Friday, 8 April 2016

Aliyoniambia Mwalimu kuhusu Maalim


Maalim Seif Sahrif Hamad (wa nne kulia) akiwa katika moja ya vikao pamoja na Mwalimu Nyerere mwaka 1984.

Na Ahmed Rajab.

KAMA ilivyo kwa Julius Kambarage Nyerere ndivyo ilivyo kwa Seif Sharif Hamad. Wote ni maarufu kimataifa kwa jina moja tu. Mmoja Mwalimu, mwengine Maalim.Majina mawili yenye maana moja. Majina hayo hutamkwa tofauti kutegemea mtu yuko wapi na amekulia katika mazingira gani.

Wote wawili, Mwalimu na Maalim,walikuwa na kazi ya ualimu kabla hawajawa wanasiasa waliobobea.

Nilianza kumjuwa Maalim kabla hajawa mwalimu tulipokuwa wanafunzi katika skuli ya King George VI Memorial Grammar Secondary School, (siku hizi Skuli ya Sekondari ya Lumumba) iliyoko Saateni, Unguja.Alikuwa mbele yangu kwa miaka miwili.

Hakuwa mzungumzaji sana. Kwa hakika, hakuwa akichanganyika sana na wanafunzi wengine. Miaka hiyo nikimuona tu skuli, akiwa mmoja wa wanafunzi kutoka Pemba waliokuwa wakiishi katika bweni ya Beit el Ras, nje kidogo ya mji.Wakiletwa skuli kila asubuhi na kurejeshwa mchana kwa magari ya bweni.

Seif wa siku hizo alikuwa mrefu, mwembamba, aliyepinda kidogo na aliyekuwa akivaa sare ya skuli, shati jeupe na suruali ya khaki.

Mara nyingine akija skuli akiwa amepiga kanzu na kofia. Mwalimu Mkuu wa skuli,G.G.Davies, akiruhusu kanzu na kofia kuwa ni sare mbadala.

Nadhani sikio moja la Seif likimpa taabu kwani alikuwa heshi kutia pamba sikioni. Jengine ninalolikumbuka ni kwamba alikuwa akitafakari sana.

Daima uso wake ulikuwa chini akiwa mwenye mawazo. Akifikiri nini? Sijui. Na alikuwa na macho, ambayo Waingereza wangeliyaita “meditative eyes”, yaani macho ya tafakuri au ya mazingatio.

Waliosoma naye darasa moja wanasema Seif hakuwa mtu wa maneno mengi, wa mizaha isiyo na maana. Alikuwa mtulivu, mpole na mkimya. Wanasema ilikuwa taabu kuzijuwa fikira zake kwa vile alikuwa si mbobokaji.

Akipendelea kuchunguza mambo tu na kuwasikiliza wengine kwa makini. Hata katika mijadala ya skuli alikuwa si mtetezi ingawa alikuwa hakosi kuhudhuria mijadala hiyo.

Seif alionyesha mapema dalili za uongozi. Alipokuwa darasa la kumi alikuwa kepteni wa bweni lao akiwasimamia hata wakubwa zake kwa umri.

Kwenye bweni lao akijulikana kwa kupenda kusoma. Baada ya saa nne za usiku jenereta lilipokuwa linazimwa, Seif alikuwa akiwasha taa ya kandili au karabai na akiendelea kusoma. Nadhani hiyo ndiyo sababu iliyomfanya baadhi ya wakati aonekane kama mtu aliyekosa usingizi.

Alipoingia Kidato cha Tano alikuwa ama kiranja au naibu wa kiranja wa skuli.
Tangu enzi hizo vijana wa Kipemba walikuwa wakinung’unika kwa namna kisiwa chao kilivyokuwa kikionewa na watawala licha ya kwamba Zanzibari kipata sehemu kubwa ya mapato yake kutoka mauzo ya karafuu za Pemba na, kwa hivyo, kisiwa cha Unguja kikinufaika zaidi.

Kulikuwa na jengine lililokuwa likiwaudhi: sisi wa Unguja tukipenda kuwafanyia stihizai.
Tukiwatumbukiza katika kapu moja na tukiwafanyia tashititi na kuwacheka, kwa mfano, kwa lafudhi zao au kwamba eti wakipenda sana vitu vitamu kiasi cha kuwafanya wawe wanakula haluwa kwa chai ya maziwa.

Nadhani idhilali hizo ndizo zilizozidi kuwafanya wawe kitu kimoja na zilizowafanya waamue kuwa na chama chao cha wanafunzi wazawa wa Pemba.

Badala ya kujiunga na All Zanzibar Students’ Union (AZSU), chama cha wanafunzi wa Zanzibar nzima, wao waliunda chama walichokiita rasmi Pemba Students’ Union(PSU, Chama cha Wanafunzi wa Pemba). Wengine wakikiita Pemba-Born Students’ Union, yaani Chama cha Wanafunzi Waliozaliwa Pemba.

Chama cha PSU kilikuwa na kamati ya watu watano na Seif ndiye aliyekuwa kiongozi wao.
Wanafunzi hao wa Kipemba wakishikamana bila ya kujali vyama vyao vya siasa.Seif alikuwa mfuasi waAfro-Shirazi Party (ASP).Mwanafunzi mwengine wa Kipemba, Enosh Timothy Bilal, niliyekuwa nikikaa naye deski moja skuli na aliyekuwa akiishi Beit el Ras,naye pia alikuwa mfuasi mkubwa wa ASP.

Nakumbuka kuna wakati vijana hawa kutoka Pemba walianzisha vuguvugu lao lisilo rasmi waliloliita “Pemba Yekka”. Waliliigiza jina la chama cha Kabaka Yekka cha Uganda, chama ambacho kilikuwa kikimuunga mkono Kabaka Mutesa, mfalme wa Wabaganda.

Kwa lugha ya Kiganda “yekka” maana yake ni “tu”, kwa hivyo “Kabaka Yekka” ilikuwa na maana ya “Kabaka Tu”.

Wabaganda wakiyatumia matamshi hayo kusalimiana. Mmoja akisema “Kabaka”, mwengine akiitika “Yekka” na halafu kila mmojawao akionyesha juu kidole chake cha shahada.

Wafuasi waPemba Yekka hawakuwa wakisalimiana kwa kaulimbiu hiyo iliyokuwa na maana ya “Pemba Tu”.

Nilipoondoka Zanzibar 1964 kwenda Uingereza kwa masomo, Seif alikuwa ameshahitimu Kidato cha Sita na alilazimishwa kusomesha skuli za sekondari. Kwanza aliajiriwa Lumumba alikosomesha Kiingereza, Fasihi na Historia.

Nasikia Maalim Seif alikuwa mwalimu mzuri. Aliendelea kusomesha hadi 1972, pale serikali ya Rais Aboud Jumbe ilipompatia nafasi ya kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikohitimu na kutunukiwa shahada ya B.A.(Hons) miaka mitatu baadaye.

Tangu 1964 sikumshuhudia tena Seif hadi mwezi wa mfungo wa Ramadhani katika miaka ya kati ya 1970 nilipokutana naye Mombasa. Ilisadifu kwamba akija kufuturu Mji wa Kale katika nyumba niliyoshukia ya Maalim Saleh Abdallah Jahadhmy “mwandani”, mwalimu wetu wa zamani aliyekuwa na asili ya Lamu.

Tulikuwa tukifuturu watu wanne; mwengine akiwa kijana wa Kikenya. Wakati wa futari, Maalim Jahadhmy alikuwa akiulizauliza habari za siasa. Wakati wote,kama kawaida yake, Seif alikuwa akisikiliza tu. Hakujifanya mjuaji ingawa nina hakika akiyajuwa mengi.Mimi ndiye niliyejidai kujuwa na nikimjibu Jahadhmy.

Maalim aliweza kuchupa na kutua kwenye medani ya siasa za kitaifa alipoteuliwa na Jumbe awe waziri wa elimu wa Zanzibar 1977.

Jumbe, mwalimu wetu wa zamani katika skuli ya King George, akimpenda Maalim na alimsaidia kwa kumpa fursa ya kusoma masomo ya juu na kwa kumuingiza katika siasa za kitaifa. Unaweza kusema kwamba ndiye aliyemjenga.

Mwalimu Nyerere, ambaye mwanzoni akimpenda Maalim, akijigamba kwamba ni yeye aliyemjenga.

Niliwahi kuandika katika ukurasa huu nilipomkuta Mwalimu akibugia njugu na bia chumbani kwake katika hoteli ya Intercontinental jijini Nairobi kabla ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake wa urais katika uchaguzi wa 1995. Mwalimu aliniuliza watu wakisemaje kuhusu mchuano huo.

Nikamjibu: “Wanasema una mtu wako.”
“Nani?”
“Salim (Salim Ahmed Salim)”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu mtoto wako.”

Kumwambia hivyo aliruka na akanambia kwa mkazo: “Lakini wote watoto wangu. Kwani hata Seif, nani unadhani kamjenga?”

Nikamwambia: “Wewe” kwa sababu nikijuwa kwamba ndivyo alivyotaka nimwambie.
“Tena!” Mwalimu alisema kwa hamasa na kana kwamba akijipongeza akiwa anapiga soga barazani na vijana wa mjini.

Ilikuwa wazi alipoyasema hayo kwamba aliona fahari kubwa kujihusisha na Maalim kwani aliutambua uwezo wake, kipaji chake na utendajikazi wake.

Ndio maana alimkabidhi nyadhifa kubwa kubwa ndani ya CCM. Hata wakati wa sokomoko la kisiasa Zanzibar katika enzi ya Rais mstaafu Salmin Amour, Nyerere aliwahi kutamka kwamba ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar lazima umhusishe Maalim.

Na kuna ule mkutano wa siri Butiama ambao mpaka leo hatujui kilipita nini baina ya Maalim na Mwalimu.
Tunachokijuwa ni kwamba Maalim hakuzuzuka kwa kupendwa na Mwalimu. Alithubutu kusimama imara akitetea msimamo wake kuhusu Zanzibar, hatua ambayo ilisababisha akamatwe na kuwekwa ndani gerezani.

Katika ushirikiano wa Maalim na Mwalimu kuna kadhia moja iliyomtia doa Maalim, doa litalomganda maisha. Hii ni kadhia ya jinsi Mwalimu na CCM walivyompindua Jumbe.

Kuna wanaomtuhumu Maalim kwamba alimwendea kinyume Jumbe na kumfanyia hiyana. Juu ya hayo, tusisahau tu kwamba historia ina mifano mingi ya watu waliowahini wenzao kwa malengo adhimu.

Maalim amejaribu sana kujitetea lakini utetezi wake bado haukuwaridhisha wanaomtuhumu.
Kwa upande mwingine, msimamo wa Maalim kuhusu suala la usawa wa Tanganyika na Zanzibar ulimfanya awe mwiba uliokuwa ukimchoma Mwalimu. Aliushikilia msimamo huo hata alipokuwa waziri kiongozi wa Zanzibar (1984-1988). Mwishowe Mwalimu alibidi ampikie jungu la kumfukuzisha kutoka CCM.

Moja ya sababu zilizomfukuzisha Maalim kutoka CCM ni idadi ndogo sana ya kura alizopata Rais Idrissa Abdul Wakil huko Pemba katika uchaguzi wa chama kimoja uliofanywa 1985.
Lawama ilimwangukia Maalim kuwa eti alimtilia fitna Abdul Wakil Pemba na ndio maana huko aliondokea patupu.

Baada ya kufukuzwa CCM na kabla ya vyama vya siasa kuhalalishwa nchini 1992, Maalim Seif alikuwa akiliongoza vuguvugu la KAMAHURU pamoja na akina Shaaban Mloo, Maulidi Makame, Ali Haji Pandu na Hamad Rashid.

Kilikuwa kipindi kigumu kwake. Wakati huo katika miaka ya 1980 tayari kulikuwako na vuguvugu la Wazanzibari nje ya nchi lililoasisiwakwenye mkutano uliofanywa mjini Malmo, Sweden, chini ya uenyekiti wa Abdulrahman Babu, aliyekuwa kiongozi wa chama cha zamani cha Umma Party.

Vuguvugu hilo likiitwa Harakati za Kuleta Mabadiliko ya Kidemokrasia (kwa ufupi HAMAKI na kwa Kiingereza likiitwa Zanzibar Democratic Alternative).

Waliokuwa kwenye vuguvugu hilo walikuwa Wazanzibari wa itikadi tofauti za kisiasa.Miongoni mwao alikuwa Dk. Yusuf Saleh Salim aliyekuwa na mahusiano mazuri na viongozi wa KAMAHURU.

Alipokuwa akiongoza KAMAHURU ndipo ukomavu wa kisiasa wa Maalim ulipoanza kudhihirika na dunia ilipoanza kutambua kwamba Zanzibar ina kiongozi wa kipaji cha juu.

Naweza kusema kwamba miongoni mwa magwiji wa kisiasa waliovutiwa naye alikuwa Babu.
Watu wawili hao walikuwa na itikadi tofauti lakini kwa maslahi ya Zanzibar fikira zao zilioana.

Ninayajuwa hayo kwa sababu mimi ndiye niliyewakutanisha ana kwa ana kwa mara ya kwanza.
Ilikuwa 1988 nilipowaalika kwa chakula cha usiku nyumbani kwangu, siku hizo nikiwa katika mtaa wa Stoke Newington, London.

Babu baadaye alijiunga na NCCR-Mageuzi lakini akitambua kwamba kiongozi atayeweza kuleta mageuzi ya kimaendeleo Zanzibar ni Maalim. Alikuwa na sababu zilizomfanya ajiunge na NCCR-Mageuzi lakini hazikuwa za kutokuwa na imani na Maalim.

Maalim Seif hajakamilika na wala hawezi kukamilika kwani ni mwanadamu.Hata hivyo,ninaamini ukiwachukuwa wanasiasa wote wa Zanzibar ya leo ukawaweka kwenye mezani uwapime kwa vigezo vyote vya umahiri wa kisiasa, Maalimatawapiku wenzake.

Yeye pamoja na Rais Mstaafu Dk. Amani Karume ni viongozi wenye sifa tofauti, kwa mfano, na zile walizokuwa nazoakina Sheikh Ali Muhsin Barwani (aliyekuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party au Hizbu) na Sheikh Abeid Amani Karume (aliyekuwa kiongozi wa ASP). Hao walikuwa viongozi wa kihistoria.

Watu wengi husahau kwamba kwa upande wa Sheikh Ali jambo la mwanzo alilolifanya baada ya kuingia siasa ni kujiuzulu kutoka Jumuiya ya Waarabu akiuweka mbele Uzanzibari wake.
Sheikh Karume, kwa upande wake, akionekana na wengi wa Wazanzibari waliokuwa wakijifaharisha na “Uafrika” kuwa ni mkombozi wao.

Babu, niliyekuwa mimi nikimfuata, kidogo ananipa taabu. Ninaweza nikamuweka katika shubaka la viongozi wa kihistoria lakini nadhani nitakuwa sahihi zaidi nikimpachikakwenye shubaka la peke yakeakiwa mkunga wa historia.

Hawa viongozi wa leo, Maalim Seif na Dk. Karume, wamethibitisha kwamba wao ni viongozi wenye ujasiri na bisara (vision) kubwa. Tunaweza kuyamithilisha Maridhiano yao ya 2010 kuwa, kwa kiwango fulani, kama yale ya Afrika ya Kusini.

Amani Karume alikuwa kamaFW de Klerk kwa kuwa na ujasiri wa kuwashawishi wenzake wafuate mkondo wa kihistoria baada ya kutanabahi kwamba Zanzibar imekuwa ikielekea pabaya na watu wake wamechoka na uhasama.

Maalim, kiongozi aliyekuwa upande wa haki na aliyedhulumiwa, amekuwa kama Nelson Mandela.Kwa bahati mbaya, Maalim hadi leobado anadhulumiwa. Ni dalili ya ujasiri wake kuwa ameweza kuwafanya wafuasi wake wawe watulivu na wayakubali Maridhiano.

Wa mwanzo kumbandika Maalim sifa ya “Umandela” walikuwa wafungwa aliowakuta gerezani Unguja alipokuwa katiwa ndani kuanzia Mei 11, 1989.Julai na Septemba 6 ya mwaka huo aliniandikia barua mbili akiwa jela akinieleza maisha yake yalivyokuwa huko kifungoni.

Miezi sita baadaye aliniletea waraka alioandika wenye kurasa 32 akizichambua siasa za kimataifa, za barani Afrika na za Tanzania. 
CHANZO: RAIA MWEMA.

No comments:

Post a Comment