Mwanafunzi akionyesha tundu la risasi kwenye dirisha la Chuo Kikuu cha Garissa. |
Mamia walikusanyika katika eneo la shambulio hilo mashariki ya Kenya kukumbuka mkasa huo ambalo ni shambulio baya kabisa la kigaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo likitekelezwa na wapiganaji wanne wa kundi la Al Shabab la Somalia lenye mafungamano na kundi la Al Qaeda.
Wapiganaji hao hatimae waliuwawa na kikosi cha makomandoo wa Kenya baada ya saa 12 na serikali ilikosolewa vikali kwa kuchelewa kuchukuwa hatua ya kukabiliana na shambulio hilo licha ya kuwepo kwa kambi ya kijeshi karibu na eneo hilo la tukio.
Kenya imekabiliwa na wimbi la mashambulio ya wapiganaji wa itikadi kali tokea ilipotuma wanajeshi wake nchini Somalia hapo mwezi wa Oktoba mwaka 2011 kuisaidia serikali dhaifu ya nchi hiyo katika mapambano yake na wanamgambo wa Al Shabab.
Chuo kikuu hicho kilifunguliwa tena hapo mwezi wa Januari baada ya ukarabati mkubwa wa majengo yaliojaa tundu za risasi lakini ni wanafunzi 150 tu kati ya 700 waliorejea madarasani.Wengine wamehamishiwa katika Chuo kikuu cha Moi magharibi mwa Kenya.
Kenya kutoondowa vikosi Somalia
Aden Duale mbunge wa Garissa amesema katika kumbukumbu hiyo kwamba vikosi vya Kenya vitaendelea kubakia nchini Somalia hadi hapo jukumu la kuleta utulivu katika nchi hiyo litakapotimilizwa.
Hata hivyo wazungumzaji wengine katika kumbukumbu hiyo wamesema familia za wahanga zinapaswa kulipwa fidia.Mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Garissa Shukran Gure amesema "Wakati umefika kwa serikali kuwafidia wanafunzi waliouwawa katika shambulio hilo.Huo ni wajibu wa serikali."
Paul Wekesa mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni mwanafunzi wa masomo ya elimu wa mwaka wa pili ambaye alishuhudia shambulio hilo anakubali kwamba serikali inapaswa kutowa fidia ya aina fulani kwa familia za wanafunzi waliopoteza maisha na msaada wa masomo kwa wale walionusurika.
Amesema yeye mwenyewe aliweza tu kunusurika kwa sababu alikuwa ameamka na mapema ili kusoma na alikuwa macho wakati shambulio hilo likianza. Akiwa pamoja na kundi jengine la wanafunzi alikwenda kuchunguza sauti za risasi ambapo walikuja kukutana na mtu mwenye bunduki aliyewafaytulia risasi.
Mwanafunzi mmoja alikufa papo hapo na wengine walikimbia kwa kuukwea uzio wa senye'nge huku risasi zikiwaandama.
Masuali mengi yanahitaji majibu
Kwa mujibu wa mchambuzi wa kisiasa Patrick Gathara kwa umma kuna masuali mengi yanayohitaji majibu kuhusu serikali kuchelewa kuchukuwa hatua,kushindwa kuzuwiya shambulio hilo licha ya kuwepo kwa tahadhari za kijasusi na ukweli kwamba hakuna mtu aliyefunguliwa mashtaka kwa uzembe wa usalama.
Amesema Kenya ni nchi ilioko hatarini.Watu hawaamini kwamba kimsingi wako salama licha ya kile inachosema serikali. Ameongeza kusema kwamba "hakuna ushahidi serikali imejifunza kutokana na makosa yake."
Ukiwa ni mwaka mmoja tokea shambulio hilo vyuo vikuuu vya Kenya vimekuwa katika hofu ambapo mara nne kumetokea mikanyangano katika taasisi mbali mbali baada ya wanafunzi kudhania kwamba wamesikia milio ya risasi au mabomu ambapo mamia walijeruhiwa na wawili kupoteza maisha yao.
CHANZO: DW
No comments:
Post a Comment