zingine zimeonesha zaidi kuwa kampuni hiyo ni ya kigeni iliyosajiliwa nchini Mauritius na kupewa leseni nchini Tanzania, Februari 20, 2005 kama Tawi la Kampuni ya kigeni; na ilianza kupatiwa fedha na BoT Agosti 1, 2005 kwa kazi isiyojulikana.

Je, ina maana kwamba Tangold ilikuwapo nchini Tanzania kabla ya kuanzishwa nchini Mauritius mwaka 2005, au ni aina fulani tu ya usanii? Hata kama ilikuwapo, iliwezaje kufungua akaunti benki, Januari 1, 2003 ambayo ilikuwa Sikukuu ya Kitaifa ya Mwaka mpya?

Kama ilikuwapo, kwa nini tume ilipendekeza kuundwa kwa kampuni ambayo tayari ilikuwapo? Nini tofauti kati ya Tangold iliyofungua akaunti Januari 2003, na Tangold iliyosajiliwa Mauritius April 4, 2005 kurithi Meremeta?

Ingawa mapendekezo ya tume na tamko la serikali yalikuwa kwamba kampuni hiyo mpya (Tangold) imilikiwe kwa asilimia 100 na serikali, utekelezaji wake ulikuwa ni kinyume chake; ambapo inaelekea wajumbe wa tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya Meremeta, ndio waliogeuzwa kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo mpya.

Hao wanatajwa (kwa baadhi majina yao kuongezwa herufi moja ya katikati), kuwa ni Daudi Balali, Gray S. Mgonja, Andrew Chenge, Patrick J. W. Rutabanzibwa na Vicent F. Mrisho.

Inawezekana, kwa mtazamo wa enzi hizo na kwa kusudi hilo, kwamba hao watano ndio walikuwa serikali yenyewe; lakini kifungu cha saba (7) cha Katiba ya Kampuni ya Tangold kinatibua dhana yote hiyo, kinaposema, “Wenye hisa ya kampuni wanaweza kurithisha hisa zao kwa ndugu zao”.

Je, ni kweli Tangold ilikuwa inamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 kama ilivyopendekeza Tume ya Balali na pia kwa mujibu wa tamko la serikali? Ni ndugu wapi hao wa serikali (kama kweli serikali ina ndugu!) waliostahili kurithishwa hisa za serikali?.

Haya ni maswali magumu, na tunashawishika kuamini kwamba, Tangold haikumilikiwa na serikali kwa asilimia 100 kama tulivyoambiwa bali ilikuwa kampuni binafsi iliyorithishwa mali za Kampuni ya Meremeta.

Wakati matatizo ya Meremeta yakiendelea na wakati huohuo tayari mapendekezo ya Tume ya Balali ya watu watano yakiwa yameanza kufanyiwa kazi, Machi 18, 2004, iliundwa kampuni nyingine iitwayo “Deep Green Finance” (DGF) ambayo madhumuni na shughuli zake hazijafahamika vizuri mpaka sasa.
Wakurugenzi wa DGF walikuwa ni Mark Ross Weston wa New Zealand; Antón Taljaard wa Afrika Kusini, na Rudolf Van Schalkwyk, pia wa Afrika Kusini.

Wanahisa wa DGF walitajwa kuwa ni Protase R. G. Ishengoma, Stella Ndikimi wa Kampuni ya uwakili ya IMMA, ya jijini Dar es Salaam; Benki ya Nedbank Africa Investment Ltd ya Afrika Kusini (ambayo Mshauri wake, Bwana Michael G. Garner, ndiye pia aliyekuwa mshauri huru wa Tume ya watu watano, iliyochunguza matatizo ya Meremeta na kupendekeza kuundwa kwa Tangold), na kampuni ya SBM Nedcor Holdings, ambayo haijafahamika bado, kama ina uhusiano wowote na kampuni ya Nedcor Trade Service, iliyolipwa na BoT malipo tata ya zaidi ya Sh. 155bn/= kwa niaba ya Meremeta.

Wakurugenzi hao watatu wa Deep Green Finance, pia ndio waliokuwa maafisa wa NedBank; na jina la Deep Green limetumiwa mara nyingi na NedBank katika miradi yake ya kijamii.

Haifahamiki pia ni kwa vipi na kwa njia ipi, Watanzania pekee wawili, Protase Ishengoma na Stella Ndikimi, walitembelewa na ngekewa ya kununua hisa za kampuni yenye kumilikiwa na wageni kama hii (DGF); na kama ni kweli inavyodaiwa, kwamba hatimaye walichukua hisa (kwa njia ya kuhamishia au kununua) katika Nedbank Ltd na Nedbank Africa Investments, Aprili 15, 2004.

Kama ilivyokuwa kwa kampuni ya Tangold, iliyofungua akaunti siku ya sikukuu ya mwaka mpya; ndivyo ilivyokuwa pia kwa kampuni ya Deep Green Finance, iliyofungua akaunti Benki ya NBC, Na. 011103024840, Tawi hilo hilo la Corporate Drive; safari hii ilikuwa sikukuu (ya mapunziko) ya Mei Mosi, 2004.

Kuna utata kuhusu utoaji wa namba za akaunti za benki hiyo, kwamba akaunti ya Tangold, Namba 011103024852, iliyofunguliwa Januari 1, 2003, ni kubwa (kwa akaunti 12 zaidi), ikilinganishwa na akaunti Namba 01110302840 ya Deep Green Finance, iliyofunguliwa zaidi ya mwaka mmoja baadaye, Mei 1, 2004.

Je, ni utaratibu wa NBC kutoa namba za akaunti kuanzia na namba za juu, kushuka chini? Kama sivyo, basi kuna uwalakini unaotufanya tuamini kwamba kulikuwa na mchezo mchafu, ikizingatiwa pia kwamba akaunti zote mbili zilifunguliwa siku za mapumziko ya Sikukuu za Kitaifa.

Toka Mei 1, 2004 akaunti ya Tangold ilipofunguliwa, hadi Julai 31, 2005 (zaidi ya mwaka mmoja), hapakuwa na shughuli za DGF zilizoingiza fedha katika akaunti hiyo, hadi Agosti 1, 2005 ilipoanza kupokea mabilioni ya fedha kutoka ama benki Kuu, Deep Green Finance au Tangold, kwenda ama Deep Green Finance, Tangold, Meremeta, IMMA Advocates au kusikojulikana.

Wakati tunaelezwa kwamba Tangold ilianzishwa April 5, 2005 na kupewa leseni ya biashara April 8, 2005 kuchukua nafasi ya Meremeta, na mali na madeni ya Meremeta kuhamishiwa au kuchukuliwa na kampuni mpya, kwa maana kwamba Meremeta ilikuwa imefilisiwa na kufungwa.

Lakini kumbukumbu zinaonesha kwamba, Oktoba 12, 2005, jumla ya Shs. 1,690,500,000 zilihamishwa kutoka Tangold kwenda kampuni (mfu?) ya Meremeta; na vivyo hivyo Novemba 23, (Tshs. 555,300,048/=) na Desemba 12 kiasi cha Shs. 551,060,000. Iliwezekanaje Meremeta kulipwa fedha hizo wakati ilikwishafilisiwa? Nani aliifufua?

Kwa kifupi, kati ya Agosti 1, 2005 na Desemba 21, 2006, jumla ya Sh. 32bn/= zilihamishwa kutoka Benki Kuu kwenda Deep Green Finance na Tangold; mbali na zile zilizopelekwa kusikojulikana.

Tunashawishika kuamini kwamba Deep Green Finance iliundwa kurahisisha na kuhakikisha utoroshaji wa fedha za Meremeta na Tangold kwenda nje ya nchi na si kwa sababu nyingine yoyote ile.

Baada ya purukushani hizo, na kuonekana kwamba mradi wa Tangold hauwezi kuendelea, serikali iliuza haki za mgodi huo kwa kampuni ya “Rand Gold” ya Afrika Kusini, kwa bei ya chini ya soko, na kusababisha hasara ya dola za Kimarekani milioni 100; na pia kulipa dola miliono 132 pamoja na adhabu na riba, kutokana na Serikali (BOT) kudhamini wakopaji/wawekezaji waliofilisika na kutupa mzigo kwa serikali kuyalipa.

Purukushani hii, toka kuundwa kwa kampuni ya Meremeta, hadi kuundwa na kufilisika kwa kampuni ya Tangold, licha ya kuruhusu uporaji mkubwa wa mabilioni ya fedha na rasilimali zetu, ilisababisha pia hasara ya jumla ya dola za Kimarekani milioni 232, sawa na Shs. 232bn/= wakati huo, kwa njia ya kifisadi.
Serikali ya Awamu ya Tatu, ya Rais Mkapa ilifanya malipo hayo Oktoba 2005, mwezi mmoja tu kabla ya kumaliza muda wake wa kuwa madarakani.

Na ndivyo hivyo awamu hiyo ya tatu ilivyolipa pia kwa malipo tata ya kashfa ya EPA, 133bn/= mwishoni mwa Oktoba 2010. Na vivyo hivyo Serikali ya awamu ya nne ilivyolipa malipo tata ya 326bn/= kutoka akaunti ua “Tegeta Escrow” kwa kuporwa na Kampuni ya PAP, miezi kadhaa kabla ya kumaliza kipindi chake.

Utamaduni huu wa kupora dakika za mwisho kwa watawala utadumu hadi lini?.

No comments:

Post a Comment