Friday, 15 April 2016

Maalim Seif alipogeuka kuwa nguvu ya umma


Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.

Na Ahmed Rajab.
“NIMEPATA habari kuwa huenda kesho ukaondoka na ungependa upate mambo ya huku.”
Hayo “ya huku” ni ya huko alikokuwako Maalim Seif Sharif Hamad aliyeniandikia barua aliyoianza kwa maneno hayo Septemba 6, 1989. Ilikuwa siku moja kabla ya mimi kurudi Uingereza kutoka Zanzibar nilikokwenda kwa mapumziko.

Sijui ni nani aliyemjuza kuhusu mipango ya safari yangu na wala sijui mtandao wake wa mawasiliano ukifanya kazi vipi. Ninachojua ni kwamba nilipokuwa nimekwishakaa kitini ndani ndege alinipita mwanamke mmoja akadondosha bundi la karatasi mapajani mwangu.

Huko alikokuwako ni jela ya Kiinua Miguu, Unguja. Mtu asiye na insafu na uadilifu angeweza sana kutia chumvi kuhusu hali iliyomkuta ndani. Angeweza kutoa sura mbaya ya hali ya mambo ilivyokuwa ili awapake tope waliomfunga. Angeweza bila ya taabu kuupindua ukweli juu chini. Lakini hivyo sivyo alivyokuwa Maalim, na sivyo alivyo hadi leo. Ibara ya pili ya barua yake ilibainisha na kujumlisha hisia zake zilivyokuwa na mambo yaliyomkuta.

“Ukweli huku hakuna mengi. Mimi ni mzima. Sina wasiwasi wala hofu wala kinyongo. Mambo yanakwenda vizuri,” aliandika. Si ajabu kwa mfungwa, hususan wa kisiasa, kutokuwa na wasiwasi au hofu. Aghalabu huwa hivyo kwa sababu ya imani zao za kisiasa, za kuamini kwamba wako upande wa haki na haki iko pamoja nao na kwamba wana umati unaowaunga mkono. Ujasiri wao hutokea hapo, kwenye nguvu za umma.

Na hutokea hao wenye kutegemea nguvu za umma, wao wenyewe hugeuka na kuwa ndio nguvu ya umma. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Maalim. Baada ya kuushawishi umma uzikubali hoja zake, umma ulimuunga mkono na akawa anazitegemea nguvu za umma.

Miaka ilipokuwa ikikatika Maalim aligeuka na kuwa nguvu ya umma, tumaini na tegemeo lao.
Lenye kushangaza ni kumuona mfungwa anayeamini kwamba kafungwa kwa kuonewa asiwawekee kinyongo waliomfunga. Kutokuwa na kinyongo ni sifa adhimu mtu kuwa nayo, hususan ikiwa mtu huyo ni kiongozi tena kiongozi mwenye umati wenye kumfuata katika jamii iliyojaa udhalimu. Mtu wa aina hiyo ni mtu wa aina yake. Huwa si mtu tu bali huwa ni mtu aliyejaa utu.

“Huku ndani sina dhiki yoyote. Wakuu wa Jela wananiheshimu sana. Jela ndio Jela tu lakini they are trying their best to treat me in the best possible way (wanajaribu wawezavyo kunitendea vyema)”.

Ni nadra kwa mfungwa kuwa mkarimu hivyo kwa waliomfunga na waliomnyima uhuru wake. Angeliupinda ukweli akaniandikia kuhusu “maovu” asiyoyakuta huko jela, na angejifanya kuwa ameyakuta, basi ningelimuamini hasa kwa vile jela yenyewe alikokuwemo ilikuwa ya Kiinua Miguu.

Hiyo si jela yenye historia nzuri. Kuna kipindi fulani baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 hadi miezi ya mwanzo ya awamu ya pili chini ya Rais Aboud Jumbe, ambapo jela hiyo ilikuwa mithili ya Jahannam, sema ilikuwapo duniani tu.

Unyama usiosemeka ukitendeka humo. Wafungwa wakiteswa kila aina ya mateso. Wakitandikwa mikwaju, wakitundikwa kichwa juu miguu chini, wakitiliwa chatu ndani ya vyumba vyao na wengine wakilawitiwa kwa nguvu. Yote hayo na mengineyo yakifanyika nyuma ya gereza hilo, kule kunakoitwa “Kwa Ba Mkwe”.

Mateso ya huko yanafanana na tunayosikia kuwa yaliwakuta wafungwa wa kisiasa katika magereza mingine duniani kama kwa mfano jela ya Black Beach, mjini Malabo, Equatorial Guinea, Jela ya Diyarbakir ya Uturuki, Jela ya Kijeshi ya Tadmor huko Syria au kwenye ile iitwayo Kambi ya 22 ya Hoeryong, nchini Korea ya Kaskazini

Wengi wa wafungwa walijikuta katika jela ya Kiinua Miguu kwa sababu za kisiasa au, zaidi, kwa visingizio vya kisiasa.

Katika barua yake Maalim aliendelea kunieleza jinsi alivyowekwa katika jumba la vyumba vitano, akiwa pamoja na watoto wawili na “trustee” (mdhamini) mmoja.

“Kila kitu kinaletwa mumu humu. Maji ya kutumia naletewa na wafungwa ambao hugombania kupata fursa ya kuleta maji ili angalau wapate kusema nami.”

Na si wafungwa tu waliokuwa wakimuangalia Maalim kwa jicho la rehema. Askari nao, kwa jumla, wakimheshimu na wakimuonea huruma.

“Hata wale ambao mwanzo walionesha kufurahi kwa mimi kuja huku sasa ndio wanaoniombea dua. Wafungwa nao dua zao nikuwa nitoke tu.”
Hao ndio wale wafungwa ambao wiki iliyopita niliandika kwamba walimbatiza jina la “Mandela”. Tayari alikuwa na jina jengine la kubatizwa: “Simba wa Nyika”.

“Pamoja na yote hayo, nadhani wakuu wa jela wamepata agizo kutoka Polisi na Usalama kuwa wasiniruhusu kuongea na watu wengi. Hivyo, wamewekwa askari wane ambao ni Usalama lakini askari magereza kunishughulikia mimi tu. Mimi binafsi hawajanambia nisizungumze na mtu. Lakini wafungwa wa Rumande wamekatazwa na hata wengine kupigwa fimbo kwa kusema nami!”

Hao askari wanne ndio waliokuwa wakiruhusiwa kuzungumza naye pamoja na hao watoto aliokuwa akiishi nao na yule mdhamini wao.

Na ni askari hao waliokuwa wakimpelekea chakula, nguo, magazeti na kuzikidhi haja zake. Pia kila asubuhi daktari wa jela akimtembelea kujua hali ya afya yake.

Kwa hivyo, kama alivyoandika mwenyewe, “mambo si mabaya.” Jambo lililokuwa likimpa moyo zaidi ni kuwa akielezwa yote muhimu yaliyokuwa yakitokea. Ile azma ya viongozi ya kumtenga na watu pamoja na matukio haikufanikiwa. Njia zake za mawasiliano zikifanya kazi vizuri sana. Huo pekee ulikuwa ushahidi wa jinsi alivyokuwa akiungwa mkono.

“Kwa jumla, naridhika na harakati zinazoendelezwa na wenzangu. Kutokana na ninayoyapata my morale is always high.”

Baada ya kunitaka niwape salaam zake watu fulani akiwemo Abdulrahman Babu, Maalim alimaliza barua yake kwa kuandika:

“Hatuna shaka ushindi utapatikana tu. Nakutakia safari njema.”
Maalim aliiandika barua hiyo ikiwa takriban miezi minne tangu afungwe Kiinua Miguu. Hakuwa huko kwa kosa la jinai. Hakumpiga mtu, hakuiba hata kuku. Alikuwa huko kwa sababu watawala wakitaka kumtia adabu kwa msimamo wake kuhusu Zanzibar.

Haya alinieleza katika barua ya kwanza aliyoniletea kutoka jela Julai 1989. Barua hiyo aliyoiandika kwa Kiingereza ilianza kwa kusema:

“Ninakuandikia kutoka jela kuu la Zanzibar, linalojulikana kama Chuo cha Mafunzo. Kama ujuavyo, nilitiwa korokoroni kuanzia Mei 11, 1989. Kisingizio cha kukamatwa kwangu na kutiwa gerezani ni shutuma kwamba nilitayarisha na kushiriki katika mkutano usio halali huko Mchanga Mdogo, Wete, Pemba.”

Maalim aliendelea kueleza kwamba walioizua shutuma hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bwana Pondera, na watu wake. Halafu Mei 23, 1989 akabandikwa mashtaka mingine kwamba alikutikana na nyaraka za siri za serikali.

Julai 19, 1989 upande wa mashtaka uliyaondoa mashtaka hayo kwa mujibu ya Sheria ya Zanzibar na badala yake akashtakiwa kwa mujibu wa Sheria ya 1970 ya Jamhuri ya Muungano.

Katika barua yake, Maalim alieleza kuwa “mashtaka yote haya yamezuliwa ili kuninyamazisha”. Kulikuwa na sababu mbili za kumyamazisha, aliandika. Ya kwanza ni kwamba watawala wakihisi kuwa kwa kumtia ndani wataliua lile dai la Wazanzibari la kutaka pafanywe kura ya maoni ya kuamua juu ya mustakbali wa Muungano.

“Nionavyo, kwa kufanya hivyo, wamekosea. Kwani Zanzibar siyo milki yangu binafsi. (Zanzibar) Ni ya Wazanzibari wote. Nao wana haki ya kujiamulia mambo yao…Kufungwa kwa wale wanaoonekana kuwa ‘viongozi wa upinzani’ hakutowavunja moyo watu walioazimia kuisaka haki yao ya kimsingi ya kuendesha mambo yao!”

Sababu ya pili iliyomchongea akafungwa, aliandika, ni takwa la watawala kujipendekeza kwa Mwenyekiti wa Chama, Mwalimu Julius Nyerere, “aliyewaagiza vibaraka wake walio Zanzibar wawafunge gerezani wote wanaowaona kuwa wanakipinga Chama kinachotawala, CCM”.

Maalim alieleza kuhusu namna Nyerere alivyomdhalilisha Abdallah Kassim Hanga katika mkutano wa hadhara Dar es Salaam, halafu akampeleka Zanzibar alikouawa na mambo ya kisheria kuhusu kesi iliyokuwa ikimkabili. Aliimaliza barua yake, kama kawaida yake, kwa matumaini, akiwa ana hakika kwamba iko siku haki itapatikana.

Desemba 27, 1987 katika uwanja wa Tibirinzi, Chake Chake, Pemba, Maalim aliwaahidi Wazanzibari kwa kusema: “…Nitaendelea kuwatumikia Wazanzibari nikiwa ndani ya serikali au nikiwa nje ya serikali. 

Nitaendelea kuwatumikia nikiwa ndani ya chama au nje ya chama…” Kwa chama hapo alikusudia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika kipindi kifupi ameweza kuwavutia na kuwaunganisha Wazanzibari wa itikadi mbali mbali za kisiasa na wafuasi wa vyama vyote vya siasa vya asilia vilivyowahi kuasisiwa Zanzibar.

Miongoni mwa wafuasi wake wakubwa wamo waliokuwa wanachama wa ASP, wa ZPPP, wa ZNP, wa Umma Party na wengineo wasiokuwa wanachama wa chama chochote. Ameweza kuyaunganisha makabila yote, na watu wa matabaka yote ya kijamii, wake kwa waume.

Katika kipindi hicho hicho ameweza kuunda chama cha kitaifa chenye uzito katika sehemu zote mbili za Muungano wa Tanzania.

Ingawa amekuwa akiziendesha siasa katika mazingira magumu ya wafuasi wake kuhujumiwa na vyombo vya dola au na makundi yanayoungwa mkono na chama kinachotawala, yeye daima amekuwa akihubiri amani.

Mara kwa mara amekuwa akiwasihi wafuasi wake wadai haki zao kwa njia za amani. Hata Jumapili iliyopita alipokuwa akihutubu kwenye mkutano na waandishi wa habari katika hoteli ya Park Hyatt, Kelele Square, Unguja,

Nadhani kilichomfanya awe kiongozi madhubuti ni mambo aliyoyapitia katika maisha yake na misukosuko ya kisiasa aliyokumbana nayo, yakiwa pamoja na kufungwa na kutukanwa matusi ya nguoni na viongozi wa kitaifa wa CCM.

Nafasi haikuturuhusu kuyanukuu maandishi yake kwa ukamilifu lakini naitoshe kusema kwamba kwa mpangilio wake wa maneno, jinsi anavyoyaeleza matukio na anavyotoa hoja msomaji lazima avutiwe na namna anavyotumia mantiki kujieleza. Na hapo, nadhani, ndipo palipo tatizo.

Anapokuwa anajadiliana na mahasimu wake wa kisiasa Maalim huwa pia anatumia mantiki — na uungwana — katika kujaribu kuwashawishi. Huo, ni mfano, ninavyohisi, wa kosa la kutegemea mantiki katika siasa.
Huwa ni kosa hasa pale mtu anapokuwa anajadiliana, anawafahamisha au anashindana na watu wasiotumia akili, majahili wasiojali ukweli, haki na utu.

Hawa ni watu wenye ubahalula wa Juha Kalulu kama wale tunaowaona wakijidanganya wenyewe kwa wenyewe. Wanajidanganya huku wakijuwa kwamba ulimwengu unajuwa kwamba wao wenyewe wanajuwa kuwa wanajidanganya. 

No comments:

Post a Comment